NA SALUM VUAI, ZANZIBAR@@@@
KUFUATIA uteuzi wa
Mawaziri wapya Zanzibar baada ya uchaguzi mkuu wa Oktoba 29 mwaka huu
uliokirudisha madarakani Chama cha Mapinduzi, waandishi wa habari hawakusita
kutoa ya moyoni wakieleza matumaini waliyonayo katika kuimarika zaidi kwa sekta
ya habari.
Wadau wa habari na
waandishi waliozungumza na gazeti hili, wamesema kwa miaka mingi, sekta ya
habari visiwani Zanzibar imekuwa ikipata mafanikio kadhaa, ingawa pia
wamebainisha changamoto mbalimbali
zinazowabana katika utekelezaji wa majukumu yao.
Wamesifu kuongezeka kwa uhuru
wa habari kwa kiasi fulani, lakini wakaeleza kuwa bado baadhi ya watu wanatawaliwa
na dhana potofu kwamba waandishi wa habari hawapaswi kuwa marafiki wa kudumu
bali ni wa msimu tu hasa pale maslahi yao binafsi yanapohusika.
Kutokana na fikra kama
hizo, mara kwa mara waandishi wamekuwa wakinyimwa taarifa au kuamriwa kutozitangaza hasa ikiwa
jambo linalotakiwa linahusu uzembe, hujuma au makosa ya mtu au taasisi
inayohojiwa.
Hata Rais wa Zanzibar na
Mwenyekiti wa Barza la Mapinduzi, aliitaja na kuikemea tabia hiyo alipowaapisha
mawaziri wapya aliowateua baada ya uchaguzi mkuu, akihoji kwa nini hata taarifa
za maendeleo zifichwe.
MUARUBAINI
Ili kuondoa vikwazo hivyo
na vyengine vinavyofanana navyo, marekebisho ya sheria ya habari kimekuwa kilio
kikubwa kwa waandishi, wakitaka sheria mpya inayokwenda na wakati uliopo na
isiyokuwa na masharti yanayoumiza.
Ifahamike kuwa, uhuru wa
habari na kutoa maoni, ni miongoni mwa haki za binadamu zilizomo katika
mikataba mbalimbali ya kitaifa na kimataifa.
Hiyo inatokana na masuala
ya haki hizo za binadamu kuanza kuingizwa katika mikataba hiyo mnamo mwaka 1950
baada ya dunia kuweka Azimio la kuzilinda kimataifa (Universal Declaration of
Human Rights-UDHR) lililofikiwa mwaka 1948.
Kama hiyo haitoshi,
barani Afrika, suala la haki za binadamu liliainishwa katika mkataba wa Afrika
kuhusiana na jambo hilo lililopitishwa mwaka 1981.
Mwenyekiti wa Jumuia ya
Waandishi wa Habari za Maendeleo Zanzibar (WAHAMAZA) Hawra Shamte, alisema haki
ya uhuru wa kujieleza ambayo pia inahusu haki ya uhuru wa habari
inalindwa chini ya Ibara ya 18 ya Katiba ya Zanzibar.
Ibara hiyo 18 (1)
inasema: “Bila ya kuathiri sheria nyengine za nchi, kila mtu anayo haki ya
uhuru wa maoni (kujieleza), kutafuta, kupokea na kusambaza habari na mawazo
yake kupitia chombo chochote cha habari bila kujali mipaka ya nchi na pia anayo
haki na uhuru wa kutoingiliwa mawasiliano yake.
Ibara hiyo hiyo kifungu
namba 2, kinasema; “Kila raia anayo haki ya kupewa taarifa wakati wote wa
matukio mbalimbali nchini na duniani kwa jumla ambayo ni muhimu kwa maisha na
shughuli za wananchi na pia masuala yenye umuhimu kwa jamii.”
Akinukuu mapungufu
yaliyomo katika kifungu cha kwanza kama yalivyooneshwa kwenye rasimu ya
marekebisho pendekezwa ya sheria ya habari, Hawra alisema kinanyang’anya haki
na hivyo kinahitaji kurekebihswa ili kisiume.
“Hapo ilipoelezwa katika
kifungu hicho cha Katiba, maneno; “Bila kuathiri sheria nyengine yoyote ya
nchi”, kinamaanisha kuwa, kufurahia uhuru wa kujieleza, kutafuta, kusambaza
habari, kunategemea sheria nyengine za nchi,” alisema.
Aliitaja pia Ibara ya 24
ya Katiba ya Zanzibar inayosomeka, “Haki za binadamu na uhuru, kanuni zake
ambazo zimeainishwa katika Katiba hii, hazitatekelezwa na mtu kwa namna ambayo
itasababisha kuingiliwa au kukandamiza haki na uhuru wa watu wengine au maslahi
ya umma.”
Mwenyekiti huyo alisema
aya iliyotajwa hapo juu, inaweka bayana kwamba haki na uhuru huo unaweza
kuwekewa mipaka na sheria iliyotungwa na Baraza la Wawakilishi ikiwa
kizuizi hicho ni cha lazima.
Shamte alionesha wasiwasi
kuwa kifungu hicho kinatoa nafasi kwa Baraza la Wawakilishi kuweka mipaka ya
kufurahia uhuru wowote ikiwa ni pamoja na ule wa kujieleza.
“Kwa uhitaji wa sheria
mpya ya habari hapa Zanzibar, uko ulazima Katiba hiyo pia ifanyiwe marekebisho
ya haraka na ni wajibu wa waandishi
kuchagiza jambo hilo lifanyike sasa bila ya ajizi,” alibainisha.
Ni wazi uharaka huo ni
muhimu kwa kuwa zipo sheria nyengine nyingi zinazoathiri uhuru wa habari na
haki ya kujieleza, kwa mfano sheria za usalama wa Taifa, Baraza la Wawakilishi,
Takwimu na ile ya makosa ya mtandaoni ambayo imetungwa Tanzania Bara na
haijaridhiwa Zanzibar lakini inatumika.
Kauthar Is-Hak, mwandishi
na ofisa habari mwandamizi Idara ya Habari Maelezo Zanzibar, alishauri sheria
ijayo ijumuishe pia maeneo yanayokataza matumizi makubwa ya nguvu kwa
wanahabari iwapo kwa bahati mbaya,
watabainika kutangaza taarifa zinazohisiwa kwenda kinyume na sheria za nchi, au
kwa upande mmoja kutopendezewa tu kutolewa kwake.
Kwa kuwa dunia inakwenda
haraka katika maendeleo ya teknolojia ya habari, amesema ni vyema sheria mpya
izingatie mabadiliko hayo.
“Dunia ya sasa ni tofauti
na kale ambapo teknolojia mpya imeshika kasi na ndio inayowaleta watu pamoja
kwa muda mfupi na haraka zaidi. Mitandao ya kijamii imerahisisha mawasiliano na
hakuna kitu kinachoweza kufichwa,” alifafanua.
Ofisa huyo alisema ingawa
uhuru una mipaka, lakini huu si wakati wa kufungana midomo, akisema dunia
ilipofika, ni vigumu kuwadhibiti watu wasitoe joto lao.
Hata hivyo, alieleza kuwa
jambo la muhimu sheria isiwabane watu
kwa kuwa tu wanagusa mambo yasiyofaa ambayo watendaji hawataki yadhihirishwe hata kama ni kwa maslahi mapana
ya umma.
ADHABU KWA VYOMBO VYA HABARI
Mjumbe wa Kamati ya
Wataalamu wa Habari Zanzibar (ZAMECO) Jabir Idrissa Yunus, aligusia suala la
adhabu kwa waandishi wa habari na vyombo vinavyokutwa na makosa ya kimaadili.
Alisema jambo hilo
linahitaji kutazamwa kwa jicho la tatu ili kuhakikisha adhabu zinazotolewa
hazimuathiri mtu asiyehusika, mathalan kukifungia chombo cha habari kwa kosa
binafsi la mwandishi.
Alieleza kuwa, kufungia chombo cha habari kwa kosa linalomhusu mwandishi si haki. Kwanza adhabu yenyewe ni kubwa sana na kufanya hivyo ni kuadhibu wanaokitegemea kihabari.
Kadhalika, alisema ni busara kushughulika na mwandishi kwa kutumia njia za kuelimisha zaidi maana wakati mwengine makosa hutokana na sifa ya kibinadamu, kuikosea au bahati mbaya.
“Kwa mfano, madaktari na wauguzi nao hukosea. Je, ifungiwe hospitali yote? Na upande wetu tunayo Mabaraza ya Usuluhishi, basi na yatumike kusahihishana," alishauri.
"Juzi tu hapa tumesikia mgogoro kati ya
Rais Trump wa Marekani na BBC. Wakosaji ni Idara ya Habari ya
BBC, halijafungiwa shirika, mtendaji mmoja ndio amejiuzulu, Shirika linaendelea na kazi. Ndivyo nasi tunapaswa kwenda."
Alihitimisaha kuwa kusema
kuwa, mchezo wa kufungia-fungia ukiendekezwa, itakuja siku watu wataamka
asubuhi hakuna hata gazeti moja mtaani, na rediio/televisheni zote zimefungwa.
Alitaka nchi isifike huko
na sheria ijayo isiweke ugumu kama huo.
WATU WENYE ULEMAVU
Jumuiya ya vyama vya watu
wenye ulemavu ni miongoni mwa wadau wakubwa wa habari, hivyo mwandishi wa
makala haya alizungumza na Mratibu wa Chama cha Watu Wasioona Zanzibar (ZANAB)
Adil Mohammed Ali kujua maoni yao kwa ujumla.
Alikumbusha kuwa,
Zanzibar ilikuwa na sheria namba 5 ya usajili wa wakala wa habari, magazeti na
vitabu ya mwaja 1988 ambayo ilionekana na mapungufu yaliyoikuwa yakikwamisha
haki ya uhuru wa vyombo vya habari na uandishi.
Alisema hata baada ya
kurekebishwa, bado imeonekana sheria iliyopo sasa haitekelezeki vizuri.
Adil alikiri kuwa huu ni
wakati muafaka Zanzibar ipate sheria mpya ya habari ili kukidhi matakwa ya
uhuru wa kujieleza na kuwa na serikali inayoendeshwa kwa misingi ya uwazi na
ukweli.
Alisema, waandishi wa
habari ni wadau wa maendeleo, na pia ni jicho linaloona mbali na ni sauti ya
wasiokuwa na sauti wanaoweza kuleta mabadiliko chanya kimaendeleo.
WIZARA YA HABARI
Akizungumza katika
mahojiano na televisheni ya Shirika la Utangazaji Zanzibar (ZBC), Waziri wa
Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo Riziki Pembe Juma, aliahidi kulianyia kazi
suala la upatikanaji sheria mpya ya habari.
Alisema anaelewa kuwa
ombi hilo ni la miaka mingi na kwamba hatua zimekuwa zikichukuliwa kuipitia na
kuichambua rasimu katika ngazi tofauti, akisema kazi iliyobaki ni kuipeleka
Baraza la Wawakilishi ikajadiliwe kuhitimisha mchakato.
Bila shaka, kauli hii ya
Mhe. Waziri inawapa wanahabari matumaini makubwa kwamba, marathoni ya kusaka
sheria mpya, itafikia mfundani kipindi kifupi kijacho.
BARAZA LA HABARI
Suala la uchechemuzi kwa waandishi wa habari kote
Tanzania ili kuwajengea uwezo wa kuyatetea kitaalamu mambo yanayowahusu, ni
sehemu ya mipango ya Baraza la Habari Tanzania (MCT).
Makongamano na mafunzo mbalimbali yamekuwa
yakiandaliwa na MCT ili kuinua uelewa
wa waandishi na wahariri, si tu
kuandika kwa weledi, bali kuweza kuchambua kitaalamu masuala yanayogusa ustawi
wa taifa na dunia kwa jumla.
Kwa mfano kuanzia Septemba 8, 2025, MCT iliendesha mafunzo
ya siku tano ya wahariri na waandishi wa magazeti, radio televisheni na mtandaoni, yaliyofanyika katika Michenzani Mall mjini Unguja.
Mafunzo hayo yalilenga kuimarisha uwezo
wa kitaaluma na kisheria,
namna
ya kung’amua taarifa zisizo sahihi (misinformation), taarifa za uongo
(disinformation) , hotuba na matamshi
ya chuki
(hate speeches) kuelekea uchaguzi mkuu uliopita.
Aidha, Novemba 17-19, MCT iliandaa mafunzo kama hayo kwa
waandishi na wahariri wanachama wa Kamati ya Wataalamu wa Habari Zanzibar
(ZAMECO) Mnarani Mapinduzi Square, kuelimisha mbinu za utetezi (Advocacy)
katika masuala na maslahi ya wanahabari.
Comments
Post a Comment