NA NA HAJI NASSOR, PEMBA@@@@
NI ya miaka 58 imepita sasa, kila mmoja hawezi kuamini, mafanikio makubwa kwa
wananchi wa visiwa vidogo vigodo vilivyoko wilaya ya Wete Pemba yaliofikiwa.
Mwaka 2022, ndoto za wananchi wa visiwa vya Njau na Kokota, zimetimia baada ya Shirika la Umeme Zanzibar ‘ZECO’, kuzima kibatali na kuwasha umeme wa sola kwa wananchi wa visiwa hivyo.
WANANCHI WENYEWE
Ali Oma Khami anayeishi Kisiwa cha Njau, anasema mabadiliko makubwa wanaendelea kutokea, ikiwemo kukua kwa biashara kufuatia kuwepo kwa nishati ya umeme.
''Umeme ni moja ya nishati inachorahisisha maendeleo ya sehemu yoyote ile, ni wazi na sisi tumeanza kunufaika na mabadiliko makubwa ya Serikali kutupatia miundombinu ya umeme,” anasema.
Chumu Omar Kai, kwa sasa wanapata kwa matumizi mbali mbali
ikiwa ni pamoja na kuweka chaji, ambapo zamani walilazimika kwenda nje ya
kisiwa masafa ya kilomita 30 hadi mjini Wete.
Nae Nyezume Abdalla Ali anawataka wenzake kuilinda miundombinu ya hio, ili iweze kudumu kwa muda mrefu, kwani huduma hiyo wameikosa kwa muda mrefu.
Mkaazi wa kisiwa cha Kokota Hamad Shamis anasema, amefurahi
sana kuona umeme unawaka ndani ya kisiwa chao, kwani hakuwahi kuwaza kwamba
kuna siku kisiwa hicho kitakuwa na umeme.
“Sisi tunajua watu wa visiwani tunasahaulika kwa mambo
mengi, lakini sasa tunajiona kama wafalme, huduma zote tulizokuwa tukizifuata eneo la Wete
sasa hatufuati tena,”anasema.
Tatu Bahati mkaazi Kokota anaeleza kuwa, umeme utawasaidia
kwa watoto kusoma katika masomo ya ziada muda wa usiku, ili kuweza kuongeza
ufaulu kwenye masomo yao.
WAVUVI
WANASEMAJE
Omar Mcha Said mkaazi wa Mbuyuni kisiwani hapo anasema, umeme huo unaendelea kuwasaidia kuhifadhi samaki wao na kuuza
kwa bei wanayoitaka.
“Awali wachuuzi walikuwa wakitulalia kwa bei, kwa kujua tusipowauzia wataharibika, lakini sasa kama wamebakia tutawahifadhi kwenye Friji na kuwauza siku ya pili,”anasema.
Anafafanua, kwa sasa hawawezi kuuza kama samaki, Pweza na Ngisi
kwa hasara kama ilivyokuwa zamani, badala yake ataweza kuhifadhi katika majokofu yaliyomo ndani ya
Kisiwa hicho.
Talib Issa wa kisiwa cha Kokota anaeleza, sasa watalazimika kuhifadhi vitu vyao kupitia majokofu (mafriji), wala hawataweza kuuza kwa bei ya hasara, kama ilivyokuwa zamani.
“Suala la kulaliwa kwa bei na wanunuzi litapungua, sasa tutauza kwa bei tunayotaka wenyewe, na tunaona sasa thamani ya kazi yetu ya uvuvi,''anasema.
WAFANYA
BISHARA WANASEMAJE
Juma Ali Juma (mlemavu wa viungo), mkaazi wa Kisiwani hapo, anasema wamejawa na furaha baada ya kuona kazi ya miuondombinu ya umeme imeanza kutumika.
Kwani anasema bishara yake ya kukusanya na kusafirisha samaki nje ya kisiwa cha Pemba, imeongezeka thamani baada ya kupatiwa huduma hiyo.
''Nilikuwa nalazimika samakini ama pweza nikishawanunua niwapeleke Wete, kukodi friji kwa shilingi 20,000 ingawa sasa ninalo ndani na biasha imeshakua,''anaeleza.
“Sasa tumeanza kujiona ni wananchi wa awamu ya nane kweli, biashara zetu hata za juisi, barafu na hata fotokopi zitakuweko Kisiwani hapa ili kuwasaidia wanafunzi,”anasimulia mfanyabiasha Asha Haji Mkema.
Anasema miradi midogo midogo kama juisi, maji baridi, soda
sasa zote zitapatikana ndani ya kisiwa, wamejipanga kuhakikisha wanakuwa na
vifaa vya kisasa vya kufanyia kazi hiyo.
Anasema umeme wa jua ni tafauti na umeme wa Tenesco, kwani
umeme huo hautokatika katika na wataweza kuhifadhi samaki wao katika majokofu
na kuuza kwa bei wanayoitaka.
VIONGOZI
WA DINI WAO WANASEMAJE
Sheikh Othman Khamis Ali anasema umeme huo kuanza kufanya kazi, ibada zinafanyika kwa muda mkubwa, darasa za usiku wanaziendesha kwa muda mkubwa tofauti na zamani.
“Umeme umepeleka furaha ndani ya kisiwa chetu, shida ndogo ndogo sasa zitaondoka, adhana itasikika kikamilifu kwa kutumia vipaza sauti”, nasema.
Anaeleza, wanafuzi wa madrasa hawatopiga tena kelele kutokana
na joto kali, kawani tayari wameshawawekea mafeni na hata darasa za usiku
zitakuwepo chuoni,” anasema.
ZECO
LINASEMAJE
Mhandisi wa mradi kutoka Kampuni ya Photons Energy Erick
Kimambo, anasema umeme wa jua unaozalishwa ni sawa sawa na umeme ZECO, unaweza kutumia
vifaa vyote vinavyotumia umeme, hata kama mafundi uwashi watakuwepo.
“Kinachotafautisha hapa ni nishati ya kuzalishiwa umeme, TENESCO
na ZECO wanatumia maji, ila huu wa visiwani unatumia vyanzo vya jua, lakini
matumizi yake ni sawa sawa”, anafahamisha.
Mhandisi Mkaazi wa mradi huo Daniel John, alisema kwa sasa
mradi huo, umekamilika kwa asilimia 100, baada ya kufungwa mitambo husika ya kuzalishia
umeme, ikiwemo vioo, betri na ujenzi wa kibanda cha kuwekea mtambo.
“Huu ni umeme mzuri ambao haukati kama ulivyo umeme wa
ZECO au TENESCO, huu zaidi unahitaji nguvu za jua na hata jua likiwa halipo
usiku chaji ya betri ndio zinazotumika”, anasema.
Afisa Mawasiliano na huduma kwa wateja ZECO Pemba Haji
Khatib Haji, anasema jumla ya kaya 84 zimeungiwa huduma ya umeme katika kisiwa
cha Kokota na Njau ni kaya 44.
Wananchi wa visiwa hivyo walipata bahati ya pekee ya
kuungiwa umeme kwa shilingi 50,000 badala ya shilingi 200,000 kama ilivyo
maeneo mengine.
“Tumetoa punguzo hili la fedha kulipa, kwa sababu ya hali
zao kimaisha, ila hata hivyo baadhi yao wameshindwa, hivyo tumetoa ‘ofa’ ya
Umeme wa mkopo kwa kulipa 30,000 pia wananchi hawana”, anasema.
Njau na Kokota ni miongoni mwa visiwa vilivyobahatika
kupata mradi wa umeme wa jua, umeme ambao hatokatika ovyo ovyo kama ulivyo wa
gridi.
Ali Faki Ali ambae ni msimamizi wa mradi wa umeme wa jua
kutoka ZECO Pemba, anasema mradi huo wa umeme katika visiwa cha Njau na Kokota,
umegharimu Dola za kimarekani 458,043.92 kwa ufadhili wa NURUWE FUND.
Anaeleza, uwezo wa mtambo ni kuzalisha kilowatt 50 na
kutoa huduma kwa wateja 100 kwa Njau na sasa ni wateja 50 tu, ambapio kisiwa
cha Kokota kuzalisha kilowati 80 na kutoa huduma zaidi ya 150 na ingawa kwa
sasa ni wateja 90 tu.
Mradi huo unatarajiwa kukamilika 2025 na utaweza kupunguza tatizo la upungufu na ukosefu wa umeme mara kwa mara.
“Mradi wa Visiwani ni uwekejazi mkubwa umefanywa na ZECO, ni
ishara tosha ya kufikisha umeme kwenye maeneo ambayo umeme wa gridi hauwezi
kufika,” anasema.
Tayari tumeshaitekeleza ilani ya CCM 2020/2025, kwa asilimia 90 hadi 95, kwa kufikisha umeme vijijini Unguja na Pemba, pamoja na visiwa vidogo vidogo, ikiswemo Kisiwa Panza, Makoongwe, Fundo, Uvinje, Kojani, Njao na kokota.
MWISHO
Comments
Post a Comment