NA HAJI
NASSOR, PEMBA::::
MOJA ya kichecheo
kikubwa cha kujitokeza kwa matendo ya ukatili na udhalilishaji kwa wamafunzi,
ni uwepo wa utitiri mkubwa wa madrassa na unaokosa waalimu na kisha wanafunzi
kujisimamia wenyewe kwa muda mrefu.
Utafiti mdogo uliofanywa na Chama cha waandishi wa habari wanawake
Tanzania TAMWA-Zanzibar kisiwani Pemba, umebaini kuwa, idadi kubwa ya madrassa
inayobeba wanafunzi wengi na kukosa waalimu wa kutosha, ni sababu ya kujitokeza
matendo hayo.
Utafiti huo unaeleza kuwa, zipo baadhi ya Madrassa zenye idadi kubwa
ya wanafunzi, ingawa waalimu ni wachache na kupelekea wanafunzi wenye mkubwa
kuwaongoza wenzao wapendavyo.
Wakizungumza kwenye utafiti huo, katika wilaya ya Chake chake, waalimu
walisema idadi kubwa ya madrassa inayokosa waalimu ni chanzo cha matendo ya
udhalilishaji.
Mwalimu ambae alikataa jina lake kuchapishwa, alisema haiwezekani
madrassa kuwa na wanafunzi 80, lakini kuongozwa na waalimu wawili.
Mwengine alisema, hao idadi ndogo ya waalimu waliopo katika baadhi ya
madrassa hawana muda mkubwa wa kukaa na wanafunzi, jambo linalopelekea
wanafunzi waliopo kujiongoza.
“Kama waalimu muda mrefu hawapo, huwa ni fursa chafu kwa wanafunzi
kujiingiza kwenye matendo maovu, hivyo ni jukumu la jamii kulijiua
hilo,’’alieleza.
Kwa upande wake mwalimu mkuu wa Madrassa iliyopo soko la Tibirinzi
wilaya ya Chake chake Walid Muhsin Juma, alisema suala la waalimu kujiingiza
kwenye vitendo vya udhalilishaji kwa wanafunzi wao, ni tabia ya mtu na sio kwa
idadi kubwa ya wanafunzi.
“Kama mwalimu hajielewi na hawezi kudbiti matamanio yake, hata kama
hayupo madrassa, anaweza kujiingiza kwenye matendo hayo,’’alieleza.
Afisa Miskti na madrassa kutoka Afisi ya Mufti Pemba Abdull-latif
Abdalla Salum, alisema wamekuwa wakijitahidi kutoa elimu ya madhara ya matendo
hayo kwa wasimamizi wa nyumba za ibada na madrassa.
Alieleza kuwa, wamekuwa na miongozo maalum kwa waalimu na hata
madrassa yenyewe, kabla ya kuisajili, ili kujiridhisha kwa lengo la kuwalinda
wanafunzi.
“Ofisi ya Mufti kila wakati inazitembelea madrassa na kuwaelezea
athari ya waalimu kujihusisha na matendo ya ukatili na
udhalilishaji,’’alieleza.
Mzazi Issa Haji Omar na mwenzake Asha Muhsin Is-mail wa Chake chake
walisema, bado Ofisi ya Mufti inatakiwa kuwa imara kabla ya kuanzishwa kwa
madrassa.
Utafiti umebaini kuwa, hadi mwezi August mwaka huu, kisiwa cha Pemba
pekee kina Madrassa 814 zilizosajiliwa na Ofisi ya Mufti, ambapo ni wastani wa
madrassa 204 kwa kila wilaya, kati ya wilaya nne za Pemba.
Wilaya ya Wete inazo madrassa 190, Mkoani 155 na wilaya ya Micheweni
inazo jumla ya madrassa 170 na Chake chake 299 ambazo zimesajiliwa ramsi.
Mratibu wa TAMWA Zanzibar ofisi ya Pemba Fat-hya Mussa Said, amesema
wapo baadhi ya waalimu wa madrassa kwa kule kukosa kwao maadili, wamekuwa wakijihusisha
na matendo hayo.
‘’TAMWA imeshakutana na waalimu mara kadhaa kuwapa elimu ya athari ya
matendo hayo, ingawa bado hali inaendelea kutisha kwa baadhi ya
madrassa,’’alieleza.
Hata hivyo amewakumbusha wazazi na walezi, wasikubali matendo hayo
kuyafanyia sulhu, na badala yake washirikiane na vyombo vya sheria
kuyatokomeza.
Mkuu wa mkoa wa kusini Pemba Mattar Zahor Massoud, aliitaka Ofisi ya
Mufti kuwachukulia hatua za kinadhamu mara maoja, waalimu wanaojihusisha na
matendo hayo.
Mkurugenzi wa Tumaini Jipay Pemba Tatu Abdalla Msellem, alisema
uanzishwaji ovyo ovyo wa madrassa na waalimu wenye umri mdogo, ni moja ya
vyanzo vya kujitokeza matendo ya udhalilishaji.
Mwanafunzi mmoja aliyewahi kubakwa na mwalimu wake Pujini wilaya ya
Chake chake, amesema kama adhabu itaendelea kutolewa ndogo, matendo hayo
yatendelea kunawiri katika jamii.
Mei 16 mwaka 2022, Mahakama ya mkoa Chake Chake, ilimuhukumu kwenda chuo cha mafunzo
miaka 15 mwalimu wa Madrassa kutoka shehia ya Mchakwe Mwambe wilaya ya Mkoani Ali
Ussi Simai mwenye miaka 25, baada ya kupatikana na hatia ya kumbaka mwanafunzi
wake, mwenye miaka minane (8), kosa hilo alilitenda Novemba 28 mwaka 2021.
Oktoba 4, mwaka
2021 Ofisi ya Mufti Zanzibar ikiongozwa na Katibu wa ofisi hiyo sheikh Khalid
Ali Mfaume, ilifika kwenye madrassatul-bisimmillah Unguja, kufuatilia tukio
ulawiti la mwanafunzi alilofanyiwa na mwalimu wake Ali Abdalla Ali na kisha
kuifunga madrassa hiyo.
Aidha mahkama ya
mkoa Mwera, ilimfunga miaka 80 chuo cha mafunzo mwalimu wa madrassa miaka (21),
na faini ya shilingi milioni 3, baada ya kutiwa hatiani kwa kosa la kumbaka
mwanafunzi wake mwenye miaka 15.
Mwisho
Comments
Post a Comment