AMINA AHMED MOH'D-PEMBA.
Waandishi wa Habari Kisiwani Pemba wameaswa kuzidisha
umakini katika utumiaji wa mitandao ya kijamii
ikiwa ni pamoja na kuweka ulinzi katika utumaji wa taarifa zao ili zisiweze kudukuliwa.
Ushauri huo ulitolewa Oktoba 27, mwaka 2022 na
Mwenyekiti wa Klabu ya waandishi wa Habari kisiwani Pemba (Pemba Press
Club) Bakar Mussa Juma
alipokuwa akifungua mafunzo ya siku moja ya Usalama wa Mitandao (Digital Security) kwa
waandishi wa habari wanaotumia zaidi
mitandao ya kijamii katika kazi
zao yaliofanyika katika ukumbi wa Ofisi hizo Misufini Chake Chake.
Alisema mitandao
imekuwa ikipeleka ujumbe kwa haraka zaidi
kwa jamii ukilinganisha na
vyombo vyengine vya habari vilivyopo nchini
lakini kumekuwa na changamoto mbali mbali ambazo kama hawakuwa makini wanaweza
kujiingiza katika matatizo wasio yategemea kwa vile kunaweza kukatokea wahalifu
wakaharibu dhamira zao.
Alieleza kuwa watumiaji wa mitandao wanawajibu wa
kujifunza na kuelewa namna ya kujilinda kwenye
mitandao yao ili isiingiliwe na wahalifu ambapo kunaweza kupelekea kutokuwepo
kwa usalama kwa
waandishi wa habari kutokana na
baadhi ya wahalifu kutumia mitandao hiyo kudukua taarifa pamoja
kufanya uhalifu .
"Kudukuliwa
taarifa kwenye mitandao ya kijamii
aidha za mwandishi mwenyewe lakini hata kazi za kihabari zinazofanywa na
kutumwa katika mitandao , kunaweza kukajitokeza upotoshaji kwa kupata taarifa
nyingi zisizo sahihi ( Fakenews) ambazo hazijafanyiwa uchunguzi wa kina na hivyo kuwa ni chanzo cha matatizo hata
usalama wa nchi “, alisema.
Aidha Mwenyekiti huyo wa Pemba Press Klab aliwataka waandishi hao
kuyafanyia kazi mafunzo watakayopatiwa
juu ya suala hilo la usalama wa mitandao ili kuweza kujiweka salama katika utumiaji wao ambao kwa sasa umekuwa ni
changamoto kwa waandishi wa habari.
"Kujiepusha na
mitandao ambayo haiko salama na
kutofautisha fake news, kutasaidia kuwaepusha kujiingiza kwenye matatizo
musioyatarajia ,ambapo mutafunzwa namna ya kuweza kulinda taarifa zako na
mitandao yenu munayofanyia kazi na hapo mutaweza kufanyakazi bila ya wasi wasi
wowote”, alisisitiza.
Kwa upande wake
Mratibu wa Klabu hiyo ( Pemba Press Club) Mgeni Kombo Khamis aliwataka washiriki wa mafunzo hayo
kufikisha elimu watakayopatiwa kwa
waandishi wengine ambao wamekosa fursa hiyo
kutokana na sababu mbali mbali.
Alisema kuwa utumiaji wa mitandao umekuwa na kasi kubwa
kutokana na uharaka wake, lakini hakuna mafanikio yasiokuwa na changamoto zake
hivyo ni lazima wasiwe wachoyo kuyapeleka mafunzo hayo kwa waandishi wengi
zaidi.
“ Klabu haina uwezo wa kuwakusanya waandishi nyote
munaotumia mitandao ya Kijamii ,lakini kwa umuhimu wake tumeona tuwaite nyinyi
muliohudhuria ili muwe mabalozi kwa wengine
hivyo itumieno fursa hii mulioipata”, alisema Mgeni.
Mratibu huyo aliwataka Waandishi wa habari ambao hadi
sasa hawajaamuwa kujiunga kuwa wanachama wa Pemba Press Club, kufanya hivyo ili
kuweza kupata fursa mbali mbali za mafunzo hususan yanayotolewa na UTPC na
Klabu wenyewe.
Akitoa Elimu ya
Usalama wa mtandao kwa waandishi hao mkufunzi aliepatiwa
Mafunzo hayo na Umoja wa Klab za Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC)
Haji Nassor Mohamed pamoja na mambo
mengine alisema kuwa usalama wa mtandao
ni kujikinga na hatari zinazoweza kujitokeza
kwa watumiaji sambamba na kujilinda na hatari
zilizokusudiwa na wahalifu na zisizokusudiwa kusambazwa.
"Kuna uhalifu katika mitandao ambao umepangwa na ule
uliokuwa haukupangwa yapo mambo mbali mbali usioyahitaji unaweza ukayakuta
katika simu au Komputa yako , masuala ya
kuingilia email ya mtu kumuazima mtu mwengine, afungue, yote hayo ni hatari na
ili ujikinge ni lazima ujue usalama na ulinzi wake "alisema.
Aliwataka waandishi hao kujiengeza zaidi katika kujifunza
mambo mbali mbali yanayoweza kuwa kinga ya kujilinda na udukuzi wa taarifa zao
kwani kumekuwepo na wahalifu wanaotumia mitandao hiyo kwa maslahi yao ama kwa
dhamira ya kumchafuwa mwandishi ama mtumiaji wa mtandao fulani.
Haji Nassor ambae pia ni Mwandishi wa habari wa Shirika
la Magazeti ya Serikali aliwasisitiza waandishi hao kutumia mitandao yao kwa
ajili ya kuihabarisha jamii mambo mbali mbali na sio kwa matumizi ambayo hayana
tija kwa jamii na taifa kwa ujumla ikuchukuliwa kuwa wananchi waliowengi
wanafuatilia kusoma habari za mitandao kila wakati.
“ Waandishi wenzangu ni wambie sio kila anaemiliki
Mtandao ni mjuzi wa matandao hivyo zitumieni simu ama Komputa zenu kujifunza zaidi mambo ambayo
yanaweza kukuweka katika hatari hata ya maisha yako binafsi”, alieleza.
Waandishi hao walipata fursa ya kujifundisha mambo mbalimbali ikiwemo ya usalama wa mitandao ikiwa ni
pamoja na kujikinga dhidi ya hatari (Safety) kujikinga binafsi
ili kuweza kuwa salama katika matumizi ya mitandao kwa vyombo vya
mitandao (Security) .
Hata hivyo walifunzwa juu ya tathmini ya hali ya hatari
pamoja na mbinu za kujua program hatarishi na zisizo hatarishi zinazotokana na
matumizi mabaya ya Mitandao.
MWISHO.
Comments
Post a Comment