NA HANIFA SALIM, PEMBA
UCHUMI wa buluu
ni shughuli za kiuchumi zinazohusu matumizi bora ya rasilimali za bahari kwa
ajili ya kuimarisha au kukuza pato la wavuvi na taifa.
Kuna nafasi kubwa
na nzuri ya kuifanya Zanzibar na Tanzania kwa ujumla kuwa na uchumi mzuri zaidi
kwa kuifanyia maarifa zaidi ‘Blue Economy’.
Elimu na mafunzo katika uchumi buluu inapaswa
kuratibiwa vizuri ili kukuza ukuaji wa sekta ya bahari, kwa hivyo unaweza kutoa
moja ya fursa kubwa zaidi kwa mafanikio ya biashara.
Sio kitu cha ajabu kwa Zanzibar
kusikia neno uchumi wa buluu, ambapo ikiwa na maana kuwa ni shughuli zote za uendelezaji
na ukuzaji wa uchumi kupitia matumizi bora ya rasilimali zote muhimu za bahari.
Dhana nzima ya uchumi wa buluu
ni pana, ambayo imebeba shughuli zote za msingi zinazofanywa katika bahari kama
vile, uvuvi wa aina mbali mbali ikiwemo raslimali zote zitokanazo na bahari.
Ikiwemo uvuvi wa
kibiashara na usio wa kibiashara katika kina kirefu na kifupi cha maji,
shughuli za usafirishaji baharini, shughuli za utafutaji na uchimbaji wa maadini
na mafuta baharini.
Makala hii itazungumzia namna ya upatikanaji wa vifaranga
vya samaki Zanzibar utakavyoimarisha sekta ya uchumi wa buluu kwa wafugaji wa
samaki kwa kuongeza pato la taifa.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali
Mwinyi amesema, kutokana na juhudi kubwa zinazochukuliwa na wafugaji wa samaki
Serikali ina kila sababu ya kuwasaidia kwa kuwapatia mitaji wanayoitaka.
Akiwa kwenye ziara yake aliyoifanya mwezi Julai mwaka huu, ambapo
alipata fursa ya kutembelea kilimo cha ufugaji wa samaki kwa kikundi cha “Siri
fish Farm” Pujini Kibaridi Chake Chake Kisiwani Pemba.
Dk. Hussein anasema, bado kunahitajika nguvu za ziada kutoka
Serikalini kuwasaidia wafugaji wa samaki, hivyo aliitaka wizara inayohusika
kuhakikisha wanawapatia vifaranga kwa muda mfupi ujao.
Iwapo wananchi wataitumia bahari vizuri itawapatia kipato wataondokana
na umaskini kwani kuna shughuli nyingi za kufanya ikiwemo uvuvi, kilimo cha
mwani, ufugaji wa samaki, kamba, majongoo bahari na mengineyo.
“Changamoto zenu ni nyingi tumezichukuwa na kuzifanyia kazi,
tumeambiwa kuna vikundi nane ni vyema tukavisaidia vikundi hivi kuliko
kuanzisha wengine,”anasema.
Anasema, Serikali imekuwa ikiwawezesha wavuvi kwa kuwapatia maboti na
zana za kisasa ili wavue vizuri sambamba na wakulima wa mwani kuwapatia boti za
kubeba mwani wao pamoja na mitaji.
‘’Wananchi wa Zanzibar watakapowezeshwa vizuri katika suala la uchumi
wa buluu, wataweza kuondokana na umasikini, na sasa anaona ulazima wa kusaidiwa
upo,’’.
WIZARA
YA UCHUMI WA BULUU NA UVUVI ZANZIBAR
Waziri wa wizara ya Uchumi wa Buluu na uvuvi Zanzibar Suleiman Masoud
Makame anasema, wizara imeshafikia makubaliano na mwekezaji, ambae ataekeza
uzalishaji wa vifaranga.
Aliwaaminisha wafugaji wa samaki wa Zanzibar, kuwa wamekubaliana awali
mwa mwezi Agost watakuwa wameshasaini mkataba wa utekelezaji.
Baada ya kusaini mkataba huo wa utekelezaji, wanategemea kwamba
changamoto ya vifaranga inayowakabili wafugaji wa samaki kuondoka kabisa.
Anaeleza, wao kama wizara jitihada zao ni kuzalisha vifaranga, jambo
ambalo ndio kipaumbele chao cha kwanza ambavyo vitawawezesha wafugaji kuzalisha
fedha nyingi kupitia shughuli zao wanazozifanya.
IDARA YA
MAENDELEO YA UVUVI PEMBA
Mtaalamu kutoka Idara ya Maendeleo ya uvuvi Pemba Haji Omar Haji,
anasema katika kutengeneza ajira za wananchi imeona ni vyema kuziendeleza
jitihada ambazo wanazifanya siku hadi siku.
Aliwahakikishia wafugaji kwamba, serikali imeshaandaa mpango wa
kuzalisha vifaranga vya samaki utakaosaidia kufikia malengo ya wafugaji hao
ambayo wamejiwekea.
“Niwatoe hofu kuhusu suala la upatikanaji wa vifaranga wafugaji wa
samaki karibuni tatizo hili, linaelekea kutatuka kwani serikali yetu
imeshatenga fedha za mradi huo ambao utakua ni chachu ya mabadiliko kupitia
sekta yetu hii,” anasema.
KIKUNDI
CHA “KICHAKAA SI CHANGI”
Katibu wa Kikundi hicho cha ufugaji wa samaki kilichopo Kiuyu
Minungwini wilaya ya Wete Othman Bakar Shehe anasema, kikundi chao ndio cha
mwanzo kilichoanzisha wazo la ufugaji wa samaki kwa Zanzibar, kikiwa na
wanachama 26.
Upatikanaji wa vifaranga umekua ni tatizo kwao, jambo ambalo awali
walikua wakisaidia kuwapatia hata wenzao ambao waliamua kufanya shughuli hizo
kwa kuwauzia na hata kuwagaia.
Mahitaji yao ya sasa ni kupata vifaranga vya aina tofauti ikiwemo
Sato, Kambare na Mwatiko, ambapo mwanzo walianza na samaki aina moja ya Mwatiko,
ingawa kwa sasa wanalengo la kupiga hatua nyengine kubwa za kiufugaji.
Miongoni mwa changamoto nyengine zinazowakabili ni kufanyiwa
matengenezo makubwa ya shamba lao la kufugia samaki wakati ikiwa hali ya uchumi
walionao kwa sasa ni dhaifu.
Anasema serikali imewaunga mkono sana wafugaji wa samaki lakini bado
wanahitaji elimu ili wafuge kwa kuendana teknolojia ya sasa pamoja na kuwapatia
vifaranga vya aina mbali mbali.
“Tuliamua sisi wenyewe kufuga samaki tulikaa kuwaza wazo
tukakubaliana, tulikwenda serikalini kuomba ruhusa tukaruhusiwa hatukua tumeona
sehemu yoyote ni ubunifu wetu wenyewe,” anasema.
Mabwawa yao ni nane yana ukubwa wa kiwanja kimoja cha mpira, nusu
kiwanja na mengine yana ukubwa mita 25 ambayo yanauwezo wa kuchukua samaki
zaidi ya 8,000 hadi 50,000 kwa wakati mmoja.
KIKUNDI
CHA ‘SIRI FISH FARM’ PUJINI
Mwenyekiti wa kikundi cha ufugaji samaki ‘Siri Fish Farm’ kilichopo
Pujini Kibaridi Ahmed Salum Issa anasema, moja ya malengo yao ni kujiajiri,
kujipatia kipato halali.
Anasema, walijenga matumaini makubwa ya kuengeza mabwawa mapya 12 ya
samaki pamoja na kufanya ukarabati wa kujenga miondombinu, ingawa kwa sasa
wanakabiliwa na ukosefu wa vifaranga.
“Jambo hili lina tunavunjika moyo kwani tunalazimika kufuga samaki
aina ya Mwatiko, ambao vifaranga vyake ni vya kubahatisha jambo linalopelekea
kuwa na idadi ndogo ya samaki na kushindwa kufikia malengo,” anasema.
Mahitaji yao ya sasa ni kupata vifaranga zaidi ya milioni 1, ambavyo
vitakidhi mahitaji yao, kutokana na changamoto hiyo inawavunja moyo kwani idadi
ya samaki walionao ni ndogo ukilinganisha na ukubwa wa shamba lao.
KIKUNDI
CHA ‘MAPAMBANO’ SIZINI
Mwenyekiti wa kikundi cha ufugaji wa samaki cha Mapambano shehia ya
Sizini wilaya ya Micheweni Pemba Khalfan Hamad Khalfan anasema, zaidi ya
shilingi 15 zimetumika kwa ujenzi wa mabwawa yao ya kufugia samaki.
Mpango wao ni kuzalisha samaki wengi kwa ajili ya biashara ingawa wanakabiliwa
na changamoto ya upatikanaji wa vifaranga vya samaki ambavyo vinarejesha nyuma
juhudi zao.
“Tuliingiza samaki zaidi ya 3,500 tuliwachanganya na kamba lakini tulijikuta
tunapata hasara kubwa wakati wa mvua, samaki wengi walipotea kwani hatukua na
taaluma kwamba mvua inaweza kupoteza rasilimali zetu,” anasema.
Mabwawa yao ni 14 ambayo ya uwezo wa kuchukua samaki 40,000 lakini
kinachowarejesha nyuma ni upatikanaji wa vifaranga vya samaki kwa upande wa
Zanzibar nzima.
“Bei yetu kwa kilo moja ya samaki ni shilingi 1000 tunapovua samaki
wetu soko letu linakua kubwa tunaingiza fedha nyingi, faida nzuri na wala
hatupati hasara kwa hii bei,” anasema.
SOKO
Wenyeviti na Makatibu wa vikundi hivyo amesema, suala la soko halina
changamoto kwao kama ilivyo kwa upatikanaji wa vifaranga vya samaki.
Wanasema, endapo serikali itawapatia vifaranga vya samaki ambavyo
vitakidhi mahitaji yao watapiga hatua kubwa kwenye sekta ya uchumi wa buluu
kwao na kwa taifa.
MWISHO.
Comments
Post a Comment