NA HAJI NASSOR,
PEMBA::::
AFISA Mipango
wilaya ya Chake chake, Kassim Ali Omar amesema, bado juhudi zaidi zinahitajika
kufanywa, na kamati ya kupambana na ukatili na udhalilishaji wilayani humo, ili
kundi la wanawake na watoto, libaki salama na matendo hayo, kama yalivyo makundi
mengine.
Hayo aliyasema leo Septemba 14, 2022 ukumbi wa TASAF mjini Chake
chake, wakati akifungua kikao cha kamati hiyo, kwenye uwasilishaji wa ripoti
kwa taasisi zinazounda kamati hiyo, ikiwemo ya kituo cha Mkono kwa mkono,
viongozi wa dini, shirika la SOS na wizara ya elimu na Mafunzo ya amali.
Alieleza kuwa, wananchi wa wilaya ya Chake chake wakiwemo
wanawake na watoto, wanaingalia kamati hiyo, ili kutafuta mwarubaini wa matendo
ya udhalilishaji yanayojitokeza siku hadi siku, hivyo lazima mkazo uwekwe.
‘’’Bado jukumu la kipekee litakuwa kwa kamati ya kupambana na
ukatili na udhalilishaji wa wanawake na watoto ya wilaya, hivyo lazima nguvu na juhudi ziongezwe
na wajumbe wa kamati hiyo,’’alifafanua.
Katika hatua nyingine, Afisa huyo Mipango wa wilaya ya Chake
chake Kassim Ali Omar, alisema licha ya juhudi zinazochukuliwa na tasisi kadhaa, lakini bado
kundi la wanawake na watoto, linaendelea kukumbwa na majanga ya udhalilishaji,
hata kwa watu wao wa familia.
Hata hivyo, ameipongeza kamati hiyo, kwa kufanyakazi ya kuifikia
jamii kielimu, licha ya kukabiliwa na changamoto kadhaa, ikiwa ni pamoja na
ukosefu usafiri wa uhakika na makundi ya vijana, kutohudhuria kwenye mikutano ya
wazi vijijini.
Kwa upande wake Katibu wa kamati hiyo, Rashid Said Nassor,
amesema juhudi za makusudi zinahitaka kwa jamii na vyombo vya sheria, ili kuona
wanawake na watoto wanaishi katika mazingira salama.
Alifahamisha kuwa, kama wananchi, vyombo vya sheria na
wahanga wa matukio hayo, hawakufanyakazi kwa pamoja, itakuwa vigumu kutokomeza
matendo hayo.
‘’Jeshi la Polisi, ofisi ya Mkurugenzi wa mashtaka, wahanga wa matukio na
jamii kwa ujumla huu sio wakati tena wa kulaumiana, bali washirikiane, ili
wadhalilishaji wapate hatia mahakamani,’’alishauri.
Afisa Elimu na Mafunzo ya Amali wilaya ya Chake chake, Bur-han Khamis
Juma, amesema wizara inaandaa mpango maalum, ili kukabiliana na waalimu, wanaowadhalilisha wanafunzi skulini.
‘’Ingawa juhudi za kuwakumbusha maadili yao ya kazi zinaendelea, lakini
huwa tunafanya mbinu ya kuwahamisha kutoka skuli moja kwenda nyingine chini ya
uangalizi maalum kwa wale waalimu wanaolalamikiwa,’’alieleza.
Kwa upande wao viongozi wa dini ya kiislamu Ali Mohamed Ali na
mwenzake kutoka dini ya kikiristo Robart Migua Ndalami, walisema sasa
wanachokifanya ni kuwajenga kimaadili wananchi na kundi la vijana, ili kuogopa
kufanya matendo hayo.
Afisa miradi kutoka shirika la SOS Pemba Abdalla Omar Kidim,
alisema wamekuwa wakiziwezesha familia na hata vijana mmoja mmoja kielimu,
katika mpango wao pia unaouhisisha kinga ya majanga.
Kikao hicho ni sehemu ya utekelezaji wa mpangao wa kitaifa wa
kupambana na ukatili wa wanawake na watoto wa Zanzibar wa mwaka 2017 hadi mwaka
2022, ambao ulitaka uwepo wa kamati hizo ngazi ya wilaya.
Mwisho
Comments
Post a Comment