NA HAJI NASSOR, PEMBA@@@@
WANANCHI 473, kati yao wanawake 295 na wanaume 178,
wa shehia za Kigongoni na Kiuyu Minungwini, wamefikiwa na elimu, ushauri na
msaada wa kisheria, ikiwemo utaratibu wa upatikanaji cheti cha kuzaliwa, kwenye
kambi ya msaada wa kisheria, iliyowekwa na Jumuiya ya Wasaidizi wa sheria wilaya
ya Wete ‘WEPO’.
Kambi hiyo ya siku moja, iliyofanyika leo Julai 7, kuanzia
saa 3:00 asubuhi hadi saa 9:30 jioni, wengi wa wananchi waliofika, walikuwa na
malalamiko ya kukosa vyeti vya kuzaliwa.
Ilifhamika kuwa, wingine ni wanaolalamikia kukosa
vitambulisho vya mzanzibari mkaazi pamoja na vile ya taifa.
Akizungumza na waandishi wa habari, Msaidizi wa sheria
kutoka ‘WEPO’, Siti Faki Ali, alisema kambi hiyo imewasaidia kuwapa mwanga, wa
aina ya changamoto iliomo ndani ya jamii.
Alisema, kambi hiyo imewaamsha kwamba, kazi ya kuwaelimisha wananchi kupitia wasaidizi wa sheria, inahitaji kuongezwa nguvu, kwani wapo ambao hawajui hata utaratibu wa kupata nyaraka hizo muhimu.
Siti, alifahamisha kuwa, jingine walilobaini kwenye kambi
hiyo, ni kuwepo kwa baadhi ya wananchi ambao, uwelewa wao juu ya kuitumia ofisi ya
sheha, uko chini.
Alieleza, wapo wananchi wakati wanawapa msaada wa kisheria, walidai
kuwa hawajui kuwa, kama una mri mkubwa unaweza kwenda wa sheha, na kuanza kwa hatua ya kwanza, kabla ya kufika wilayani.
Hata hivyo, alisema wapo wingine wameshindwa kufuatilia
wenyewe, maana walishaanza harakati ingawa nenda rudi ya wilayani, walikata
tamaa, kwa kupoteza gharama.
‘’Sisi ‘WEPO’ imetulazima kurudia tena kwenye sheha hizo
za Kigogoni na Kiuyu Minungwini, maana wapo wananchi ambao hatukuwamalizia taratibu
nyingine za kisheria,’’alifafanua.
Mapema Mratibu wa Mradi wa Uwezeshaji wa Kisheria na Upatikanaji
wa Haki ‘Legal Empowerment and Access to Justice’ Rashid Hassan
Mshamata kutoka WEPO, alisema mradi huo, unaovipengele kadhaa, kikiwemo cha
kuweka kambi katika shehia.
Alieleza kuwa, mradi huo ambao sasa unakwendea ukingoni
ndani ya mwaka huu, umeshasaidia mno, kwanza kwa kundi la wanafunzi na vijana.
kutambua viashria vya ukatili na udhalilishaji, kupitia makongamano na semina zao.
‘’Kwa hakika wenzetu wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa
Mataifa ‘UNDP’, kuturidhia mradi huu, wameiokoa jamii ya Wete, katika kujua
haki na wajibu wao, maana ilikuwa nyuma,’’alieleza.
Alifahamisha kuwa, wanatamani mno mradi kama huo, waupate
tena, ili kuendeleza nguvu ya elimu ya kisheria, pale walipofikia, ili kutimiza
mwelekeo wa ‘WEPO’ wa kujua haki na wajibu wao wanajamii.
Awali akizungumza kwenye baadhi ya mikutano, Mkurugenzi wa ‘WEPO’ Mwalimu. Hemed Ali Hemed, alisema sasa wapo wananchi wamejua haki na wajibu wao, kupitia
mradi huo.
Sheha wa Kiuyu Minungwini Nachia Yahya Salum, alisema ujio wa kampeni hiyo, sasa wananchi wake, wameamka katika kutafuta nyaraka za lazima, ikiwemo cheti cha kuzaliwa na cha ndoa.
Akizungumza kabla ya kuanza kwa kambi hiyo, Afisa sheria kutoka
Kamisheni ya Ardhi Pemba Asha Suleiman Said, aliwatahadharisha wananchi hao,
kuacha kununua na kuuza ardhi kiholela.
Mwanasheria Afisi ya Mwanasheria Mkuu, Ali Hamad Mbarouk,
alisifu ‘WEPO’ kwa kambi hiyo, ambayo imetoa fursa kwa wananchi wa shehia hizo,
kupata uwelewa wa changamoto zao za kisheria.
Hata hivyo, Msaidizi wa sheria, shehia ya Mtemani Wete Said Rashid
Hassan, alisema kazi iliyofanywa na ‘WEPO’ inafaa kuungwa mkono na jamii, ili
kuendelea kupata uwelewa wa kisheria.
Aidha vilabu kama hivyo kupitia mradi huo, vimeanzishwa shehia za Uwondwe,
Mzambarauni, Mlindo, Utaani, Kipangani, Bopwe na Kinyasini.
MWISHO
Comments
Post a Comment