TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI SIKU YA HAKI ZA BINADAMU DUNIANI 2025
Kamati ya Wataalamu wa Masuala ya Habari Zanzibar (ZAMECO) inaungana na wanaharakati, wanahabari, na watetezi wa haki za binadamu duniani kote, kuadhimisha siku ya Haki za Binaadamu ambayo hufanyika kila ifikapo tarehe 10 Disemba ya kila mwaka.
Kaulimbiu ya mwaka huu, haki za binadamu kama “Mahitaji ya Kila Siku”, inasisitiza kuwa haki hizi lazima zilindwe bila kusuasua kila siku, kwa kila mtu, na katika kila mazingira.
Katika maadhimisho ya mwaka 2025, ZAMECO inasisitiza kwamba uhuru wa kupata na kutoa taarifa ni nguzo muhimu ya utawala bora na msingi wa kulinda haki nyingine zote za binadamu.
Haki hii haipaswi kutazamwa kama ridhaa ya mamlaka bali kama wajibu wa kikatiba na kimataifa unaopaswa kuheshimiwa, kulindwa na kutekelezwa.
Tunawakumbusha wadau wote kuwa tangu kupitishwa kwa Tamko la Ulimwengu la Haki za Binadamu (UDHR) mwaka 1948 uhuru wa kujieleza umeendelea kuwa nguzo muhimu katika kuhakikisha kwamba jamii inakuwa na nguvu ya kushiriki, kuuliza, na kuhoji madaraka.
Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Zanzibar katika Ibara ya 18 zimeeleza haki hiyo ya kujieleza na kupata taarifa.
Hii hupelekea upatikanaji wa taarifa sahihi, waandishi wa habari na wananchi wanapata uwezo wa kuhoji, kushiriki, kuwawajibisha watawala na kuchochea uwazi katika masuala ya kijamii, kisiasa na kiuchumi.
Hata hivyo, pamoja na msingi huu muhimu, bado tasnia ya habari Zanzibar inakumbana na vikwazo vinavyozuia utekelezaji kamili wa haki hizi. Sheria zilizopitwa na wakati, mazingira ya hofu, vitisho dhidi ya waandishi, pamoja na ukosefu wa upatikanaji wa taarifa za umma kwa wakati.
Hali hii inadhoofisha uwezo wa vyombo vya habari kufanya kazi yao kwa uhuru na uadilifu na kuwanyima wananchi haki ya kupata taarifa sahihi, jambo ambalo linaathiri ushiriki wao katika maamuzi ya nchi.
Sheria hizo ni pamoja na Sheria ya Wakala wa Habari, Magazeti na Vitabu ya mwaka 1988 ilifanyiwa marekebisho mwaka 1997 pamoja na Sheria ya Tume ya Utangazaji Zanzibar ya mwaka 1997 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2010 ambazo zinaendelea kutoa mamlaka makubwa kwa taasisi za usimamizi na kuathiri uhuru wa vyombo vya habari kufanya kazi kwa weledi na bila ya hofu.
Katika taarifa yake ya mwisho kwa waandishi wa habari, kabla ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025, ZAMECO ilieleza masikitiko yake ya kuzorota kwa mazingira ya upatikanaji wa habari na ukiukwaji wa haki za kujieleza na kupata habari.
Miongoni mwa ukiukwaji huo ni kunyimwa taarifa muhimu kwa waandishi wa habari, kutishiwa kufungiwa kwa baadhi ya vyombo vya habari kutokana na kutokulipa ada na kurusha maudhui ambayo hayakuelezwa bayana tatizo lake.
Pamoja na changamoto hizo, ZAMECO inaona umuhimu mkubwa wa wadau wote kushirikiana kurejesha imani na kujenga mazingira salama na huru kwa uandishi wa habari.
Tunatoa wito kwa Serikali ya Zanzibar kufanya mapitio ya kina ya sheria za habari ili ziendane na hali ya sasa ya soko huria, maendeleo ya teknolojia, matakwa ya Katiba, viwango vya kikanda na kimataifa. Katika Maadhimisho ya Siku ya Haki za Binadamu ya mwaka huu, ZAMECO inasisitiza kuwa uhuru wa habari ni uti wa mgongo wa utawala bora na msingi wa demokrasia jumuishi.
Hakuna maendeleo, uwajibikaji, wala uchaguzi huru bila habari huru na waandishi walio salama. Kwa msingi huo, ZAMECO itaendelea kusimama imara kutetea haki, usalama, na maslahi ya waandishi wa habari Zanzibar, huku tukihamasisha wadau wote kutambua haki zao na kuzidai pale zinapokiukwa. IMETOLEWA NA:
Klabu ya Waandishi wa Habari Zanzibar (ZPC), Chama Cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania, Zanzibar (TAMWA-ZNZ) Waandishi wa Habari za Maendeleo Zanzibar (WAHAMAZA) Baraza la Habari Tanzania, Zanzibar (MCT, ZNZ) Jukwaa la Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania, Zanzibar (THRDC, ZNZ).
MWISHO
Comments
Post a Comment