BAKAR KHAMIS, PEMBA@@@@
WANANCHI kisiwani
Pemba, wameaswa kuacha tabia ya wizi wa zao la karafuu, kwani kufanya hivyo pia
wanaweza kuingizwa kwenye vitendo vya ukatili na udhalilishaji.
Hayo yameelezwa na
Mkaguzi wa Polisi Inspekta Hamad Ali Faki, kwenye kikao cha kuimarisha maadili
ndani ya jamii, wakati akizungumza na wananchi wa shehia ya Kukuu Kangani
wilaya ya Mkoani.
Alisema wapo baadhi
wanajamii, wamekuwa na tabia ya kukwapua karafuu za wenzao wanapokuwa shambani,
jambo ambalo linaweza kusababisha madhara zaidi, ikiwemo udhalilishaji.
Alieleza kuwa, zipo
kesi kadhaa kila unapofika msimu wa uchumaji wa zao karafuu, hujitokeza
zikiambatana na wizi wa karafuu.
"Ndugu zangu wanajamii,
niwasihi sana kujiepusha na dhulma ya wizi wa karafuu, maana ndio chanzo cha
udhalilishaji, ikiwemo watoto kupewa mimba, kulawitiwa na wengine kuhujumiwa
kwa kipgo,"alifafanua.
Katika hatua
nyingine, aliwakumbusha wazazi na walezi, kutowaachia watoto wao kuzurura ovyo,
kwenye mashamba ya wakulima pasi na ruhusa ya mwenye mali.
‘’Watoto wetu
wanakuwa ndio wa kwanza, kujiingiza kwenye mashamba ya wakulima kwa dhana ya
kuokota karafuu zilizoanguka ‘mpeta’, ingawa huishia na wizi, kw ahili
tujitahidini,’’alifafanua.
Aidha Mkaguzi huyo
wa Polisi Inspekta Hamad Ali Faki, aliwataka wakulima na waliokodi mashamba ya mikarafuu,
kujiepusha kuuza karafuu zao kwa watu wasieleweka, na badala yake wazipeleke Shirika
la Taifa la Biashara ‘ZSTC’.
Alifahamisha kuwa,
kuziuza kinyume na ZSTC, ni hujma nyingine ya kiuchumi, hivyo hawana budi kuondokana
na tabia hiyo.
‘’Wakulima na
waliokodi mashamba ya mikarafuu, nawakumbusha kuwa, baada ya karafuu kuchumwa
na kukauka, ni hatua ya kuzipeleka ZSTC kwa kuziuza na sio kwa walanguzi,’’alifafanua.
Mkaguzi huyo wa
Polisi, alitumia nafasi hiyo, kuwasihi wanaume, kuwa makini na ndoa zao, na
kuacha kuwacha kuwaruhusu wake zao, kwenda kuokota karafuu ‘mpeta’.
"Wanaume
acheni tabia ya kuwapa ruhusa wake zenu kwenda mpeta, wakati unajua wewe huna
shamba wala hujakodi, ni chanzo cha kuvunjika kwa ndoa, na kesi za aina hiyo
tumeshawazi kuzipokea,’’alisema.
Omar Mwadini Omar
kwa niaba ya wazazi wenzake, alisema jambo hilo lipo na limezoeleka, lakini kwa
sasa watalidhibiti kwa pamoja na halitatokea tena.
Nae Mohamed Omar
Haji, alieleza kuwa, watoto na wanawake, wamekuwa wakiranda kwenye mashamba ya
wenyewe, na kisha ili kurudi na karafuu, baadhi yao mpaka wadhalilishwe.
Mwisho
Comments
Post a Comment