NA HAJI NASSOR-PEMBA
+255777 870191
email: kakahaji2016@gmail.com
WANANCHI wa Zanzibar 40, kati ya kila 100, wamejiajiri moja kwa moja kupitia sekta ya kilimo na vivyo hivyo 70 kati ya kila 100 wanategemea kilimo moja kwa moja kwenye maisha yao ya kila siku, kama ilivyothibitishwa ofisi ya Mtakwimu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar mwaka 2016/2021
Ndio maana mwaka wa fedha 2016/2017 sekta hii ilichangia asilimia 25.7
ya pato la taifa na ilikua kwa asilimia 5.7 ikilinganishwa na asilimia 2.5 ya
mwaka 2015/2016.
Kutokana na umuhimu wa sekta hiyo, kwa uchumi wa nchi na
ustawi wa wananchi, Wizara ya Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi, ina dhima
kubwa ya kuhakikisha inawawezesha wakulima wote ili kufikia malengo.
Wizara hiyo lazima iweke mikakati maalum kwa ajili ya
uzalishaji wa mpunga hapa Zanzibar, kwani ndicho chakula chenye kutumiwa na
kupendwa zaidi na sehemu kubwa ya jamii ya Wazanzibari.
Tunapozungumzia mpunga ambao unazalisha mchele wenye kutoa
chakula kinachoitwa wali ambao unaweza kupikwa kwa staili mbalimbali na hivyo
kubadilishwa majina baada ya kuitwa wali utaitwa ubwabwa, pilau au biriyani, si
chakula chenye kupendwa Zanzibar pekee.
Ukitembelea nchi za mashariki ya mbali kama vile China,
Japan, Myanmar, Thailand, Singapore, Laos, Vietnam na nchi nyengine za ukanda
huo, ratiba ya siku ya chakula katika familia haikamiliki kama wali haupo
mezani.
Pamoja na wazanzibari kuzalisha mpunga kupitia mabonde yake
maarufu kama Cheju, Kibokwa na Kirombero, mabonde ambayo kwa hakika yana ardhi
inayoweza kutosheleza uzalishaji kwa matumizi ya ndani na hata kusafirisha nje
ya nchi, hata hivyo bado Zanzibar inaagiza mchele kutoka nje ya nchi.
Kwa mujibu wa takwimu, Zanzibar ina upungufu wa tani 64,000
za mchele kwa mwaka katika mahitaji halisi ya tani 80,000, ikiwa na maana
kwamba wastani wa uzalishaji wa mchele ni tani 16,000.
Tunachokiangalia zaidi kwenye makala hiini kwanini Zanzibar
isijitosheleze kwa chakula wakati ina mabonde makubwa na yenye rutuba
yanayoweza kuzalisha chakula na kujitosheleza kwa mahitaji ya ndani ya nchi.
Katika kuliangalia kwa undani suala hilo, nimelazimika
kukutana na wadau kadhaa wa uzalishaji wa mpunga wakiwemo wakulima na mamlaka
zenye jukumu la kusimamia kilimo hapa nchini.
WAKULIMA
Wakizungumza na mwandishi wa makala hii katika mahojiano
maalum, baadhi ya wakulima katika bonde la Bumbwisudi wilaya ya Magharibi ‘A’
Unguja, wanasema licha ya serikali kuweka miundombinu ya umwagiliaji, bado
wanakabiliwa na changamoto nyingi ikiwemo pembejeo na wataalamu.
Mmoja wa wakulima hao, Suleiman Aman mwenye umri ya miaka
60, mkaazi wa Bumbwisudi, anaelima nusu ekari ya mpunga, anasema tatizo la
pembejeo linasababisha mavuno kutokuwa mazuri.
“Kwa mfano, baadhi ya msimu ikiwa mavuno mazuri anavuna hadi
kilo 700 za mpunga, lakini mara nyengine navuna kilo 300 tu kwa sababu ya
kukosa pembejeo,” anasema.
Mkulima mwengine wa bonde hilo aliejitambulisha kwa jina la
Hadha Hamid Khamis (58) mwenyeji wa Bumbwisudi, anasema anajishughulisha na
kilimo cha mpunga kwa zaidi ya miaka 35 sasa.
Anasema, changamoto kubwa inayowakabili wakulima wa bonde
hilo ni pembejeo ambazo hazipatikani kwa wakati, hali ambayo inasababisha
mavuno kutokuwa mazuri.
Kwa mfano, anasema msimu ambao pembejeo na maji yanapatikana
kwa wakati anavuna hadi tani mbili za mpunga vyenginevyo, uzalishaji hushuka
hadi robo tani.
“Natumia zaidi ya shilingi 500,000 kila msimu kwa maandalizi
ya kilimo hiki, lakini kwa sababu ya kukosekana pembejeo au kutopatikana kwa
wakati na wakati mwengine maji kuchelewa kupatikana fedha hizi zinakuwa
zimepotea bure,” anasema.
“Shamba lenye ukubwa wa robo ekari tunalimisha shilingi
30,000 kwa ajili ya umeme wa kusukumia maji na kama mvua zitakuwa ndogo, gharama
hizi huongezeka mbali ya fedha za ununuzi wa pembejeo na kulimiwa,” anasema.
Mkulima mwengine Amina Juma Kheir, anaelima kwa kutegemea
mvua katika bonde hilo, anasema anakabiliwa na matatizo makubwa hasa kipindi
ambacho mvua zinakosekana.
Mbali ya mvua, anasema tatizo jengine ni pembejeo kupatikana
kwa wakati.
Mwandishi wa mahaka hii, pia alifanya mahojiano na wakulima
wa bonde la Cheju wilaya ya Kati Unguja, wanaolima kwa kutegemea mvua.
Bonde hili ambalo ni miongoni mwa maeneo yanayotegemewa kwa
kilimo cha mpunga Zanzibar, lina miundombinu ya umwagiliaji, lakini sio eneo
lote, hali hii inawafanya wakulima wengi kuendelea kutegemea mvua.
Abdilahi Abdi Hisabu (28) mkaazi wa Jendele, analima eneo
hilo kwa miaka saba sasa. Anasema kilimo cha kutegemea mvua ni kigumu tofauti
na umwagiliaji. Anasema eka moja anayolima, anapata kilo 250 tu za mpunga
wakati mvua zinapokuwa nzuri, ambazo hazitoshelezi kwa mahitaji ya chakula.
Hata hivyo, anapokosa pembejeo na mvua kutonyesha, anapata
chini ya kilo 100, wakati gharama anazotumia kuandaa kilimo hicho hazipungui.
“Ninalipa shilingi 60,000 kulimiwa kwa trekta, lakini pia
kuna gharama za pembejeo, sasa mvua zinapokosekana napata hasara kubwa kwa
sababu sina ninachokipata,” anasema.
Mkulima Juma Ibrahim Juma (60) mkaazi wa Ndijani, mwenye watoto 9 wanaotegemea anasema
anavua hadi kilo 600 za mpunga kwa msimu, lakini anapokosa pembejeo na mvua
anapata chini ya kilo 200.
Anasema changamoto kubwa ipo katika pembejeo kwani
inapatikana kwa bei kubwa na uwezo wao ni mdogo.
“Natumia mbolea za aina mbili, moja nanunua shilingi 15,000
na nyengine shilingi 75,000, kwa mimi mwenye ekari moja natakiwa nitie dawa
lita nne kwa shilingi 40,000, gharama hizi ni kubwa na uwezo wetu mdogo,”
anasema.
Fatma Simai mkaazi wa Jendele mwenye watoto sita, anaelima ekari moja, anasema
kilimo cha juu mapato yake ni kidogo na kina matatizo mengi.
Anasema ekari anapata kilo 400 za mpunga lakini akilima
kilimo cha umwagiliaji ambacho analima robo eka, anapa hadi kilo 700.
“Natumia gharama nyingi kwenye kilimo cha juu lakini mapato
madogo tofauti na umwagiliaji,” anasema.
Akizungumzia umeme anasema robo ekari analipa shilingi
30,000 kwa ajili ya umeme wa kusambazia maji kwenye mashamba.
Pia gazeti hili lilifika bonde la Kibokwa wilaya ya
kaskazini ‘A’ Unguja, ili kubaini changamoto zinazowakabili wakulima.
Mkulima Haji Pandu Khamis (60) mwenye watoto wanne na wake wawili ambae analima robo eka kwa
zaidi ya miaka 30, anasema kilimo cha umwagiliaji hakina shida muhimu mkulima
awe na pesa za kununulia pembejeo na gharama nyengine.
“Mimi nalipa shilingi 30,000 za umeme, kulimiwa shilingi
60,000 na gharama nyengine za pembejeo, hadi navuna natumia kama shilingi
500,000,” anasema.
“Lakini navuna hadi kilo 800 za mpunga kama hali ya hewa
itakuwa nzuri lakini kama hali itakuwa mbaya navuna chini ya kilo 300,” anasimulia.
JUMUIYA ZA WAKULIMA
Mjumbe wa jumuiya ya wakulima wa Cheju, Abdu Hisabu Zidi,
anasema kazi kubwa ya jumuiya ni kusimamia wakulima.
Anasema bonde hilo lina eka 3,020 za umwagiliaji na kilimo
cha juu ambazo zinatumiwa na wakulima kutoka maeneo mbali mbali ya Unguja.
Hata hivyo, anasema wakulima katika bonde hilo wanakabiliwa
na changamoto nyingi ikiwemo pembejeo, ushauri kutoka kwa wataalamu
kutopatikana kwa wakati na matrekta kuchelewa.
“Haya ndio matatizo makubwa yanayorejesha nyuma juhudi za wakulima
hapa,” anasema.
“Kama bonde hili litaimarishwa kwa kuwekwa miundombinu ya
umwagiliaji na kulimwa kitaalam, tatizo la kuagiza mchele litaondoka,” anasema.
Mjumbe wa jumuiya ya wakulima wa bonde la Kibokwa, Haji
Pandu Khamis, anasema bonde hilo lina hekta 133 na wakulima 350 kati ya hao 150
ni wanaume na 200 wanawake.
Anasema kazi ya jumuiya hiyo ni kuwashajiisha wakulima
kusafisha misingi ili maji yapite vizuri pamoja na kufuatilia matatizo
yanayowakabili.
“Tukimaliza mavuno tunakutana ambapo kila mkulima anachangia
shilingi 2,500 kila mtu kwa ajili ya kufanyia matengenezo mashine na misingi,”
anasema.
Aidha alitumia fursa hiyo kuitaka serikali kuifanyia
matengenezo misingi ya ndani kujengewa kwa matofali ili iweze kukaa kwa muda na
kuhifadhi maji kwa muda mrefu zaidi.
WATAALAMU WA KILIMO
Bwana shamba aliyejitambulisha kwa jina la Juma Ame Ame,
anasema hali ya kilimo ipo vizuri, kwani wizara inajitahidi kuwasaidia wakulima
Unguja na Pemba.
Anasema elimu inatolewa kwa wakulima kuhusu kilimo bora
chenye tija na kupunguza gharama za kupatikana pembejeo.
WIZARA YA KILIMO
Mkurugenzi wa kilimo, Mohammed Khamis Rashid, akizungumzia
uzalishaji wa mpunga na kama unasaidia kupunguza uagizaji mchele nje ya nchi,
anasema hali ya uzalishaji bado haijatengemaa kutokana na mabadiliko ya hali ya
hewa.
“Uzalishaji unapanda na kushuka kwa sababu ya mabadiliko ya
hali ya hewa,” anasema.
Tatizo jengine anasema ni upatikanaji wa pembejeo na
wakulima kutotumia mbinu za kitaalamu.
Aidha anafahamisha kuwa kutokana na hali hiyo maranyingi
hutokea kwamba kinachozalishwa huwa hakikidhi mahitaji ya wananchi.
“Ili kukabiliana na matatizo haya, wizara inafanya jitihada
kadhaa ikiwemo kununua pembejeo, wakulima kupewa elimu ili kuongeza
uzalishaji,” anasema.
“Changamoto tuliyonayo maeneo mengi yanategemea mvua, hivyo
kutokana na hali ya hewa kubadilika mara kwa mara wakulima wanapata hasara,”
anasema.
Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi,
Maryam Abdalla Juma, anasema lengo la serikali ni kulima eka 33,350, hata hivyo
hadi 2017 wamelima eka 29,016.9 za mpunga.
Akizungumzia uzalishaji anasema 2013 mpunga wa juu tani
24,651 zilivunwa na umwagiliaji zilipatikana tani 9,003.15. Hata hivyo, anasema
uzalishaji ulishuka mwaka 2014 ambapo tani 21,679.50 zilipatikana kwa kilimo
cha juu na tani 7,884.50 kwa kilimo cha umwagiliaji.
“Lakini kwa 2015 kilimo cha juu uzalishaji ulishuka zaidi
hadi kufikia tani 18,477.65 na kilimo cha umwagiliaji uliongezeka hadi tani
10,605.05 na 2016 kilimo cha juu tulivuna tani 3,589.00 na umwagiliaji tani
754.80 na 2017 tulipata tani 35,791.33 kwa kilimo cha juu na umwagiliaji tani
3,891.35,” anasema.
Anasema maeneo yaliyoongoza kuzalisha mpunga katika kipindi
hicho niChake Chake, Wete na Mkoani kisiwani Pemba.
SULUHISHO
Wakizungumzia suluhisho la changamoto zilizopo katika
ukulima wa mpunga, wakulima hao walisema katika kuelekea kwenye kilimo cha
mpunga ambacho kitaweza kupunguza utegemezi wa mchele kutoka nje ni vyema sana
mabonde ya kilimo yakawekewa miundombinu ya ukulima wa umwagiliaji maji.
Abdilah Abdi Hisabu na Juma Ibrahim Juma wanasema, kwa
kutumia njia hii wakulima wataweza kulima zaidi ya mara mbili kwa mwaka kuliko
kilimo cha kutegemea mvua ambacho hulimwa mara moja kwa mwaka.
“Umetembelea hili bonde letu la Cheju nadhani umejionea, ni
asilimia ndogo sana linatumiwa kwa kilimo cha umwagiliaji maji wakati eneo
kubwa linalimwa mpungwa wa kutegemea mvua.Hali hii haitaweza kutufikisha
tuendako kwani wakati mwengine jua linakuwa kali mpunga unakauka”, alisemaJuma
Ibrahim Juma kutoka Ndijani.
Naye Abdilah Abdi Hisabu mwenye watoto wawili anasema wakulima wa mpunga wa
Zanzibar wanaweza kupunguza tatizo la uagizaji mchele kutoka nje, hata hivyo ni
muhimu kwa serikali kuhakikisha pembejeo zinapatikana kwa wakati.
Anasema pembejeo za kilimo zikipatikana
kwa wakati, kama vile dawa za kuulia wadudu na magugu, uzalishaji wa mpunga
utaongezeka maradufu.
“Wakati mwengine mpunga huingiliwa na wadudu, tunaomba dawa lakini zinachelewa kufika,” walisema.
Aidha alipendekeza matumizi ya teknolojia kwenye kilimo
tofauti na hivi sasa wanalima mpunga kama walivyolima wakulima wa miaka 40
iliyopita.
Wakulima hao pia walishauri iwepo mipango ya kupunguziwa bei
za pembejeo hasa ikizingatiwa kuwa zinauzwa kwa bei kubwa na hali zao za maisha
ni ngumu kwani ni watu wa kutegemea kilimo tu.
Suluhisho jengine walilolitoa katika kufanikisha Zanzibar
kujitegemea kwenye uzalishaji wa mpunga na kuondokana na uagizaji mchele kutoka
nje ni matumizi ya teknolojia na zana za kisasa za ukulima.
“Nadhani unaniona nimeshapiga makoongo ya kupandia mpunga saivi naufukia kwa kutumia matawi ya miti, hii njia ya kizamani ambayo haina tija na isiyoleta ufanisi. Tunahitaji tekonolojia za kisasa za ukulima ili tuondokane na utegemezi,” anasema.
mwisho
Comments
Post a Comment