NA HAJI NASSOR, PEMBA@@@@
‘KABLA ya kuongezeka kwa wavuvi na wachuuzi hapa soko la samaki Mkoani, nilikuwa mauzo yangu ya uji na maandazi ni shilingi 35,000 kwa siku, lakini sasa yamezidi mara mbili,’’anasema Aisha Hemed Khalifa.
Anasema, kwanza hakujua nini sababu ya kuongezeka kwa wavuvi na wachuuzi kwenye soko hilo, na alijikuta akiishiwa na biashara yake kabla ya saa 5:00 asubuhi, muda aliouzoea tokea zamani.
Kwa kwaida, alishazoea anapoanza biashara yake hiyo, humaliza kati ya saa 5:00 hadi 5:30, ingawa kuanzia mwezi Januari jana hali imebadilika.
Biashara yake hiyo aliyoianza miaka mitano sasa, anasema ilikuwa ni ya kusua sua, kutokana na kuwa na idadi ndogo ya wavuvi na wachuuzi (wateja) kwenye soko hilo.
Awali aliacha biashara ya duka la vyakula, na kujiingiza kwenye uuzaji wa uji na maandazi, soko la samaniki Mkoani Pemba, ili kuongeza pato lake.
Akiwa kwenye soko hilo, anasema biashara ilikuwa ya kudoro dora kiasi, ingawa pato lake lilikuwa tofauti, ikilinganishwa na biashara ya duka aliyokuwa nayo awali.
“Biashara hii ya uji na maandazi makavu kwangu, inalipa zaidi kuliko ile ya duka, maana kwanza hapa huwa naifanya kulingana na hali ya wavuvi na wachuuzi wanapokuja na sio kila wakati,’’anasema.
Mjasiriamali huyo aliyeachika miaka mitatu akiwa na watoto wanane (8) sasa akiwa anawahudumia, kwa kwaida ikifika saa 5:30 mchana huwa ameshamaliza biashara na kurudi nyumbani kuendelea na shughuli za kilimo.
SERA YA UCHUMI WA BULUU ULIVYOKUZA BIASHARA
Anasema, kuanzia mwezi Januari mwaka huu , sasa biashara yake imekuwa ikipanda siku hadi siku, akisema sera ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi, imeongeza idadi ya wavuvi na wachuuzi.
Anasema, sio wavuvi lakini hata vijana wameamua kufunga susu nyuma ya baiskeli, kuamua kuchuuza samaki, wakiamini kuwa sekta hiyo, sasa imepata mkombozi.
“Sina takwimu halisi lakini sasa wavuvi wapya ninaowajua mimi tu wanafika 20, sambamba na wawachuuzi 30 wapya waliongezeka, wakifurahia uchumi wa buluu,’’anasema.
Mjasiriamali huyo anasema ahadi ya Dk. Mwinyi ya kuitumia bahari kwa ajili ya kukuza pato la wananchi, kwake limeanza hata kabla ya kuvua rasilimali yoyote baharini.
Sera ya uchumi wa buluu anaifahamu kuwa, ni kuinua pato la serikali na hata la mtu mmoja mmoja, likisababishwa na uwepo wa bahari.
“Hata mimi sasa kuongeza pato langu la biashara kutoka kilo nne za zamani za unga wa mtama hadi sasa kufikia kilo sita sio jambo dogo,’’anaeleza.
Anasema hata kwenye maandazi, alikuwa kabla ya ujio wa sera ya uchumi wa buluu, akitumia unga wa nganu kilo mbili kwa ajili ya maandazi, lakini sas analazimika kutumia kilo nne.
“Mimi amaandazi yangu sio kwa ajili ya wateja wa uji tu, lakini hata wengine wanaokuja sokoni, lakini ukweli kuanzia mwezi Januari hadi Machi mwaka huu mauzo yangu yamepaa,’’anasema.
Huyu ni mmoja tu, lakini wapo wapishi wa uji na maandazi na wengine chai wanaouza kwenye madiko (masoko ya samaki) 22 walielezea kupata manufaa.
Halima Omar Haji, aliyepo soko la samaki Wete, anasema sera ya uchumi wa buluu, kwake umeshapanda chati, baada ya kujikuta akiongeza mauzo ya biashara zake.
“Mimi nauza maandazi ya mafuta, ya kupambia na chai lakini sasa nimeshahama mauzo ya shilingi 35,000 kwa siku na sasa nahesabu kwenye shilingi 50,000 kwa siku,’’anasema.
Nilipotaka kujua sababu za kuongeza mauzo, akajikuwa kuwa anachokishuhudia ni kuongeza kwa wavuvi hata wale ambao walishatangaaza kustaafu.
Sababu nyingine ni kuongeza kwa wachuuzi vijana, jambo ambalo wapo waliopata mshangao na walipoulizwa wamesema wamejenga matumaini kwa ahadi ya rais Dk. Mwinyi.
Hata mjasiriamali wa juisi, vileja, uji na chai aliyepo bandari ya Tumbe wilaya ya Micheweni Tumu Haidari, anasema ameanza biashara hiyo kwa miaka sita sasa.
Kwa miaka yote hiyo, anasema hakuwahi kushuhudia mauzo ya shilingi 65, 000 kwa siku, ambapo hayo ameyashuhudia ndani ya mwaka huu.
“Mimi ilikuwa biadhaa zangu zote nikishauza najikuta nna shilingi 40,000 tu, lakini sasa dhana ya chumi wa buluu na kuongeza kwa wavuvi na wachuuzi, kwangu ni neema,’’anasema.
Hivyo hivyo, nae muuza mihogo ya kukaanga, chai na samaki soko la samaki Micheweni, Mwache Haji Hija anasema kwa sikukuu hii ijayo, anahakika ya watoto wake kuwanunua nguo kwa uhakika.
Anasema awali alikuwa akiifanya biashara hiyo kama eneo lake la mapunziko tu, lakini anataka kutanua mafya kwa sasa na kujenga kibanda cha kudumu.
“Lazima nimpongeze rais wangu wa Zanzibar Dk. Hussein Ali Mwinyi, kwa kuamua kuinua kipato chetu kwa mtazamo wa bahari, hii kwangu ndio yajayo ni neema tupu,’’anasema.
Mjasiriamali huyo anasema, kwa vile amekuwa akiingia kwa zamu na mwenzake sokoni hapo, ndio hasa pato lake huwa la uhakika zaidi.
Anasema, kwa miaka iliyopita kwa vile hakukua na idadi kubwa ya wachuuzi wala wavuvi na walaji, inaweza ikapita siku tatu bila ya kushuka sokoni.
“Sera ya uchumi wa buluu na ukweli wa vitendo wa rais Dk. Mwinyi, naamini ndio iliyoongeza idadi ya wanunuzi wa samaki, wachuuzi na wavuvi na wao baada ya kuuza na kununua hujipatia kinywaji kibandani kwangu,’’anasema.
MALENGO YA WAJASIRIAMALI HAO NI YEPI?
Wanasema, sasa wanajipanga kwenda Idara ya Uwezeshaji, ili kuomba mikopo, kwa ajili ya kuendeleza biashara zao na ikiwezekana waajiri wenzao.
Halima Juma Khamis wa aliyepo sokoni Wesha Chake chake, anasema aliwahi kuchukua mkopo wa shilingi 200,000 mwaka 2013, ingawa ulimshinda kurejesha.
“Kwa hatua ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi kuimarisha uvuvi na wengine wanaotegemea rasilimali za bahari, sasa najiamini kuchukua mkopo hadi shilingi 500,000,’’anasema.
Nae Halima Omar Haji, anaiomba Idara ya Uwezeshaji kupunguza masharti, ili sasa na wao waingie kwenye sekta ya mikopo, kama walivyo wenzao,’’anasema
WAVUVI NA WACHUUZI WANASEMAJE
Msaidizi mkuu wa diko la Wesha Chake chake Mohamed Haji, anakiri kuongezeka kwa wavuvi kwenye diko hilo, ambao baadhi yao walishataka kustaafu.
Anaema, sio wavuvi tu lakini hata kuna ongezeko kubwa la wachuuzi, na wengi wao kutoka nje ya mji wa Chakechake.
“Hivi sasa wapo wachuzui wanaotumia gari ndogo aina ya ‘carry’ kutoka miji ya Mkoani na Wete wakifuata samaki hapa, hivyo hawa wengi wao baada ya kufika hupata vinywaji,’’anafafanua.
Kwake anasema, dhana ya uchumi wa buluu ambao hata ndani ya soko hilo matunda yake yameshaonekana, ndio miongoni mwa sababu za kuongezeka kwao.
Mkuu wa wilaya ya Mkoani Khatib Juma Mjaja, anasema azma ya serikali, sasa kuwa ndio mkombozi wa kuinua kipato cha taifa na hata mtu mmoja mmoja.
Mvuvi Haji Kheir Haji wa Mwambe mwenye ngalawa jina la ‘joka pevu’ anakiri kuwa, ongezeko la wavuvi ni manufaa kwa wafanyabiashara hasa walioko kwenye madiko.
Pandu Mjanaheri Ussi ambae ni mchuuzi mpya, anasema kilichomvuta kufanya shughuli hiyo, ni kutokana na kauli ya rais wa sasa wa Zanzibar, wa kuiimarisha sekta ya uvuvi.
“Ni kweli, nimeona kundi la vijana wenzagu wakiwa wamefunga masusu na kuchuuza, lakini tukifika kwenye diko, kwanza hupata kifungua mdogo kwa wale mama zetu,’’anasema.
AHADI YA DK. MWINYI KUINUA PATO KWA UCHUMI W A BULUU
Wakati akinadi sera za chama chake cha Mapinduzi CCM kwenye kampeni, kuelekea chaguzi mkuu, aliwaahidi wananchi kuinua pato kupitia bahari.
Akisema kuwa, bado bahari ya Zanzibar haijaguswa kiuvuvi, na pindi akipata ridhaa, atakahakikisha anaongeza pato la taifa na la mtu mmoja mmoja kupitia shughuli zilizoko baharini.
Uchumi unaotokana na rasilimali za bahari kama vile samaki, chaza, majongoo na mwani (uchumi wa buluu) utaweza kuongeza pato la taifa.
Dk. Mwinyi aliwaambia wananchi wa Zanzibar kuwa, hali hiyo inaweza kuongeza makusanyo la mapato ya ndani kutoka shilingi bilioni 428. 511 kwa mwaka 2015 hadi kufikia shilingi bilioni 748.9
Lakini dhana ya uchumi wa buluu, ikitumika vilivyo inaweza kupunguza utegemezi wa bajeti na kufikia asilimia 5.7 na kuvuuka lengo lililoanishwa kwenye Ilani ya CCM ya mwaka 2020/2025, na kufikia asilimia 7 hapo mwakani.
Dk. Mwinyi anaamini kuwa, kwa vile uchumi wa buluu hauwalengi, wavuvi, wachuuzi, wakulima wa mwani, majongoo, wavuvi wa mishipi, nyavu na madema pekee, anaona hata wanaofanya shughuli za juu watanufaika.
Hapa, alilenga sekta binafasi ambapo serikali inaazimia kushuka kwa riba ya mikopo, kutoka wastani wa asilimia 18 ya mwaka 2015 hadi asilimia 14 ya mwaka 2020.
Jambo moja ambapo wavuvi na wengine wanaotegemea bahari wanatarajia kulipata kama alivyoahidi Dk. Mwinyi wakati wa kampeni, ni kukamilisha utayarishaji wa sera mpya ya uvuvi na kufanya mapitio ya sheria ya uvuvi nambari 7 ya mwaka 2010.
Kwenye Ilani hiyo ya CCM, ambayo imeahidi pia kuongeza uzalishaji wa samaki, aina ya Jodari katika bahari kuu na ufugaji maalum wa kutumia vizimba ‘cage farming’ kutoka tani 36,728 hadi tani 44, 450.
Kubwa zaidi, ambalo nalo litafanywa ni kujenga miundombinu kwa ajili ya kuimarisha utendaji wa kampuni ya uvuvi ya Zanzibar ‘ZAFICO’ ikiwemo vyumba baridi vya kuhifadhia samaki.
Hapa Mkurugenzi mkuu wa Shirika la Uvuvi Zanzibar ‘ZAFICO’ Zahoro Kassim, anasema alichokiahidi Dk. Mwinyi sio ndoto bali yanaukweli, na hasa kwa vile hata ununuzi wa boti za uvuvi kwa ajili ya bahari kuu zinakuja.
Matumaini pia kwa wananchi na hasa wavuvi na wachuuzi wa samaki ni pale, Dk. Mwinyi alipowaahidi wizara husika ya Uchumi wa Buluu, kuzalisha na kusambaaza vifaranga milioni 10 vya samaki, kaa na majongoo kila mwaka.
Haya sasa yakifanyika kwa pamoja, wale mama mtilie ambao wanaendesha biashara zao kando kando ya madiko na masoko ya samaki, wanaweza kuongeza pato lao mara dufu.
Mwisho
Comments
Post a Comment