NA
HAJI NASSOR, PEMBA:::
MKUU
wa mkoa wa kusini Pemba, Mattar Zahor Massoud, amesema ana imani na kuiamini kamati
maalum ya maandalizi ya kuelekea kilele cha siku 16 za kupinga ukatili wa
kijinsia kisiwani Pemba.
Alisema, kamati hiyo imejipanga
vyema na kutokana na shughuli ambazo wamezipanga kuzifanya zinaweza kuwa chanzo
kizuri kwa kufikisha ujumbe kwa jamii husika.
Mkuu huyo wa mkoa ameyasema hayo
mbele ya kamati hiyo ofisini kwake mjini Chake chake, wakati akizungumza na
kamati hiyo, kuwasilisha mapendekezo ya shughuli zinazotarajiwa ndani ya siku
16 za kupinga ukatili wa kijinsia.
Alisema, shughuli zilizopangwa ikiwa
ni pamoja na matembezi, makongamano, elimu kwa jamii, vipindi vye redio na tv
ni dhahiri kuwa elimu hiyo itasambaa na kuwafikia walengwa.
Alieleza kuwa, kamati hiyo imelenga
hasa kule ambako serikali imekuwa ikitilia mkazo kila siku, juu ya elimu na
kujadili changamoto katika kutokomeza matendo hayo kwa wanawake na watoto.
‘’Kwanza nichukue nafasi hii
kuipongeza kamati hii ya maandalizi kutokana na maono yenu, ambayo yametoa dira
ya namna ambavyo mtaifikia jamii, tukiwa kwenye shamra shamra za kuelekea siku
16 za kupinga ukatili wa kujinsia,’’alieleza.
Katika hatua nyingine Mkuu huyo wa
mkoa wa kusini Pemba Mattar Zahor Massoud, ameridhia baadhi ya shughuli ambazo
zilipendekezwa kufanywa na kamati hiyo, ikiwa ni pamoja na kuzungumza na vyombo
vya habari na matembezi kama eneo moja la uzinduzi.
Hata hivyo, ameitaka kamati hiyo
kuwasiliana na mkuu wa mkoa wa kaskazini Pemba, ili nae atoe ushauri na
mapendekezo yake, katika kuona shughuli hiyo inanoga.
Mapema Katibu wa kamati hiyo Khalfan
Amour Mohamed, mara baada ya kuwasilisha mpango kazi wa kamati hiyo, alisema
hayo ni mapendekezo ya awali ya kamati.
Alisema, mara baada ya kamati
kukutana, iliamua kumpelekea mapendekezo hayo, ili kwanza ayapate na kisha atoe
ushauri wake katika kufanikisha shughuli nzima.
Hata hivyo Katibu huyo alisema
wameyachukua na kuyafanyia kazi mapendekezo yote yaliotolewa na Mkuu wa mkoa
ikiwa ni pamoja na kuangalia uwezekano wa kupunguza shughuli.
‘’ Ni kweli katika jambo ambalo mkuu
wetu wa mkoa alitushauri na tunaona ni sahihi ni kupunguza shughuli, na hizo
chache ambazo tumezipanga kuzifanya, tuchaguwe wawasilishaji
wanaokubalika,’’alisema.
Mjumbe wa kamati hiyo Tatu Abdalla
Msellem, alisema mapendekezo waliyopewa na Mkuu wa mkoa watayafanyiakazi, maana
yanalengo la kuimarisha shughuli hiyo.
Nae mjumbe wa kamati hiyo Asha Mussa
Omar, alisema watajipanga vyema ili kuona shughuli hiyo inafanikisha kama
walivyokusudia.
‘’Kwanza tunampongeza mkuu wa mkoa
kwa ushauri ambao ametupa katika kuona tunaendeleza shughuli za kuelekea siku16
za ukatili wa kujinsia,’’alieleza.
Siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia ni kampeni ya
kimataifa ya kupinga ukatili dhidi ya wanawake,
ambapo kampeni hii hufanyika kuanzia tarehe 25 Novemba na
kumalizika tarehe 10 Desemba ya kila mwaka.
Siku hiyo ilianza kuadhimishwa rasmi mwaka 1991, siku hii inaongozwa
na Kituo cha
kimataifa cha Wanawake tarehe 10 ilichaguliwa rasmi kuwa siku
ya kilele cha maadhimisho haya ikiambatana na siku ya haki za binadamu duniani.
MWISHO
Comments
Post a Comment