NA
HAJI NASSOR, PEMBA::::
WANAHARAKATI
wa haki za watoto kisiwani Pemba, wamewataka wazazi na walezi, wanaomiliki
nyumba zilizozungushwa kuta ‘fens’ kuwapa muda watoto wao kuchangamana na wenzao,
ili kucheza pamoja, ikiwa ni sehemu moja wapo ya kukuza ubongo wao.
Walisema, njia moja na rahisi ambayo haihitaji gharama
katika kumkuza mtoto ni kumpa haki ya kucheza na wenzake wasioishi pamoja, ili
kupata habari na matukio ya mtaani.
Wakizungumza na mwandishi wa habari hizi juu ya njia
rahisi ya kukuza ubongo wa mtoto, wanaharakati hao walisema, wazazi wasipokuwa
makini wanaweza kudumaza akili na ukuaji wa watoto wao.
Walisema, akili ya mtoto haijengwi kwa chakula bora, gari
ya kwendea skuli, uzuri wa nyumba pekee tu, bali njia nyingine rahisi ni kuwapa
fursa watoto, kuchangamana na wenzao katika michezo mbali mbali.
‘’Inawezekana wazazi wanamaisha mazuri na nyumba kubwa
yenye ukuta na mbwa mkali, lakini kama mtoto hawakumtoa nje kucheza na wenzake,
atanyemelewa na udumavu wa kuduma,’’alieleza.
Mwanaharakati Aisha Hemed Khamis wa Chake chake, alisema
mtoto anapopata taarifa kutoka nje ya nyumba yao, huwa rahisi kutanua akili na
ufahamu wake mara moja.
‘’Kadiri mtoto anapochangamana na wenzake wa nyumba za
jirani au mtaa wa pili, na ufahamu wake ndivyo unavyoongezeka mara dufu,’’alisisitiza.
Afisa Ustawi wa Jamii wilaya ya Chake chake Rashid Said
Nassor, alisema wazazi waliowengi wenye uwezo, wanadhani ni dhambi kubwa, watoto
wao kuchangamana na kucheza na watoto wengine.
Alieleza kuwa, kadiri mtoto anavyokwenda masafa yenye
usalama kwa ajli ya kucheza na wenzake, vivyo hivyo na akili yake hupanuka kwa
haraka.
Mkuu wa wilaya ya Chake chake Abdalla Rashid Ali, akizungumza
hivi karibuni, aliwataka wazazi na walezi pamoja na kuwapa fursa watoto wao
kucheza na wengine, hata wao wajitengee muda kushirikana kwa michezo.
‘’Ipo michezo kama vile mdako, kupigana mito, mpira,
kurusha chungwa, kupangwa kokoto kwa mfumo wa picha na kung’waruziana macho kwa
njia ya kutishana mzazi na walezi wanaweza kucheza na watoto kama sehemu ya
uchangamshi,’’alieleza.
Nae Mkuu wa Idara ya
Ustawi wa Jamii Pemba Omar Mohamed Ali, amesema haki ya kucheza kwa
mtoto, inatambuliwa na sheria ya mtoto nambari 6 ya mwaka 2011, hivyo ni wajibu
kwa wazazi kuitekeleza kwa vitendo.
‘’Sheria inataka watoto
wapewa haki ya kucheza na wenzao, sasa kama kuna wazazi wanafungia kwenye
mageti, wanaweza kuwa chanzo cha kusinyaa kwa akili yao.
Nae Msimamizi wa kitengo cha lishe Wilaya ya Chake Chake, Harusi Masoud Ali,
akizungumza hivi karibuni, amewakumbusha wazazi na walezi, kuwapatia lishe bora
watoto wao.
Waziri wa Afya Zanzibar Nassor Ahmed Mazrui, alisema yapo
mambo ambayo jamii wanatakiwa kuyafanya, ili kuwa na kizazi bora cha hapo
baadae.
‘’Ni nafasi kwa wazazi na walezi, pamoja na kuwapa haki
watoto wao kushiriki michezo mbali mbali, lakini wajenge utamaduni wa
kuwashauri watoto kwa mambo yanayowahusu,’’alieleza.
Mzazi Is-mail Ali Juma, amekiri kuwa, wamekuwa wakiwafungia
watoto wao kwenye kuta ‘fens’ kutokana na uwepo wa majanga kadhaa kwa watoto.
‘’Mtoto ukiwa humuoni dakika 30, tayari wasi wasi, sasa
mimi huwafungia, lakini pia huwatoa nje kucheza nawenzao pale nikiwepo,’’alieleza.
Mjumbe wa baraza la watoto shehia ya Mwambe Hija Omar Ussi na mwenzake wa Mkoani Hamida Issa Machano, waliwakumbusha wazazi kuwa, suala la kucheza kwao halina mbadala.
Nae Aisha Haji Mohamed wa Machomane Chake chake, alisema
huwa wanafanya hivyo, ingawa kwa ule muda ambao wazazi wapo nyumbani.
Muwezeshaji
kwenye mafunzo ya Kitaifa ya Sayansi ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya
Mtoto ‘SECD’ Everlyne Okeyo, yaliofanyika mkoani Dodoma Tanzania anasema,
watoto wanakosa ukuaji mzuri wa kutengeneza ubongo wao, kwa kule wazazi kutowapa
muda nafasi ya kucheza.
Katika
hatua nyingine, Everlyne alisema, ubongo wa binadamu una nyuroni bilioni 100,
na ndio maana mtoto mara anapozaliwa, huwa na asilimi 25 ya ubongo wake ni mtu
mzima.
‘’Mtoto
anapofikia mwaka mmoja, hufikia asilimia 60, wakati miaka miwili huwa na
asilimia 75 na kuanzia miaka minne hadi sita, hubeba asilimia 90 ya
uwelewa,’’alieleza.
Akizungumza kwenye ufunguzi wa mafunzo hayo, Waziri wa Maendeleo
ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum wa Tanzania bara Dk. Dorothy
Gwajima, aliwataka waandishi wa habari, kuifikisha kwa jamii, dhana ya malezi
ya kisayansi ‘SECD.
Mwisho
Comments
Post a Comment