Na Mwandishi wetu OMKR
Mwenyekiti wa Nuru Foundation Mama Zainab Kombo Shaib
ambae pia ni mke wa Makamu wa Kwanza wa Rais amesema Jumuiya yao imeamua kujikita
zaidi kumuangalia mtoto wa aina yeyote hasa yatima na anaeishi kwenye mazingira
magumu
Ameeeleza hayo wakati alipofanya ziara ya kuwatembelea
watoto wenye vichwa maji na mgongo wazi katika kituo chao cha nyumba ya
matumaini iliyopo eneo la Mwanakwerekwe ndani ya Wilaya ya Magharibi B.
Mama Zainab amesema kumlea mtoto mwenye kichwa maji na
mgongo wazi kunahitaji elimu kwa mzazi na walezi ili kufahamu namna ya kumlea
hatimae nae mtoto akuwe katika mazingira mazuri yaliyo salama katika hali zote
Ameahidi kuwa taasisi ya Nuru Foundation ina kila
sababu kuona inawasaidia kielimu kwa kutafuta njia za kupata ufadhili na kupata
vifaa visaidizi pamoja na kumuandaa kisaikolojia mama au familia yenye mtoto
mwenye ulemavu wa aina hii ili waweze kujikomboa na kujihudumia kiuchumi.
Aidha amesema kuwa Taasisi ya Nuru Foundation pia ina
jukumu la kumuwezesha mwanamke ambae kwa kawaida ndie mlezi anaekuwa karibu
sana na watoto hivyo taasisi hio itaanza rasmi kutoa mafunzo kwa akina mama
wenye watoto wenye ulemavu na mazingira magumu ili waweze kuwa na mipango
mizuri ya kujiinua kimaisha.
Mwenyekiti huyo wa Taasisi ya Nuru Foundation ameikumbusha
jamii kuwa na utamaduni wa kubadili matumizi ya vyakula na kuzingatia ulaji
vyakula vyenye afya ili kulinda afya ya mwili hasa kwa akina mama wanapokuwa
wajawazito na
Pia amewakumbusha akina baba kuwa karibu na wake zao
hasa wakati wa ujauzito pamoja na kusaidiana ulezi mama anapojifungua kwani
mtoto ni mtoto ila mwenye ulemavu anahitaji uangalizi zaidi
Nae Katibu wa Umoja wa wenye vichwa maji na mgongo
wazi ndugu Hussein Moh’d Saleh ameishukuru Taasisi ya Nuru Foundation kwa kuwa
ni taasisi ya mwanzo kuwatembelea na kutoa msaada ambao kwa sasa wanauhitaji
Hussein amesema nyumba ya matumaini inahitaji
ushirikiano mkubwa na Serikali, jamii na taasisi zisizo za kiserikali na
wafanya biashara ili kuweza kutatua kwa pamoja changamoto zinazowakabili
ikiwemo pempas, suala elimu, vifaa visaidizi, chakula, wataalamu na kuandika
miradi
Nao akina mama na walezi wa watoto wenye vichwa maji
na mgongo wazi wameelezea changamoto wanazozipata kutoka kwa wanajamii ikiwa ni
pamoja na kudharauliwa na familia, majirani, watoto kupewa majina mabaya na
kuachika kwa waume
“siku moja alikuja jirani yangu kuniangalia akaniuliza
nimeambiwa umezaa mtoto mlemavu nikamwambia ndio lakini baada kumuona
akaniambia huyo si mtoto ni jini niliumia sana sana”alisema mama huyo ambae
hakutaka jina lake kutajwa.
Kina mama hao wamesema bado jamii hawajaelewa kuhusu
watoto wenye ulemavu wenye vichwa vikubwa na mgongo wazi hivyo wameomba jamii
wapatiwe elimu ili kuondosha unyanyapaa na dharau.
Kikao pia kilihudhuriwa na Katibu wa Umoja huo Omar
Kaiza Omar ambapo Mama Zainab amekubali kuwa mlezi wa umoja huo na kukabidhi
zawadi ya Box 20 za mchele lishe na Pempas kwa ajili ya wale wanaofika katika
nyumba yao mara wanapotoka hospitali baada ya kupata matibabu katika hospitali
ya Mnazi Mmoja na wale wanaosubiri matibabu
Comments
Post a Comment