HABIBA ZARALI,
PEMBA::::
MAENDELEO ni
mabadiliko yanayoonekana kuimarisha katika nyanja mbali mbali za maisha,
ikiwemo za uchumi, sayansi, historia, falsafa na hata za kijamii.
Kupitia msemo wa mjenga nchi ni mwananchi na nvunja nchi ni
mwananchi, inaonesha dhahiri kuwa, hali nzuri ya upatikanaji wa huduma na
nyenzo zilizo bora, haziwezi kuja wenyewe bila wananchi kuwa na utayari.
Kwa maana hiyo basi, ulipaji wa kodi, utowaji na kudai risiti
unapouza na kununua bidhaa, ni moja ya utayari huo wa kufikia maendeleo endelevu
ya nchi.
Kodi hiyo Serikali, imekuwa ikiitegemea kujipatia mapato yake,
hutekeleza miradi mbali mbali huduma za kijamii ikiwemo afya, elimu, maji safi
na salama, miundo mbinu ya umeme, barabara na nyengine ambazo ni muhimu kwa
wananchi.
Ni dhahiri kwamba, kwa sasa dunia imo kwenye katika mabadiliko
ya sayansi na teknolojia, jambo ambalo linatufanya na sisi tuwe macho, ili
tusibakie nyuma na mabadiliko hayo.
Zanzibar kama ilivyo nchi nyengine, zinazoendelea duniani, mbali
na rasilimali walizonazo, lakini kodi inaendelea kubaki kuwa ni chanzo muhimu
katika kujipatia mapato ambayo huleta maendeleo.
Kwa vile Serikali ina dhamana kwa wananchi wake imeweka vipau mbele
kadhaa, ikiwemo vya ulipaji kodi kwa hiari kwa kutumia mashine za kielektroniki,
bila ya kumpendelea mtu yoyote.
Kwa maana hiyo, Serikali imechukua hatua ya kutangaza utoaji wa
risiti za kielektroniki (VFMS) wala haikuwa na nia mbaya ya kuwakandamiza
wafanyabiashara ama kuwaumiza wananchi wake.
Bali bali ni kuhakikisha inadhibiti mapato na kuimarisha huduma
za kimaendeleo ambazo ndio ndoto ya wananchi wake.
Kifungu cha 23 (1) cha Sheria ya usimamizi wa kodi (TAPA)
kinamtaka kila mlipa kodi ambae anauza bidhaa ama huduma kwa fedha taslim au
mkopo ni lazima ampe mteja wake ankara ya kodi au risiti.
WANANCHI WANASEMAJE
Ali Mohamed Ali wa Mkoani na Asha Kombo Bakar wa Mwambe wanasema,
hakuna kitu chochote kinacholeta faida kikawa na ubaya hivyo kulipa kodi kwa
njia ya risiti za kielektronik ni jambo jema kwa vile linaleta faida.
“Kwa vile wananchi wanategemea Serikali yao katika kuwaletea
maendeleo, ili waweze kuwa na maisha bora yenye manufaa, haina budi kuendeleza
yale ambayo yataweza kufanikisha hilo”, Ali anasema.
Farida Abdi wa Mtambile alivyofahamu baada ya kupata elimu
kupitia kwa baadhi ya viongozi wa Serikali, kodi ina asilimia kubwa ya
kuiwezesha nchi kuleta huduma za kimaendeleo.
“Katika nchi hali zinatofautiana wapo wanaomudu huduma katika
familia zao kama vile za afya, elimu na nyengine nyingi lakini pia wapo ambao
wanategemea kupata huduma hizo kupitia Serikalini”, anaongeza.
WAFANYA BIASHARA WANASEMAJE
Gharib Mohamed Ali ambae ni Meneja wa sheli ya Mkoani Pemba
anasema, kutumia mashine za kielektroniki kwa wafanyabiashara kunaleta usawa
kila mmoja analipa kodi bila ya kufanya ubabaifu.
Anasema, katika kazi zake hulazimika kutumia muda wa kuwapa
elimu ya kupokea risiti hizo kwa wateja wanaofika hapo kutaka huduma, kwani
wengi huwa na haraka ya kutaka kuondoka kabla ya kupewa risiti hizo.
“Ni vyema kila mmoja kuchukuwa jitihada yakuelimisha kuhusianana
umuhimu wa kutowa risiti za kielektroniki kwani zinaleta faida kwa wananchi na
nchi yao”, anasema.
Habiba Mohamed Kombo ni mfanyabiashara ya nguo Chakechake
anasema kutumia risiti za kielektroniki ni sahihi, kwani zinafikisha mapato
kule kunakostahiki.
Anasema kila mfanyabiashara ana wajibu wa kufuata utaratibu huo
uliowekwa na serikali ili kufikia malengo yaliyokusudiwa ya kuhakikisha
maendeleo yanakuwa mazuri zaidi.
Said Ali mfanyakazi wa Cable tv Mkoani anasema, ni jambo jema la
kutumia risiti za kielektroniki, ingawa yeye humlazimu kutumia kalamu kujaza
baadhi ya sehemu kutokana na mashine hizo zilivotengenezwa.
“Risiti zenyewe haziendani na matumizi sawa kwa wafanyabiashara
wate, hivyo kwa vile kazi zetu hutofautiana na risiti hizo, mimi huandika kwa
kalamu mwezi anaolipa mteja wangu”, anasema.
Nuru Abdalla mmiliki wa duka la nguo chakechake anasema sheria
iliyowekwa na serikali ikiwemo za ulipaji wa kodi kwa njia za kielektroniki
itawasaidia wafanyabiashara wenyewe kwani kumbukumbu zake zinabakia tofauti na
risiti za karatasi.
VIONGOZI WA SERIKALI WANASEMAJE
Raisi wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.
Hussein Ali Mwinyi ni namba moja kati ya viongozi wanaoelezea umuhimu wa kulipa
kodi kwa njia ya elektroniki .
Anasema, bila ya kodi nchi haiwezi kupiga hatua za maendeleo kama
vile elimu, afya, maji safi na salama, ujenzi wa miundo mbinu na mambo mengine
mengi yanayofanywa na Serikali yanategemea fedha zitokanazo na kodi.
Makamu wa Pili wa rais wa Zanzibar Hemed Suleiman Abdalla katika
matembezi ya kuhamasisha zoezi la kudai risiti za kielektroniki anasema,
umuhimu wa kukusanya kodi kwa kutumia mashine za kielektroniki ni kukuza mapato
ya nchi.
Anasema, ni vyema wananchi kudai na kutoa risiti kwa wanaofanya
miamala ya kibiashara, ili kudhibiti ukusanyaji wa mapato yasiweze kupotea.
“Jukumu la msingi kwa serikali ni kuweka mipango madhubuti ya
ukusanyaji wa mapato ambayo yatatumika katika ujenzi wa miradi mbali mbali ya
maendeleo ili kuijenga Zanzibar mpya”, anasema.
Waziri wa nchi Ofisi ya Rais fedha na Mipango wakati akitoa
tamko la kuwataka wafanyabiashara wote waliopo Zanzibar kuhakikisha wanatumia
mashine za kielektroniki (VFMS).
Anasema, mfumo huo maalum ambao unatengenezwa na bodi ya mapato
Zanzibar (ZRB) unalenga kuziba mianya ya upotevu wa mapato nchini na kuongeza ari
ya ukusanyaji wa mapato.
‘Virtual fiscal management system’ (VFMS) ni mfumo ambao
tayari umeshazinduliwa kwa matumizi rasmi ya kuuzia bidhaa, kutoa huduma na unatengenezwa
kuongeza mapato ya Serikali na kuondoa mianya ya upotevu wa mapato.
“Mfumo huu unawezesha kuhifadhi na kutoa taarifa za mauzo,
kukokotoa mauzo na kodi, urahisi wa ujazaji ritani za kodi pamoja na kufatilia
taarifa za wageni wanaoingia”, anasema.
Spika wa Baraza la Wawakilishi la Zanzibar Zubeir Ali Maulid anasema
kuwa, ni vyema kwa wauzaji na
wafanyabiashara kuweka matangazo katika maeneo yao ya biashara ambayo
yataonesha umuhimu wa kudai risiti kwa anaenunua bidhaa katika maeneo yao ya
kazi.
ZRB WANASEMAJE
Kamishna wa Bodi ya Mapato Zanzibar (ZRB) Yussuf Juma Mwenda
anasema, risiti ama Ankara ndicho kidhibiti cha taasisi za kodi kuthibitisha
kwamba mfanyabiashara ameuza bidhaa au huduma na ametoza kodi na kuifanya Serikali
ikusanye mapato yake inavyostahiki.
Anasema, Serikali imeanzisha mfumo huo ili kuhakikisha kodi yake
inafika Serikalini kwani wadau wakubwa wa kodi ni wananchi wanaonunua bidhaa
kwa wafanyabiashara.
Meneja wa
Idara ya Sera, Utafiti na Mipango wa Bodi ya mapato Zanzibar (ZRB), Ahmed
Haji Sadat anasema ni vyema wafanya biashara kuwa na utamaduni kutoa risiti za
bidhaa zao, ili waweze kufahamu faida na hasara ya biashara wanazozifanya.
“Wafanyabiashara
tambueni suala la risiti ni kitu muhimu kwenu
kwani kutawawezesha kufahamu maendeleo ya biashara zenu”, alisema
Saadat.
Mkuu wa kitengo cha walipa kodi,
Bodi ya Mapato ZRB, Shaaban Yahya Ramadhan anasema ulipaji wa kodi ni jambo rahisi, iwapo
wafanyabiashara watakuwa na utamaduni wa kuweka kumbu kumbu za kudumu pale
wanapofanya mauzo ama manunuzi katika biashara zao.
Anawataka wafanyabiashara
wasiogope kutumia mashine za kutolea risiti kwa kisingizio chochote kile kwani
ziko salama hasa kwa vile zinawawekea kumbukumbu ya kudumu.
Mkurugenzi wa ZRB Pemba Jamal
Hassan Jamal anasema kuwa iwapo mashine za kielektroniki zitatumika ipasavyo
zitaongeza mapato zaidi na hata kuvuuka malengo ya makusanyo ya shilingi bilioni
33.226 ambazo wamewekewa kwa Pemba.
‘’Kwa mwaka wa fedha wa 2022/2023
kwa Pemba tumepangiwa kukusanya kiasi hicho, na naamini tutavuuka lengo, maana
sasa kunaukusanyaji wa mapato kwa njia ya kielektroniki,’’anaeleza
Anasema kazi kubwa ya ‘ZRB’ ni
kusimamia na kuhakikisha ulipaji wa kodi kwa kutumia mashine hizo, kwani kodi
inayolipwa itakwenda moja kwa moja kwenye mfuko wa serikali, tofauti na hapo
awali ambapo risiti zilitolewa kwa mkono”,anafahamisha.
VIONGOZI WA DINI
Sheikh Said wa ofisi ya mufti Pemba anasema asili ya kodi
inatoka katika uislam kama vile kwenye
zaka, ngawira , kodi ya ardhi ,kichwa ambapo zilikuwepo katika dola ya
kiislamu na zilikuwa zinahifadhiwa katika hazina ya serikali iliyokuwa
ikijulikana kwa jina la Bait-ul-mal.
Anasema katika uislamu
kiongozi wa nchi anayohaki ya kuwataka wananchi wachangie kodi kwa dharura
maalum anaweza kuweka kiwango ama asiweke.
“Mfano wa hilo Mtume Muhammad (S.A.W) katika vita vya taabuk
dola ya kiislamu haikuwa na uwezo katika kufadhili vita hivo lakini bwana Mtume
aliwataka waislamu wachangie katika vita hivyo”,anafafanua.
Samwel Elias Maganga wa kanisa la TAG Makangale anasema kwa dini
ya kikiristo kodi sio dhambi kwani inatambua uwepo wa mamlaka nyengine ikiwemo
ya Serikali.
Anasema, dini hiyo inatambuwa kuwa Serikali ni sawa na baba
hivyo ni wajibu wake kupanga mipango yake ikiwemo ya kiuchumi na kuifanya
iendelee mbele.
“Bibilia inasema tutii mamlaka zilizopo na kodi ambayo haikubaliki
ni kama ile ya utapeli, dhuluma lakini kama ni andiko la Serikali lenye haki na
usawa inakubalika”, anasema.
Serikali ya Mapinduzi Zanzibar inahimiza wafanyabiashara na
wananchi kutoana kudai risiti za elektoniki, ili iweze kufanya shughuli zake za
kuwaletea wananchi maendeleo endelevu.
Mwisho
Comments
Post a Comment