NA HAJI NASSOR, PEMBA@@@@
NI majira ya saa saa 2:00 asubuhi, hali ya hewa ikiwa ya baridi, na jua nalo hilooo…. linaanza kupanda juu na miale yake kwa mbali, ikijitokeza kwenye miti mirefu.
Nipo kijiji cha Chimba wilaya ya Micheweni Pemba, ni kilomita zisizozidi 45, kutoka mji mkuu wa Pemba, Chake chake.
Hapa mbele yangu kuna bonde lenye urefu wa uwanja mmoja na nusu wa mpira wa miguu, likizungumkwa na minazi na migomba pembezoni yake.
Pembezoni kuna kisima kidogo, kilichochimbwa kwa kutumia jembe la mkono, na kwa mbali naona tanki lenye ujazo wa lita 5000, ikitiririsha maji kwenye mboga mboga.
Punde si punde, niliona wanawake wawili wakiwa na visu mkononi mwao, nililazimika kurudi nyuma hatua tatu, na nikawapisha njia, kwa hadhari.
Baada ya kuwasalimia, mmoja aliyekuwa nyuma, hakusita kuniuliza ikiwa nahitaji bilingani, mchicha ama tungule, jawabu likawa hapana.
aa…. haaa.... kumbe walikuwa ndio wenyeji wangu, ambao ni wanaushirika wa ‘Mwanamke anaweza’ ambao baada ya kuzungumza nao, tukiwa tumesimama, walidakiza hayo ndio matunda ya TASAF.
USHIRIKA WA MWANAMKE ANAWEZA
Sharafe Salim Hamad, kumbe ndio Katibu wa ushirika huo anasema, uliasisiwa mwaka 2019, lengo hasa ni kuwa na eneo la uhakika, la kujipatia fedha kwa ajili ya akiba.
Kumbe wanachama wote 10 waanzilishi na saba (7) waliobakia sasa wote ni walengwa wa mpango wa kunusuru kaya maskini, chini ya TASAF, kwa upande wa Pemba.
Anasimulia kuwa, wakati wanaendelea kupokea ruzuku hiyo ya TASAF kati ya shilingi 30,000 hadi shilingi 44,000 na wakati mwengine hadi shilingi 60,000, walihimizwa namna ya kuziendeleza.
‘’Kwanza, sisi tunaopokea ruzuku hiyo, na kuanzia mwaka 2018 tuliamua kuanzisha mpango wa kuweka na kukopa ‘kisanduku’ ili sasa, fedha hizi tunazopokea ziweze kuzaa,’’anasema.
Ndio hapo, walipoamua kuanzisha ushirika na kuupa jina la ‘mwanamke anaweza’ ambao unajishughulisha na kilimo cha mchicha, bilingani, tungule na bamia.
Walibuni mradi huo, ili kila mwanachama awe na uhakika wa kujipatia fedha, kwa ajili ya kujiwekea hakiba, na tayari waliwahi kuvuna mara tatu, na kujipatia faida.
Mwenyekiti wa ushirika huo, Fatma Khamis anasema mavuno ya kwanza, walijipatia wastani wa shilingi 500, 000 na baada ya kutoa gharama pamoja na za mfuko, waligawana shilingi 50,000 kwa wanachama wao saba waliobakia.
Mara ya pili, wanawake hawa saba waliomo kwenye kilimo cha mboga mboga, walifanikiwa mno, hasa kwenye kilimo cha tungule, na walijipatia shilingi 700,000.
Mwenyekiti anasema, kisha baada ya kutoa gharama kama za dawa na kuweka fedha za mfuko, kila mwanachama waliondoka na donge la shilingi 70,000.
‘Wanaushirika hawa, wako kwenye kikundi cha hisa, lakini baadhi yao wamo kwenye ushirika wa kilimo cha mboga mboga, hivyo faida ya shilingi 70,000 wengine wanazitumia kujiwekea akiba,’’anasimulia.
Mwenyekiti anakumbuka sana, kuwa wakati wanaanza kupokea ruzuku hiyo ya TASAF, walielekezwa namna ya kuzikuza na kuziendeleza fedha hizo.
Mwanachama wa ushirika huo, Maryam Othman Faki miaka 65, anasema, sasa anajua wapi pakwenda anapokuwa na shida ya fedha, tofauti na hapo zamani.
‘’Kwa miaka zaidi ya 56 katika maisha yangu, shilingi 100,000 zikiwa zangu binafsi kuzikamata ni shida, lakini sasa kupitia ushirika huu, pamoja na hisa sina wasi wasi,’’anaeleza.
Maryam, tayari ameshawahi kukopa fedha na mara ya kwanza shilingi 100,000 kwa ajili ya matibabu ya mtoto wake, na mara ya pili, kwa kiwango kama hicho kwa ajili ya kufanikisha harusi.
Wakati huu akiendelea kupokea ruzuku za TASAF kuanzia mwaka 2014 hadi sasa, anajigamba kuwa, wajukuu zake wanaomtegemea, wanakwenda skuli na vifaa kamili.
‘’Hata milo mitatu sasa, ni jambo la kawaida, na suala la kuwa na akiba kati ya shilingi 300, 000 hadi shilingi 500,000 sina wasi wasi,’’anasimulia.
Lakini Mwanaisha Hassan Shaib, anasema kwa yeye ruzuku ya TASAF ni zaidi ya kipato, maana sasa hata ndoa yake imeimarika, baada ya muume wake kumuona ana uhakika wa kipato.
''Mimi zamani ilikuwa muume wangu hanishirikishi kwa jombo lolote, maana siku na nguvu kifedha, ingawa kwa sasa hata hivi juzi aliponunua gari ya Ng'ombe kwanza tulikaa mkekani,'anasema.
Hata Bimkubwa Hemed Juma, anasema kipato ni jambo moja, lakini la pili ni kuimarika kwa mapenzi baina yake ni muumewake na hata ndugu wa muuume wake.
'Kwa sasa hata muume akiondoka siku tano, mimi naiendesha familia kwa chakula cha asubuhi, mchana na jioni na hili sasa limenipa heshima kwa muume na jamaa zake,''anakiri.
Muume wake Haji Khamis Haji, anakiri kuwa mwanamke mwenye kipato na ndoa yake nayo huimarika, maana mchango wake sio wa maneno tu.
''Mimi hata mwaka jana nilimkopa shilingi 500,000 nimeshanunua piki piki na sasa nimeshalipa fedha zote, kwa hakika TASAF ni zaidi ya ruzuku,''anakiri.
KABLA YA UJIO WA TASAF
Wenyewe wanasema kwanza, hawakufikiria kuanzisha kisanduku cha kuweka fedha na kukopa, kutokana na kukosa msingi wa awali wa fedha.
Fatma Khamis, anasema shida waliokuwa nayo ya maisha hakuna hata mwananchi wa moja wa kijijini hapo, aliyefikiria kuita wenzake kuanzisha ushirika.
‘’Mwaka mmoja, tuliwahi kukutana kutaka kuanzisha mpango wa kuweka fedha na kukopa, ingawa ulikufa ndani ya siku saba, kwa ukosefu wa mtaji,’’anasimulia.
Maryam Othman Faki, anasema hakuwa na uhakika wa chakula kabla ya ujio wa mpango wa TASAF, kutokana na maisha yake kuwa ya kubahatisha.
Kilimo cha mihugo, migomba na mpunga ndio shughuli yake kuu, aliyokuwa akiitegemea, ambapo kipindi cha kiangazi hali duni ya maisha iliongezeka kwake.
‘’Sikufikiria kuwa siku moja, nitakuwa na uwezo wa kutimiza milo mitatu kama walivyo watu wengine, maana ilikuwa zaidi naangalia mlo wa jioni, baada ya watoto kurudi masomoni,’’anasema.
Hata Sharafe Salim Hamad, anasema sasa TASAF imekuja kumvisha nguo ya moyo na imani, na kujiona ni sehemu ya wananchi, wenye kipato cha kati.
‘’Niliwahi kukaa zaidi ya miaka saba, sikuwa natimizi michango ninayotakiwa kutoa na familia, maana nilikuwa na njia moja tu ya kujipatia fedha, pale ninapoouza ndizi,’’anasema.
Kwa wakati huo, watoto wake wawili waliwahi kusimamisha masomo, baada ya kukosa ada za mwaka, na mmoja hakufanya mtihani wa wilaya, kwa kukosa fedha za michango.
Kwa sasa, anasema wakati huu akipokea ruzuku akiwa mlengwa wa kaya maskini, ni mwanachama wa mfuko wa kuweka na kukopa na ushirika wa kilimo cha mboga mboga.
MALENGO YAO YA BAABADAE
Ushirika huo, unakusudia kuendeleza mradi wa ufugaji kuku 500 wa kienyeji, utengenezaji wa vipochi na mikoba ya punje na mafuta maalum, kwa ajili ya tiba ya ngozi.
SHEHA
Sheha wa shehia ya Chimba wilaya ya Micheweni, Saleh Salim Khamis anaseme, moja ya eneo analojivunia ni ushirika wa ‘Mwanamke anaweza’ ambao umeibeba shehia kati ya vyama vya ushirika saba, vilivyoanzishwa shehiani humo.
Akasema kuwa, TASAF haikupoteza fedha kwa kuwa na walengwa 168 waliomo kwenye mpango wa kunusuru kaya maskini, kati ya wananchi wote 4,215.
“Kwenye shehia yangu, pamoja na mlengwa mmoja mmoja kujiajiri, lakini ipo miradi ya mikubwa ambayo wananchi wote wamenufaika nayo,’’anasema.
Hata hivyo, Katibu wa sheha wa shehia hiyo Omar Salim Hamad, anasema TASAF imeikomboa shehia yao, kwa kuwepo vikundi ambavyo kwa njia ama nyingine, vimeshaondokana na umaskini wa kipato.
‘’Mfano ushirika wa ‘maskini hajengi’ wanaolima mboga na ufugaji wa kuku, ‘lako jicho’ ni ushirika ambao unajishughulisha na ufugaji, hisa na kilimo cha mboga na kukusanya walengwa 20,’’anasimulia.
TASAF
Mratibu wa TASAF Pemba Mussa Said, anasema wapo walengwa 14,280 kwa Pemba, ambao wanaendelea kupata fedha za kunusuriwa na umaskini.
Walengwa hao, wapo kwenye shehia 78 ikiwemo za Tumbe Mashariki, Chimba, Makangale, Kiwani, Ndagoni, Ukunjwi na Fundo.
Ambapo tayari TASAF Pemba, imestumia shilingi bilioni 14. 4 kwa ajili ya kuwapa ruzuku walengwa hao, fedha za kazi na zile za msingi pamoja na za masharti.
Tayari, kila shehia kati ya hizo 78, zimesafikiwa na wastani wa zaidi ya shilingi milioni 230, ambapo kwenye walengwa wote 14,280 wa Pemba, kila mmoja ameshasaini zaidi ya shilingi milioni 2, ingawa inategemeana na eneo husika.
Mratibu wa TASAF alimtolea mfano wa kuigwa mlengwa kama Khadija wa Chimba, Amina wa Mgogoni na mwenzake Mfaki kuwa wameyatekeleza kwa vitendo malengo hasa ya mpango huo.
‘’Wezetu kama hawa ambao wapo zaidi ya 5000 kwa Pemba, wamekwenda sambamba hasa na malengo na mwelekeo wa TASAF, wa kumtoa mwananchi katika unyonge hasa wa kipato,’’anasema.
Jengine ambalo ni jema ni kwa walengwa hao kuanzia mwaka 2014 hadi mwaka 2108 kuibua miradi 146 kwa ajili ya wananchi kama vile ufufuaji wa mito ya asili.
‘’Mfano wa miradi hii hata Makangale upo wa upandaji miti, ujenzi wa matuta ya kuzuilia maji ya chumvi mfano Ndagoni, Tumbe na Micheweni,’’anafafanua Mratib wa TASAF Pemba.
Achia mbali idadi ya watu 5000 waliojiwekeza wenyewe, vipo vikundi 942 vikizaa walengwa 12,000 vilivyoanzishwa, kuanzia mwaka 2014 hadi sasa, ingawa vilivyosajiliwa ni 700.
Mwisho
Comments
Post a Comment