NA HAJI NASSOR, PEMBA
WAZAZI na walezi kisiwani Pemba,
wametakiwa kuwasiliana kwa ishara, maneno na kuwafanyia uchangamshi wa michezo kadhaa
watoto wao wachanga, kwani kufanya hivyo ni njia rahisi ya kugundua, ikiwa wamezaliwa
na ulemavu ama laa.
Aidha wazazi
hao wameelezwa kuwa, kufanya njia hizo zitakuza kwa haraka ufahamu wa wazazi kwa
watoto wao, ikiwa wamezaliwa na ulemavu ama laa.
Wakizungumza
na mwandishi wa habari hizi, wataalamu wa malezi na makuzi ya awali ya
kisayansi ya mtoto ‘SECD’ kisiwani Pemba, walisema wapo watoto wamekuwa
wakizaliwa na ulemavu, ingawa kisha huishi nao kwa wazazi kukosa kuwafuatilia.
Mmoja kati
ya wataalamu hao, Rashid Said Nassor alisema, ni rahisi kwa wazazi na walezi,
kutambua ulemavu wa awali wa watoto wao, ikiwa wataanza utamaduni wa
kuwasiliana nao mapema.
Alisema, mtoto
baada ya kuzaliwa ubongo wake uko tayari kupokea jambo lolote, hivyo ni wakati
mwafaka kwa wazazi na walezi, kuanza nao mawasiliano na uchangamshi ili kujua,
ikiwa wana aina yoyote ya ulemavu waliozaliwa nao.
Mtaalamu huyo
alisema, sayansi inakubali kuwa, mtoto baada ya kuzaliwa anauwelewa mkubwa
ikiwemo kusikia suati na milio mbali mbali, hivyo ni wakati mwafaka kwa wazazi
kufanya uchangamshi.
‘’Njia moja
ya kumgundua mtoto ikiwa amezaliwa na ulemavu ama laa, ni wazazi na walezi
kuchangamana na watoto kuanzia siku moja baada ya kuzaliwa hadi miaka minane
kwa kufanya michezo mbali mbali,’’alieleza.
Aidha
mtaalamu huyo wa ‘ECD’ alifahamisha kuwa, kazi ya kuchangamana na mtoto sio
jukumu la mama pekee, bali hata akinababa wanatakiwa kufanya hivyo.
Nae mtaalamu
wa ‘ECD’ Omar Mohamed Ali, alisema upo uwezekano mkubwa wa mtoto aliyezaliwa na
ulemavu na kama ukiwahiwa mapema kutibika.
‘’Hili
haliwezi kugundulika, ikiwa wazazi na walezi wataacha kuwasiliana, kuchangamana
na kufanya uchangamshi na watoto wao kwenye makuzi ya awali,’’alifafanua.
Hivyo
amewaasa wazazi na walezi, kujenga utamaduni wa kuwa karibu kimawasiliano na
watoto, na kufuatilia usikivu wao ili kugundua umahiri na udhaifu wao mapema.
‘’Inawezekana
watoto wanahitaji kupata matibabu ya mapema, iwe koo, maskio, macho, viungo au
ngozi kwa lengo la kuzuia ulemavu wa kudumu, na hili litawezekana kwa ukaribu
wa wazazi kwa watoto wao wachanga,’’alifafanua.
Alieleza
kuwa, ubongo wa mtoto mchanga unawezo wa ufahamu wa asilimia 25 na kupokea kila
kitu, ambapo ni wakati mwafaka kwa wazazi na walezi, kuchangamana nao.
‘’Wazazi
wasisite kuchangamana na watoto wao, maana sayansi inakubali kuwa, ukitaka
kumgundua mtoto juu ya aina ya ulemavu alionao, hiyo ni njia moja
wapo,’’alieleza.
Baadi ya
wazazi na walezi wamesema, wamekuwa karibu na watoto kufanya uchangamshi,
ingawa sio kwa kugundua aina ya ulemavu walio nao.
Mzazi Mwanaisha
Himid Hussein wa Wawi Chake chake, alisema hawana uwelewa wa elimu ya malezi ya
kisayansi na makuzi ya awali ya watoto ‘ECD’ bali, wamekuwa wakifanya kama
mazoea tu.
‘’Tunawasiliana
na watoto wetu na kufanyanao uchangamshi, ingawa hatutengi muda maalum kama
wataalam wanavyopendekez,’’alieleza.
Nao wazazi
Habiba Soud Khalfan na mwenzake Aisha Hussein Khamis walisema, wakati mwengine
wamekuwa wakipuuzia uchangamshi na kufanya mawasiliano na watoto wao, wakidhani
hawana uwezo wa uwelewa.
‘’Kwanza
hatuamini kuwa, mtoto aliyezaliwa ndani ya siku moja, anauwezo wa kusikia zaidi
ya lugha 600, kama watalaamu wanavyotueleza, na ndio maana hatukuona umuhimu
huo,’’alieleza.
Kwa upande
wake Meneja ‘ECD’ tasisi ya Maendeleo ya Binadamu kutoka Chuo Kikuu cha Aga
Khan, Mombasa Kenya Joyce Marangu alisisitiza kuwa, wataendelea kuisaidia
Tanzania katika malezi ya kisayansi.
‘’Moja ya
faida kubwa ya malezi ya ‘CED’ kwa wazazi na walezi ni kugundua ufahamu na
umahiri wa mtoto tokea mapema, lakini hata juu ya uwezo wake wa kutambua mambo
kadhaa,’’alifafanua.
Kaimu Afisa
Mdhamini wizara ya Afya Pemba Dk. Yussuf Hamad, alisema elimu hiyo ya ‘ECD’
hutolewa kwenye kliniki za mama wajawazito.
Hata hivyo
alikiri kuwa, elimu hiyo inalazimika kutolewa kwa ngazi ya jamii nzima, ili
malezi hayo yawe maarufu, katika malezi, makuzi ya watoto wote.
Mkurugenzi Mkaazi
wa tasisi ya Children in Cross fire Cragi Ferla aliwataka waandishi wa habari
kuisambaaza elimu ya ‘ECD’ kwa jamii, ili taifa liwe na watoto wanaojifahamu.
Mwisho
Comments
Post a Comment