NA MWANDISHI MAALUM@@@@
MENEJA miradi kutoka Chama
cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania, Zanzibar (TAMWA ZNZ) Nairat Abdulla
amewaomba wanawake kutumia vyombo vya habari kwa lengo la kutangaza kazi zao wanazozifanya.
Akifungua mafunzo ya siku mbili
ya kuwajengea uwezo wakulima viongozi kutoka shehia nne (4) za Unguja, juu ya
umuhimu wa kutumia vyombo vya habari, yaliofanyika ofisi za TAMWA-ZNZ Tunguu,
Mkoa wa Kusini Unguja, amesema wanawake wanajishughulisha na harakati mbalimbali
zikiwemo za uzalishaji pamoja na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi lakini
bado sauti zao hazisikiki ipasavyo kupitia vyombo vya habari.
Hivyo amewaomba wanawake hao
kutumia vyombo vya habari hasa mitandao ya kijamii, kuelezea mafanikio na
changamoto zinazowakabili katika kupambana na mabadiliko ya tabianchi ili
kufikisha ujumbe kwa wahusika na hatimae kupatiwa ufumbuzi.
Akiwasilisha mada inayohusu
vyombo vya habari, Meneja Mawasiliano kutoka TAMWA ZNZ, Sofia Ngalapi amesema wanawake
wakulima viongozi wanafanya kazi nzuri ya kutunza mazingira na kukabiliana na
mbadiliko ya tabianchi, hivyo wapaze sauti kutangaza kazi wanazozifanya kupitia
vyombo vya habari kwa lengo la kuhamasisha jamii kuwa vinara kupitia masuala ya
mabadiliko ya tabianchi.
Khairat Haji, Afisa
mawasiliano kutoka TAMWA ZNZ akiwasilisha mada inayohusu mitandao ya kijamii, amesema
mitandao ya kijamii ni njia moja wapo ya kujitangaza endapo itatumika ipasavyo
hasa katika dunia hii ya sayansi na teknolojia.
Aidha amesema ili kuepuka
udhalilishaji kupitia mitandao ya kijamii, ni vyema kuepuka kuchapisha taarifa na
picha zinazohusu maisha yao binafsi kwa kulinda usalama wao na badala yake kuitumia
kama njia moja ya kujiongezea kipato.
Nao wakulima viongozi kutoka
shehia nne (4) za Unguja, Mkoa wa Kusini, ambazo ni Bungi, Unguja Ukuu, Uzi na
Ng’ambwa wamesema wamefarajika kupata mafunzo hayo kupitia program ya Zanzadapt
na wameahidi kuwa mabalozi wazuri kwa kufikisha ujumbe kwa jamii.
Mradi unaohusu nafasi ya
mwanamke kiongozi katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, (Zanzadapt) umejikita
kuangalia maeneo manne yakiwemo uhifadhi wa mikoko, kilimo mseto, wanawake
viongozi na masuala ya jinsia ambao unatekelezwa kwa pamoja na TAMWA ZNZ,
Jumuiya ya misitu Pemba (CFP), Jumuiya ya misitu Kimataifa (CFI) kwa
kushirikiana na Ubalozi wa Canada.
MWISHO
Comments
Post a Comment