NA
HAJI NASSOR, PEMBA
WANANCHI
kisiwani Pemba, wamewaomba viongozi wa ofisi za umma, kupunguza mikutano ya
ndani ya nje ya ofisi, kwa siku ambazo wamezitenga wenyewe, kwa ajili ya
kukutana na wananchi, kusikiliza malalamiko yao.
Walisema zipo ofisi za umma,
zimejiwekea utaratibu wa kukutana na wananchi kila wiki mara moja au mbili,
ingawa hata kwa siku hizo, imekuwa shida kuwapata.
Wakizungumza na mwandishi wa
habari hizi, walipofika ofisini kulalamika, walisema viongozi wa ofisi za umma,
wamejiwekea utaratibu wa kukutana nao, ingawa kwa baadhi yao imekuwa
changamoto.
Mmoja kati ya wananchi hao
Nassor Salim, alisema wamekuwa wakiitumia siku ya Jumanne na Alhamis, kumfuata
mkuu wa wilaya ya Chake chake, ingwa changamoto ni mikutano isiyokwisha.
āāWakati mwengine, anaingia
kiongozi mwenzake anatumia zaidi ya saa mbili au tatu na sisi tunaendelea
kusubiri bila ya kujua wakati gani tutampata,āāalieleza.
Nae Asha Issa Nassor,
alisema tatizo hilo lilimkumba wiki mbili zilizopita, baada kufika ofisi ya
mkuu wa wilaya ya Chake chake, bila ya kukutana nae.
āāBahati mbaya hata
tulipomuuliza katibu wake muhutasi, alisema Mkuu wa wilaya ametoka kidogo,
ingawa alitimiza saa nne, bila ya kurudi na mimi nikarudi Ndagoni,āāalieleza.
Nao Is-mail Ali Khamis na
Rukia Mohamed Hamad, walisema njia pekee kwa viongozi hao, ni kupunguza safari,
mikutano na vikao na kutumia siku hiyo, kwa ajili ya kuwasikiliza.
Hata hivyo alisema, hata
ofisi ya mkuu wa mkoa kuna siku maalum ya kukutana nae ingawa, mara nyinyi
unaonana na Katibu tawala wake.
āāSisi wananchi shida yetu
ni kukutana na mkuu wa Mkoa, lakini utaulizwa mara mia moja, na mwisho
unaambiwa leo mkuu wa mkoa hayupo, unakutana na Katibu tawala,āāalilamikia.
Mkuu wa mkoa wa kusini Pemba
Mattar Zahor Massoud, alikiri kuwepo kwa changamoto hiyo, na kusema hawapendi
kuwakimbia wananchi, lakini wakati mwengine majukumu huingiliana.
Alieleza kuwa, ni kweli
wakati mwengine viongozi hao wakiwemo wakuu wa wilaya, wamekuwa hawapo ofisini
kwa siku ambazo wamewatengea wananchi, lakini hakuna mwananchi anarejeshwa.
āāNimekuwa nikiwaambia
viongozi wenzangu, kuwa hata siku ambayo sio iliyoko kwenye ratiba, kama
wananchi wapo wawasikilize, na mimi kwenye ofisi yangu, nimetoa maagizo hayo
pamoja na kuweka namba ya simu ya 0733008787 ya kupokea malalamiko,āāalieleza.
Aidha Mkuu huyo wa mkoa
alisema, pamoja na kwamba amejiwekea utaratibu wa kila Jumanne wa kukutana na
wananchi, lakini ameweka utaratibu wa kila mwisho wa mwezi kuzungumza na
wananchi.
āāKila mwisho wa mwezi
huchukua shehia tano za mjini Chake chake kuzungumza nao kwenye mkutano wa wazi,
uwanja Tenis, lengo ni kusikiliza malalamiko ya wananchi,āāalieleza.
Mkuu wa wilaya ya Chake
chake Abdalla Rashid Ali, alisema ni kweli kuwa, kwa baadhi ya wananchi
hulazimika kukosa kukutana nao, kutokana na kuingiliana kwa majukumu.
āāInawezekana siku kama ya
Jumanne na Alhamis ambayo mimi ndio siku za kukutana na wananchi, pengine
nisiwepo ofisini maana hutokezea mizozo baina ya wananchi na hulazimika kuifuatilia,āāalieleza.
Hata hivyo Mkuu huyo wa
wilaya alisema, suala la kukutana na wananchi sio siku mbili pekee, bali hata
Jumapili, kwenye mikutano na jamii na wakati mwengine hata kwa njia ya simu,
fursa hiyo ipo.
Hivyo amewataka wananchi
wanapokuwa na changamoto wasisubiri siku mbili zilizotengwa katika wiki, bali
wakati wowote milango ya ofisi yake, iko wazi.
Kwa upande wa mkuu wa wilaya
ya Micheweni Mgeni Khatib Yahya, alisema baada ya kuona siku moja ya kazi
haikidhi haja kwa wananchi, amejiwekea utaratibu mwengine.
āāKwa sasa kuanzia saa 1:00
hadi saa 3:00 asubuhi kila siku ya kazi, ni muda wananchi na mimi huingia
kazini saa 12:45 asubuhi, ili kuwasubiri wao,āāalifafanua.
Katika siku za hivi karibuni,
ofisi kadhaa za umma zimejiwekea utaratibu wa kila wiki mara moja au mbili,
kukutana na wananchi, wakati kwa Rais wa Zanzibar Dk. Hussein Ali Mwinyi
hukutana na waandishi wa habari kila mwisho wa mwezi.
Mwisho
Comments
Post a Comment