NA MOZA SHAABAN, PEMBA@@@@
SHERIA
ya watu wenye ulemavu ya Zanzibar nambari
8 ya 2022 kifungu cha 45 kinakemea udhalilishaji kwa watu wenye ulemavu.
Kwa kueleza mtu yeyote atakae mdhalilisha au
kumkandamiza mtu mwenye ulemavu, kwa kumuita jina lisilofaa kutokana na aina ya
ulemavu wake, atakua ametenda kosa.
“Atakae tiwahatiahi kwa kufanya kosa hilo, atalipa
faini isiyopungua shillingi 100,000 na isiozidi shillingi million 1, au kifungo
kwa kipindi kisichopungua mienzi miwili au vyote wiwili”, kimefafanua.
Mkataba wa kimataifa wa watu wenye ulemavu wa mwaka 2006
ibara yake ya 17, inazungumzia kuhusu kuheshimu tofauti za kimaumbile.
“Kila mtu mwenye ulemavu anayo haki ya kuheshimiwa kwa
ukamilifu wake kimwili na kiakili kwa misingi ya usawa na watu wengine,”
imeeleza ibara hiyo.
Ieleweke kua katika jamii, lugha ina nguvu kubwa
katika kuunda mitazamo na hisia kuhusu makundi mbali mbali ya watu.
Hata hivyo,
matumizi ya majina na lugha zisizofaa, yanaweza kuathiri vibaya jinsi tunavyo
watendea wingine, hasa wale wenye ulemavu.
Pamoja na kuwepo kwa sera kanuni na sheria zinazotaka
watu wenye ulemavu kuheshimiwa na kuthaminiwa kwa kutofanyiwa udhalilishaji wa
aina yeyote, bado jamii haijaliafiki hili.
Sheria za
kuwalinda watu wenye ulemavu ni muhimu sana katika kuhakikisha haki zao
zinaheshimiwa na wanapata fursa sawa katika jamii, ingawa hazifuatwi ipasavyo.
Kwani wapo wanao wadhalilisha kimwili, hata kiakili
kwa matumizi yao ya lugha iliyojaa kejeli , ikiwemo kuwaita majina kutokana na
aina ya ulemavu wao na kuacha jina halisi.
WATU
WENYE ULEMAVU
Zuhura Haji mwenye ulemavu wa uziwi anasema, jina lake
sasa halitiliwi maanani katika jamiii inayo mzungumka, na badala yake huitwa
jina kutokana na aina yake ya ulemavu.
Amekua akipambana na hili kwa muda mrefu na hadi sasa
ameamua kukaa kimya ingawa si jina linalo mridhisha.
Said Saleh Sultan mwenye ulemavu wa viungo, anasema
katika jamii yake aina ya ulemavu
imekua umaarufu au utambulisho wake,
ingawa haridhishwi na hafurahishwi na hilo.
Aneleza pamoja na kukataa na kuelimisha jamii juu ya
athari ya jambo hili, bado jamii haijakubali kuwapokea watu wenye ulemavu,
kutokana na walivyo.
“Watu hutumia aina yangu ya ulemavu kama ni
utambulisho wangu, na jina langu kamili limesahaulika kabisa, si pendi iwe hivi
ila jamii haijakubali utofauti wa kimaumbile tulionao” anaeleza.
Rehema Juma Makame mwenye ulemavu wa uoni anasema sio
yeye tu, hata watoto wake huitwa jina lililoambatana na aina ya ulemavua alio
nao.
Anasema hili halimuathiri yeye pekee, bali hata watoto
wake kwani wanapokua mitaani na watoto wingine, watu hutumia ulemavu wa mama
yao, kama ni adhabu kwao.
Halima Ahmada Hussein ni mzazi mwenye mtoto mwenye ulemavu anasema, mtoto wake mwenye ulemavu wa viungo, hukataa kujumuika na wenzake na kunawakati alikataa kwenda skuli kutokana na watu kumdhalilisha.
JAMII
Habibu Khatib Faki wa Mjimbini Mkoani Pemba anasema,
suala hili mara nyingi huanza katika ngazi ya familia.
Anaeleza baadhi ya wazazi walezi au watu wa karibu na
watu wenye ulemavu, huwatambulisha kwa majina yatokanayo na aina ya ulemavu wao
badala ya majina yao ya kuzaliwa.
“Katika hili familia zinamchango mkubwa, kwani baadhi
yao hutumia majina yatokanayo na ulemavu wa mtu katika kumtambulisha, na hapo
jamii hujenga mazoea”, anafafanua.
Khulayta Hamad Shapandu wa Micheweni anasema, hali hii pia husababishwa na uwelewa
mdogo wa jamii kuhusu unyanyapaa na athari zake, kwa yeyote atakae fanyiwa.
Anaeleza kuwa, jamii haina uelewa wa nini maana ya unyanyapaa,
na wingi wanadhani unyanyapaa ni wa kimwili pekee na mengineyo hunaona ni
kawaida.
JUMUIYA
ZA WATU WENYE ULEMAVU
Maryam Mohamed Salim Afisa watu wenye ulemavu Pemba wa
‘UWZ’ anasema hili ni miongoni mwa tatizo kubwa linalowakumba watu wenye
ulemavu.
Anaeleza changamoto hii, ni ya muda mrefu ingawa kila
siku jamii inaelimishwa juu ya athari za jambo hili.
Mratibu baraza la watu wenye ulemavu Pemba Mashavu
Juma Mabrouk anasema, hali hii husababisha watu wenye ulemavu kujitenga na
kujiona wamekosa thamani.
Huathirika saikolojia ya watu wenye ulemavu na
kusababisha kujikataa na mwisho kuvunja
ustawi wao.
NINI
KIFANYIKE?
Hidaya Mjaka Ali ni mwenye ulemavu wa viungo anasema
vizuri jamii kuanzia ngazi ya familia,
kulipiga vita suala hilo, kwa kuhakikisha kila mmoja anakua na uelewa kuhusu athari za unyanyapaa.
Mashavu Khamis Omar wa Kangani Pemba anasema, vizuri
taasisi zinazohusika kushiriki katika kutoa elimu kwa jamii kuhusu nini
unyanyapaa.
Afisa Ustawi wa Jamii wa taasisi ya Early Childhood
Program Zanzibar (MECP-Z) Haji Ali Hamad anasema, ni vizuri, jamii kukubali
tofauti za kimaumbile zilizopo, ili kukuza utu na heshma ya kila mtu katika
jamii.
MWISHO

Comments
Post a Comment