TAARIFA YA MABADILIKO YA NAULI NA BEI ELEKEZI ZA
VYOMBO VYA USAFIRI WA UMMA BARABARANI ZANZIBAR
Ndugu
Wananchi
Asalam Alaykum Warahmatullah Wabarakatu
Nianze kwa
kumshukuru Mwenyezi Mungu Mtukufu kwa, kutujaalia
uhai na afya njema na kutuwezesha kuiona siku ya leo,
Aidha napenda
kuchukuwa fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa
Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi kwa kuendelea kuiongoza nchi yetu
ikiwa katika hali ya amani na utulivu unaowezesha wananchi kuendelea kufanya
shughuli zao bila matatizo zikiwemo shughuli za Usafiri na Usafirishaji.
Ndugu Wananchi, Baada ya kutoa shukurani hizo,
Naomba sasa
nitoe taarifa fupi juu ya mabadiliko ya nauli na bei elekezi za vyombo vya
usafiri wa umma barabarani Zanzibar
ikiwemo Magari ya shamba, Daladala na Taxi.
Ndugu Wananchi, Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar imekuwa ikichukua jitihada mbali mbali katika kudhibiti upandaji
wa bei za mafuta na bei za nauli za vyombo vya kusafirisha abiria kwa lengo la
kuhakikisha kwamba wananchi wanaishi katika maisha nafuu, ikiwemo kufidia gharama
za bei za mafuta. Hata hivyo, bei ya mafuta imekuwa ikipanda katika soko la dunia pamoja
na gharama za uendeshaji vyombo vya moto jambo ambalo linapelekea
wafanyabiashara wa vyombo vya usafiri wa umma kujiendesha kwa hasara.
Ndugu Wananchi, Utaratibu huu wa
kuweka nauli kwa vyombo vya usafiri wa
umma mijini na vijijini unatoa ruhusa kwa jumuiya za usafirishaji abiria
kuwasilisha mapendekezo mapya ya nauli kwa Serikali na baada ya kuyapitia na
kuyafabyia uchambuzi kwa maslahi ya watumiaji na watoa huduma Serikali
huyatangaza.
Ndugu Wananchi, Nauli na bei za
vyombo vya abiria zinazotumika hivi sasa
zimeanza kutumika tokea mwaka 2019
ambapo tokea wakati huo gharama za uendeshaji zimekuwa zikipanda kama vile
mafuta, vilainishaji, leseni ya biashara ya kusafirisha abiria, ruhusa za njia,
bima na tozo nyinginezo.
Ndugu Wananchi, Serikali ilipokea
maombi ya Jumuiya za kusafirisha abiria
kutoka Unguja na Pemba ambayo yalilenga kuongeza nauli na bei za gari za
biashara kwa asilimia 50 (50%) kwa
daladala na asilimia 17(17%) hadi 26 (26%) kwa gari zinazokwenda vijijini
pamoja na bei elekezi kwa gari za Taxi.
MABADILIKO YA NAULI
Ndugu Wananchi, Kwa kuzingatia
mapendekezo ya nauli kutoka Jumuiya za
Usafirishaji Serikali imefanya uchambuzi kwa kutafuta gharama za usafirishaji
abiria kwa vyombo vya usafiri Unguja na Pemba.
Kwa upande wa Unguja, Nauli ya gari za daladala kwa umbali mfupi wa
kilomita 1
hadi 12
imepanda kutoka TZS 400 hadi TZS 500 na kwa umbali mrefu wa kilomita 19 hadi 21
nauli imepanda kutoka TZS 800 hadi TZS 900. Na kwa gari za shamba nauli ya umbali mfupi wa kilomita 1 hadi 14 imepanda kutoka TZS 500 hadi TZS 600
na kwa umbali mrefu wa kilomita 60 hadi
70 nauli imepanda kutoka TZS 2,300 hadi TZS 2,500.
Kwa upande wa Pemba, Nauli ya gari za
abiria zinazotembea umbali mfupi wa
kilomita 1
hadi 7 imepanda kutoka TZS 400 hadi TZS 500 na kwa umbali mrefu wa kilomita 8
hadi 12 nauli imepanda kutoka TZS 500
hadi TZS 600. Na kwa gari za shamba
nauli ya umbali mfupi wa kilomita
1 hadi 9
imepanda kutoka TZS 600 hadi TZS 700 na kwa umbali mrefu wa kilomita 60 hadi 70 nauli
imepanda kutoka TZS 3,000 hadi TZS 3200.
Kwa upande wa usafiri wa Gari za Taxi: Bei elekezi
ya taxi kwa sasa itakuwa ni kuanzia TZS 8,000 kwa kilomita tano.
Ndugu Wananchi, mabadiliko haya ya
nauli na bei elekezi yataanza kutumika
wiki moja baada ya Tangazo hili.
Aidha, niwaombe
Jumuiya za usafirishaji kufika katika Ofisi
za Mamlaka ya Usafiri na Usalama Barabarani Unguja na Pemba kwa ajili ya
kupatiwa Mchanganuo wa nauli kwa Ruti zote za Zanzibar na kuhakikisha mchanganuo
huo unawekwa katika kila chombo cha usafiri wa umma ili kuepusha usumbufu kwa
wananchi wanaotaka kutumia usafiri huo.
Ndugu Wananchi, Nichukue nafasi
hii, kuwashukuru watoa huduma za usafiri wa umma na jumuiya zao kwa kuwa na
uvumilivu katika kipindi chote hiki gharama za uendeshaji zilipopanda, hali hii imekuwa ni ya
mfano na tunachowaomba muendelee kuwa hivyo. Pia nitumie nafasi hii
kuwakumbusha kuzingatia Sheria na kanuni za usafiri barabarani ili kuepusha
ajali zinazoweza kuepukika.
Ndugu Wananchi, Kwa kumalizia,
niwaombe wananchi kutoa taarifa kwa wale wote watakao kwenda kinyume na toleo
la mabadiliko haya ya nauli ili hatua za kisheria kuchukuliwa.
Imetolewa na Dkt. Khalid Salum Mohamed
Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi
Zanzibar
USALAMA
BARABARANI NI JUKUMU LETU SOTE
AHSANTENI
SANA KWA KUNISIKILIZA
14 Septemba,
2022
Comments
Post a Comment