NA
HAJI NASSOR, PEMBA::::
SHAHIDI
nambari moja ambae ni mtoto wa miaka 13, aliyedai kubakwa, ameshindwa kufika
mahakamani kutoa ushahidi, licha kuitwa na mahkama mara saba (7), na kisha mtuhumiwa
kuachiwa huru.
Mtoto huyo pamoja na mama
yake mzazi, walipelekewa wito ‘samos’ wa mahakama mara saba, kuanzisha
Julai 22, na Septemba 21 mwaka huu, ili kufika mahakama ya makosa ya
udhalilishaji kutoa ushahidi, lakini hawakufika.
Mwendesha mashtaka kutoka
Ofisi ya Mkurugenzi wa mashtaka Ali Amour Makame, aliimbia mahakama hiyo kuwa,
mtoto aliyedai kubakwa anakua shahidi nambari moja kisheria.
Alidai kuwa, baada ya
kumpata mtuhumiwa, walianza taratibu za kumuandikia muathirika ‘shahidi
nambari moja’ ili afike mahakamani yeye pamoja na mama yake, lakini
hawakufika hata mara moja.
Wakili huyo wa serikali
alidai kuwa, baada ya kuona mtuhumiwa anasota sana rumande na kesi hiyo
kutokwenda, mbele, aliiomba mahakama kumuachia huru mtuhumiwa, ili akaendelee
na shughuli zake.
Aliiambia mahakama hiyo,
kuwa Ofisi ya Mkurugenzi wa mashtaka haina tena nia ya kuendelea na shtaka
hilo, kwa vile mashahidi waliowategemewa hawafika mahakamani, licha kufikiwa na
wito.
‘’Wito wa mahkama unawafika
kila unapotolewa, na mimi nimekuwa nikiwapigia simu kila wakati, lakini inapofika
siku ya kuendelea na kesi hawafiki mahakamani, naomba mtuhumiwa aachiwe
huru,’’alidai.
Baada ya maelezo hayo,
Hakimu Muumini Ali Juma, alimuuliza wakili wa utetezi, ikiwa ana jambo lolote,
na kudai kuwa wakati umefika kwa mtuhumiwa huyo kuachiwa huru.
Hakimu Muumini alitumia
kifungu cha 103 (a) cha sheria nambari 7 ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai ya
mwaka 2017, kumuachia huru mtuhumiwa huyo.
Awali Hakimu huyo kabla ya
kumuachia huru mtuhumiwa huyo Kombo Mohamed Ali, alimpa nafasi na kuelezea amejifunza nini, wakati alipokua
anatuhumiwa kwa kosa la ubakaji.
‘’Kwa kweli nimeona kuwa,
kesi hizi ni mbaya maana zinaweza kukupeleka eneo ambalo hujalitarajia, hivyo
nitaiasa jamii na hasa vijana wenzangu, kujitenga na makossa haya,’’alieleza
mtuhumiwa huyo.
Hata hivyo Hakimu Muumini,
alimtaka mtuhumiwa huyo kwenda kwa jamii kutoa elimu, juu ya namna ya
kuyaondosha matendo hayo, ambayo yamekuwa mengi.
Awali ilidaiwa mahakamani
hapo kuwa, mtuhumiwa huyo Julai 15, mwaka huu majira ya 6:30 za usiku eneo la
Muhogoni wilaya ya Chake chake, alimbaka mtoto mwenye miaka 13.
Kufanya hivyo ni kosa
kinyume na kifungu cha 108 (1), (2), (e) na 109 (1) sheria ya Adhabu nambari 6
ya mwaka 2018 sheria ya Zanzibar.
Mwisho
Comments
Post a Comment