NA HAJI NASSOR, PEMBA@@@@
JUMUIYA ya Wasaidizi wa sheria wilaya ya Wete
Pemba ‘WEPO’ asubuhi hii, inatarajia kuendesha kambi ya siku moja, ya msaada wa
kisheria kwa wananchi wa shehia za Kigongoni na Kiuyu Minunwgini wilayani humo,
bila ya malipo.
Kambi hiyo, ambayo inatarajiwa kuwakusanya zaidi ya wananchi
500 wa shehia hizo, ni sehemu ya utekelezaji wa mradi wa kupambana na ukatili
na udhalilishaji, chini ya ufadhili wa shirika la UNDP.
Akitoa taarifa kwa waandishi wa habari, Mratibu wa mradi
huo, Rashid Hassan Mshamata, alisema kambi hiyo itawahusisha wataalamu wa
masuala ya ardhi, mahakama, ofisi ya Mkurugenzi wa mashtaka, ofisi ya Mwanasheria
mkuu.
Alieleza kuwa, wataalam wingine watakaokuwepo kwenye kambi
hiyo ni Jeshi la Polisi, dawati pamoja na wasaidizi wa sheria, kutoka Jumuiya
ya wasaidizi wa sheria wilaya ya Wete Pemba ‘WEPO’.
Aliwataka wananchi wa shehia hizo na nyingine, kufika kwenye
kambi hiyo ya siku moja, ili kuwasilisha matatizo yao ya kisheria, ikiwemo migogoro
ya ardhi, mirathi, matunzo ya huduma za mtoto, migogoro ya ndoa.
Eneo jingine ambalo aliwakaribisha wananchi hao, ni wale
waliochukuliwa ardhi zao bila ya kulipwa fidia, waliokosa vitambulisho, vyeti
vya kuzaliwa, vya ndoa pamoja kupata elimu ya kisheria bila ya malipo.
‘’Niwaombe sana wananchi wa shehia hizi, kuitumia siku ya
leo kuanzia saa 3: 00 hadi saa 10: 00 jioni, kufika skuli ya Minungwini,
kufikisha malalamiko yao ya kisheria, ili kupatiwa ufumbuzi wa papo hapo,’’alifafanua.
Mapema Mkurugenzi wa Jumuiya hiyo, Hemed Ali Hemed, alisema
fursa hiyo ni adhimu na adimu kwa timu ya wataalamu wa masuala ya sheria,
kuwafuata wananchi walipo.
‘’Ijapokuwa kazi ya wasaidizi wa sheria ni kuwafuata wananchi
walipo na kuwatatulia shida zao za kisheria, lakini kwa kambi hii ambayo
itahusisha wataalamu wa masuala ya kisheria, ni muhimu mno,’’alifafanua.
Msaidizi wa sheria, shehia ya Mtemani Wete Said Rashid
Hassan, alisema kazi iliyofanywa na ‘WEPO’ kuupata mradi huo ni jambo jema,
hasa kwa wananchi kupata haki zao.
‘’Ni kweli leo hii, skuli ya Minungwini ni fursa ya bure kwa
wananchi kupata ufumbuzi wa changamoto mbali mbali za kisheria, maana kila aina
ya wanasheria watakuwepo,’’alifafanua.
Hata hivyo, alisema bado wasaidizi wa sheria wataendelea
kuwa mwega kwa wananchi wasiokuwa na uwezo, kupata haki zao za kisheria.
WEPO, inaendelea kutekeleza mradi wa upatikanaji haki na
kupamba na ukatili na udhalilishaji, ambapo mradi huo unatarajiwa kumalizika
mwishoni mwa mwaka huu.
Tayari ‘WEPO’ kupitia mradi huo, umeshaanzisha vilabu vya
kupambana na ukatili na udhalilishi kwa skuli kadhaa, ikiwemo Uwondwe, Chasasa,
Pandani na baadhi ya madrasaa za qur-an.
Aidha vilabu hivyo kupitia mradi huo, vimeanzishwa shehia za
Uwonde, Mzambarauni, Mlindo, Utaani, Kipangani, Bopwe na Kinyasini.
MWISHO
Comments
Post a Comment