NA ZUHURA JUMA, PEMBA
JAJI Mkuu
wa Zanzibar Khamis Ramadhan Abdalla amewataka mahakimu kuendelea na kasi ya
kusikiliza kesi za udhalilishaji kwa haraka, ili ziweze kupata hatia kwa muda
mfupi.
Akiwasilisha ripoti ya ziara ya Jaji huyo iliyofanyika kuanzia
Julai 18 mwaka huuu, Kaimu Mrajis Mahakama Kuu Zanzibar Salum Hassan Bakar alisema,
takwimu zinaonesha kupungua kwa kiasi kikubwa mrundikano wa mashauri hayo
mahakamani.
Alisema kuwa, katika ripoti hiyo Jaji Mkuu aleleza kuwa,
pamoja na kuridhika kwa kasi ya uendeshaji wa mashauri hayo kwa mahakama za
udhalilishji Mkoa wa Kaskazini na Kusini Pemba, lakini bado mahakimu wana
jukumu la kuziendesha kesi hizo kwa haraka zaidi.
‘’Vile vile aliridhishwa na ujaji wa mashahidi mahakamani na
kuwaasa wale wachache ambao wanakaidi, wajitokeze kufika mahakamani ili
kuyamaliza kabisa mashauri hayo’’, alisema Kaimu huyo.
Aidha aliwaagiza mahakimu na makadhi kuyafanyia kazi mashauri
yaliyofikishwa mahakamani kuanzia mwaka 2020 kuja chini, ambapo katika
kutekeleza hilo amewataka kushirikiana na wadau wote wanaohusika ili kufanya
kazi hadi siku za mapumziko.
‘’Mushirikiane na ofisi ya Mkurugenzi wa mashitaka pamoja na
mawakili wa kujitegemea katika kuhakikisha kesi hizo zinamalizika haraka,
ambapo mahakama imeandaa bajeti maalumu kwa ajili ya kufanya kazi hiyo kwa siku
ambazo ni za mapumziko’’, alifafanua.
Kaimu huyo alisema kuwa, Jaji mkuu katika ziara yake hiyo pia
amepiga marufuku utengenezaji wa hati zote za kisheria ikiwemo hati za madai,
majibu ya madai, sababu za rufaa, hati za kiapo na mikataba kwenye mahakama
zote Unguja na Pemba.
‘’Hati hizo zinatakiwa zitengenezwe kwenye ofisi za mawakili,
mavakili, Idara ya msaada wa kisheria au vituo vya msaada wa kisheria, kwani ni
kazi yao na wao wanalipa kodi Serikalini, hivyo kazi hizo zinatakiwa kufanyika
huko’’, alisema.
Kwa upande wake Naibu Mrajis Mahakama Kuu Pemba Faraji Shomari
alisema kuwa, jumla ya kesi 56 za udhalilishaji zimefunguliwa kwa mahakama za Pemba,
ambapo Kaskazini ni kesi 27 na Kusini ni kesi 26.
Alifafanua kuwa, kati ya kesi hizo 27 za Mkoa wa Kaskazini
Pemba kesi tisa zimetolewa maamuzi na kesi 18 zinaendelea huku Mkoa wa Kusini
Pemba kesi tisa zimetolewa maamuzi na 17 zimnaendelea.
Aliwataka mahakimu kwamba wasijibweteke katika kuzitolea
maamuzi kesi hizo, ili kuona kwamba zinamalizika kwa muda mfupi jambo ambalo
litasaidia kupunguzika kwa matendo hayo katika jamii.
Ziara hiyo ya siku tatu ilikuwa na lengo la kuwashukuru
wafanyakazi kwa ushirikiano wao pamoja na kusikiliza na kujadiliana na
wafanyakazi kuhusu changamoto mbali mbali zinazokwamisha utendaji kazi za kila
siku na kuweka mikakati ya kuzipatia ufumbuzi.
MWISHO.
Comments
Post a Comment