Skip to main content

DAKTARI MWENGINE PEMBA ALIYEDAIWA KUMBAKA MGONJWA WAKE, ACHIWA HURU

 


NA HAJI NASSOR, PEMBA

MAHAKAMA ya mkoa Chake chake, imemuachia huru daktari Hassan Said Mohamed miaka (38) wa kituo cha hospitali  ya Chake chake Pemba, baada ya mtoto wa aliyedai kubakwa mara tatu kumkana daktari huyo mahakamani.

Mahakama hiyo maalum ya makosa ya udhalilishaji, chini ya hakimu Muumini Khamis Juma, ililazimika kumuachia huru daktari huyo, kwa vile muathirika (mtoot) amesema hajawahi kukutana kimapenzi na mtuhumiwa huyo.

Akiwa mahakamani hapo tokea Juni 29, mwaka huu akisubiri hukumu baada ya upande wa mashtaka kufunga ushahidi wao, daktari huyo hakuamini macho yake, baada ya hakimu Muumini alipomtamkia kumuachia huru.

‘’Licha ya ushahidi uliotolewa na mashahidi watatu mahakamani hapa, lakini kutokana na maelezo ya mtoto wa miaka 17, ambae anadaiwa ulimbaka mara tatu, na yeye kushindwa kukutambua, sasa uko huru,’’alisema Hakimu huyo.

Hakimu huyo alisema, ushahidi ambao ungepaswa kuzingatiwa zaidi ni wa mtoto mwenyewe, anayedai kubakwa, ingawa kila anapohojiwa, alikuwa akimkana mtuhumiwa huyo.

Mwendesha mashataka kutoka Afisi ya Mkurugenzi wa mashataka Ali Amour Makame, aliiomba mahakama hiyo, kutoa adhabu kali kwa mshitakiwa, ili kukomesha matendo hayo.

‘’Mheshimiwa Hakimu, leo (juzi) kesi hii ya daktari Hassan Said Mohamed ipo mbele yako kwa ajili ya kutolewa hukumu, na tayari tumeshafunga ushahidi wetu sisi,’’aliiambia mahakama.

Ingawa, hakimu wa mahakama hiyo, alimuachia huru daktari huyo kutokana na shahidi nambari moja (muathirika) kutomuunganisha na kosa la msingi.

Awali ilidaiwa mahakamani hapo kuwa, daktari huyo alimbaka mtoto wa miaka 17 mara tatu kwa siku tofauti, ndani ya hospitali ya serikali iliyopo Chake chake Pemba.

Kosa la kwanza alidaiwa kulitenda Novemba 7, kisha Disemba 9 na Disemba 11 mwaka jana, ambapo kesi hiyo ilifunguliwa kwa mara ya kwanza Disemba 16, mwaka jana na kuachiwa huru Juni 29, mwaka 2022.

Kwa mwaka huu, hii ni kesi ya pili kuondolewa mahakamani zikiwahusisha madaktari, ambapo ya pili ni ile ya Is-haka Rashid Hadid, ambapo iliondolewa mahakamani Julai 13, mwaka huu kwa sababu kama hizo.

Tukio jengine linalofafana hilo, lilitokea Novemba 21, mwaka 2019, katika hospitali ya Chake chake, baada ya daktari wa kitengo cha Atrasaund, kudaiwa kuomba rushwa ya ngono kwa mjamzito, kama sharti la kumpa huduma. Ambapo kesi hiyo ilifutwa Januari mwaka 2021.

Aidha Disemba 18, mwaka mwaka 2019, TBC 1, iliripoti Afisa Muuguzi Msaidizi wa kituo cha Afya Mamba mkoani Katavi kushikiliwa na Jeshi la Polisi, kwa tuhuma za kumbaka mjamzito, wakati alipokuwa akimsaidia kujifungua.

                    Mwisho

 

 

 

 

                     

 

 

 

                      Mwisho  

Comments