NA HAJI NASSOR, PEMBA:: email: pembatoday@gmail.com::
MRATIBU wa Chama cha waandishi wa habari Tanzania TAMWA-Zanzibar ofisi ya Pemba Fat-hya Mussa Said, amewataka waandishi wa habari kisiwani humo, kuandika habari za uchambuzi wa kitakwimu zinazolenga kuwahamasisha wanawake kudai haki zao za kisiasa, demokrasia na uongozi.
Alisema, vyombo vya habari vinamchango mkubwa wa kuibadilishaji jamii, juu ya mitazamo hasi ya wanawake kuwa viongozi, hivyo uandishi wao wenye uchambuzi wa takwimu utasaidia kwa wanawake hao.
Akizungumza kwenye ufungaji wa mafunzo ya siku tatu yaliyofanyika ofisi ya TAMWA-Pemba, alisema wanawake wana haki kama wanaume kupata fursa za kuongoza kuanzia ngazi ya jamii hadi taifa, na hilo litawezekana ikiwa vyombo vya habari, vitafanya ushawishi na utetezi wenye uchambuzi.
''Kayafanyieni kazi mafunzo haya, kupitia mradi huu wa kuwawezesha wanawake kudai haki zao za uongozi, demokrasi na siasa 'SWIL' , maana wanawake wana haki sawa kwenye fursa kama wanaume,''alieleza.
Kwa upande wake Afisa Mawasiliano kutoka TAMWA-Zanzibar ofisi ya Pemba Gaspery Charles, alisema bado mitandao ya kijamii haijatumika vilivyo, katika kufanya ushawishi na utetezi.
Alieleza kuwa, moja ya eneo ambalo watoa uamuzi na watunga sera wanaweza kufikiwa ni kupitia mitandao ya kijamii, hivyo ni wajibu kwa waandishi hao, hilo kulifanya kwa vitendo.
Akiwasilisha mada ya ushahiwishi na utetezi kupitia vyombo vya habari, Katibu mkuu wa klabu ya waandishi wa habari Pemba 'PPC' Ali Mbarouk Omar, alisema lazima mtaka fanya ushawishi na utetezi, ajue mbinu shirikishi.
Wakichangia kwenye mafunzo hayo, mwandishi wa habari wa ZBC Asma Abassi, alisema kazi iliyobakia ni kwao, kuandaa vipindi na kuandika habari na makala zenye kuvutia kwa jamii.
Meneja wa redio Jamii Micheweni Pemba Ali Massoud Kombo, alisema mbinu za kuwasilisha mada ya uchechemuzi inahitajika mno, ili kundi kandamizi libadilike.
Mradi wa Kuwawezesha wanawake kudai haki zao za uongozi, siasa na demokrasia 'SWIL' ambao ulizinduliwa mwaka 2020, ukitarajiwa kumalizika mwaka 2023, unatekelezwa na Chama cha waandishi wa habari wanawake Tanzania TAMWA-Zanzibar, Jumuiya ya Utetezi wa Kijinsia na Mazingira Pemba ‘PEGAO’. na Chama cha wanasheria wanawake Zanzibar ZAFELA.
Mwisho wa mradi huo unatarajiwa kuwafikia wanawake wasiopungua 6,000 na iwe wameshawezeshwa kudai haki zao za uogozi, siasa na demokrasia.
mwisho
Comments
Post a Comment