NA HAJI NASSOR, PEMBA@@@@
JESHI la Polisi Tanzania, limesema kuwa,
watu 3,192 wamepoteza maisha nchini kote, kufuatia ajali za barabarani, katika
kipindi cha kuazia mwaka 2022 hadi Disemba mwaka 2023.
Kati ya hao waliopoteza maisha, watu 1,545
waliripotiwa mwaka 2022 na watu wengine 1,647 waliripotiwa kuanzia Januari hadi
Disemba mwaka 2023.
Aidha, kwa upande wa Zanzibar, kuliarifiwa
kuwepo kwa watu 297 walipoteza maisha, na kati yao mwaka 2022 walikuwa 137 na
mwaka 2023 idadi iliongezeka 23, na kufikia watu 160 walipoteza maisha.
Hii ni kwa mujibu wa ripoti ya takwimu
za uhalifu na matukio ya usalama barabarani, ya Jeshi la Polisi Tanzania ya mwaka
2023, iliyosainiwa na Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania Camillus M. Wambura na
kuweka kwenye tovuti ya Ofisi ya taifa ya takwimu Tanzania.
Ripoti ikaeleza kuwa, watu hao
waliofariki, walitokana na matukio ya ajali 3,453 ambapo kati ya hayo, mwaka
uliobeba ajali nyingi ni mwaka jana.
Ambapo kulikuwa na matukio 1,733 na mwaka 2022 yakiripotiwa kupungua 13 na kuwa na matukio1,720.
Kwa upande
wa Unguja na Pemba, matukio ya ajali ya vyombo vya moto, yalikuwa 358, kati ya
hayo mwaka 2022, kuliripotiwa matukio 166 na mwaka 2023 yaliongezeka 26, na kuifanya
idadi ya 192.
Aidha ripoti hiyo ikafafanua kuwa, katika matukio yote ya usalama barabarani, matukio makubwa (ajali) yalikuwa 1,733 na matukio madogo yalikuwa 3,170,073 kwa mwaka 2023.
Ikilinganishwa
na matukio makubwa 1,720 na matukio madogo 2,543,482 yaliyoripotiwa kwa mwaka 2022.
‘’Hii ni ongezeko
la matukio makubwa
13 sawa na asilimia 0.8 na
ongezeko la matukio madogo 626,591 sawa na asilimia 24.6,’’ ilifafanua sehemu
ya ripoti hiyo ya Jeshi la Polisi Tanzania.
Ripoti hiyo ikafafanua kuwa, kati ya matukio makubwa 1,733,
ajali za pikipiki kwa mwaka jana zilikuwa 431, ikilinganishwa na matukio 448
yaliyoripotiwa mwaka 2022.
Eneo jingine la ripoti hiyo, ni kuwepo kwa majeruhi 4,994
kwa miaka miwili, ambapo mwaka 2022 kuliripoti majeruhi 2,278 na mwaka 2023 ulikuwa
na majeruhi 2,716.
Majeruhi hao wote, walitokana na idadi ya ajali 941
zilizosababisha majeruhi, zilitokea mwaka 2022 kwa ajali 470 na mwaka jana kukiripotiwa
ongezeko la ajali moja.
Baadhi ya madereva
kisiwani Pemba, wamesema ajali kadhaa, husababishwa na uchakavu wa miundombinu
ya barabara.
Ali Khamis Omar, anaefanyakazi ya gari ya mzigo Wete,
alisema uchakavu uliopo kwa baadhi ya barabara za Pemba, huchangia kutokezea
kwa ajali ambazo zinaweza kuzuilika.
''Hakuna hata dereva mmoja, anaetoka kwake anapoingia
barabarani asababishe ajali, bali ubovu na uchakavu wa barabara ni chanzo,’’alisema.
Nae Khalfan Mjaka Khalfan mwenye gari ya abiria ya Mkoani-Chake
chake, alisema miaka kadhaa barabara ya Mkoani, imekuwa na mashimo yenye kina
kirefu.
‘’Uwepo wa mashimo yenye kina kirefu, uchakavu na ongezeko
la vyombo vya moto na ufinyu wa barabara, ni chanzo kikuu cha ajali za barabarani,’’alisema.
Nae dereva wa boda boda eneo la Chambani Khamis Mcha
Khamis, alisema upo uzembe kwa baadhi yao, ambao wakati mwingine, husababisha
ajali.
‘’Dereva hujifanya anawahi kukatiza mbele ya gari, au
wakati mwingine kuegesha kwenye mipindo kwa kushusha au kuchukua mzigo, hapo
hutokezea ajali ya kizembe,’’alisema.
Afisa Mdhamini wizara ya Masiliano, Uchukuzi na Usafirishaji
Pemba Ibrahim Saleh Juma, alisema kama madereva hawakuamua kuzifuata kwa
vitendo alama za barabarani, matukio ya ajali hayatopungua.
Akiifungua barabara ya Birikau Chake chake hivi
karibuni, Rais wa Zanzibar Dk. Hussein Ali Mwinyi, aliwakanya madereva, kuacha
kuzitumia vibaya barabara mpya.
Mwisho
Comments
Post a Comment