NA HABIBA ZARALI, PEMBA
WAANDISHI wa habari wametakiwa kuongeza nguvu katika kuandika habari zinazowajengea uwezo wanawake kutambua sera mbalimbali zinazozungumzia haki zao, ili iwe rahisi kujua namna ya kushiriki na kudai haki zao za uongozi.
Kauli hiyo imetolewa na Mkurugenzi wa Chama Cha waandishi wa habari TAMWA Zanzibar Dk. Mzuri Issa Ali wakati akifunguwa mafunzo ya kuwajengea uwezo waandishi wa kuandika habari za uchambuzi kuhusu ushiriki wa wanawake katika masuala ya uongozi.
Alisema ni wajibu wa waandishi kuendelea kuelimisha jamii kuondokana na mitazamo hasi inayorudisha nyuma jitihada za wanawake kuweza kushika nafasi za uongozi.
Alifahamisha kuwa ni vyema kwa waandishi hao kuelimisha jamii kuhusu itikadi mbovu zinazowavunja moyo wanawake na watoto wa kike na badala yake ziweze kuwajengea uwezo kuhusu kuwania nafasi za uongozi.
"Tunataka nafasi za uongozi kwa sasa ziangalie uwiano wa kijinsia kwa wanaume na wanawake wakati tukijiandaa kwa safari ya 2025", alisema.
Alisema ni vizuri kuwahamasisha wanawake na wanaume kubadilika na kutenga muda maalum kushirikiana na wake zao katika utekelezaji wa majukumu ya kifamilia ili iwe kikwazo kwa mwanamke kufikia katika nafasi ya uongozi.
Kwa upande wake Mratibu wa chama cha waandishi wa habari Pemba Fat-hiya Mussa Saidi alisema ni vyema waandishi wa habari kuandika na kutangaza vikwazo ambavyo vinawakwamisha wanawake na kuonesha njia ya kuzipatia ufumbuzi kwa maslahi mapana ya Taifa.
Alisema licha ya juhudi mbalimbali zinazochukuliwa na Serikali na taasisi binafsi lakini bado baadhi ya mifumo inakwamisha wanawake kuweza kufikia usawa katika vyombo vya kutowa maamuzi.
"Katika mafunzo ya Leo hakikisheni mnayatumia vizuri kwa kuleta usawa na kufikia malengo ya kuwepo uwiyano katika ngazi ya kutowa maamuzi",alielekeza.
Akitowa mada ya jinsia na uongozi mwandishi Haji Nassor Mohamed alisema bado mifumo dume inaendelea kuwakosesha wanawake haki zao za msingi ikiwemo za uongozi.
Alifahamisha kuwa ni vyombo vya habari pekee ndivo visivotumia nguvu kubadilisha mfumo huo na mitazamo finyu mbalimbali ya kubadilisha kundi moja ama jengine hivyo ni wajibu wao kuhakikisha wanatumia vyombo vyao kutowa elimu hiyo.
Wakitowa mchango wao katika mafunzo hayo mwandishi wa ZBC Mchanga haroub na Asma Abas walisema mbali na waandishi kuandika habari za Wanawake na uongozi lkn bado Kuna changamoto zinazowakabili Wanawake hao ikiwemo umaskini na tabia ya kukata tamaa.
Walisema wanawake ni chachu ya kuleta maendeleo kwani anaweza kushika nafasi za uongozi katika sekta zote na kufikisha sauti kwa walio chini yao.
Mafunzo hayo ya siku tatu ni kupipitia mradi wa kuwawezesha wanawake kushiriki katika masuala ya uongozi na demokrasia unaotekelezwa kwa mashirikiano na taasisi za chama Cha waandishi wa habari wanawake Tanzania,TAMWA-Zanzibar, jumuiya ya wanasheria wanawake Zanzibar ZAFELA, na jumuiya ya utetezi wa jinsia na mazingira Pemba (PEGAO) kwa ufadhili wa ubalozi wa Norway.
Mwisho.
Comments
Post a Comment