NA HABIBA ZARALI, PEMBA@@@@
‘MWANZO wa kuanza mchezo huu, nilipata changamoto
kubwa na kuambiwa nacheza mchezo wa kiume, wa kihuni lakini sikuvunjika moyo’.
Hayo ni maneno ya kocha
wa mpira wa miguu timu ya Mkoani Qunes, Ramla Khamis Juma aliyenza kwa
kutandaza soka hapo awali.
Kocha Ramla aliyasema maneno hayo wakati akizungumza na
makala haya huko katika uwanja wa mpira wa miguu Mpikatango Mkoani kisiwani
Pemba, wanapofanyia mazoezi.
Akinisimulia sababu ya
kupenda michezo ni pale alipokuwa skuli ya msingi Ngwachani, akiwa darasa la
sita baada ya kuwaona wanafunzi wenzake wakishiriki michezo mbalimbali ikiwemo mpira
wa pete ‘netball’.
Wakati akiingia skuli ya
Sekondari Uweleni, alikuwa anachezea timu ya netball ya wilaya, ndipo hapo hapo
alipoanza kujifunza kucheza mpira wa miguu.
“Kwa vile mchezo wa mpira
wa miguu kwa wanawake, ilikuwa haujazoeleka wilaya ya Mkoani na ni ajabu, ambapo
wengi walishangaa na kunikataza lakini haikuwa lolote mimi niliendelea kujifunza,”alisema.
Baadae alikwenda kujiunga
na Chuo kikuu cha Zanzibar ‘SUZA’ kisiwani Unguja, na baada ya kurudi Pemba
ndipo aliposhawishiwa na rafiki yake anaeitwa Maida, kwenda kujifunza mchezo wa
mpira wa miguu.
Na baada ya kumaliza kusoma
na kurudi Pemba mwaka 2012, akaanza mchakato wa kuanzisha timu ya mpira wa
miguu ya ‘Mkoani Queens’ mwaka 2014 na hadi leo inaendelea.
Akimtaja mwenzake ambae walibahatika
kuchaguliwa kufudishwa mchezo huo ni Maida Mohamed Salum ,ambapo wote
wanaendelea na mpira huo.
Alianza kufundisha vijana
mchezo huo wakiwa katika mazingira magumu, jamii haielewi wanachokifanya maneno
na kejeli nyingi ingawa hawakuvunjika
moyo.
“Lakini kwa hatuwa ya
mwanzo tulifundisha tukiwa hatuna vifaa vyovyote, ilikuwa ni duni mipira hatuna
ni ya kubaka baka tu hakuna wadhamini,”anasema.
Pamoja na mazingira
magumu ya mchezo huo, lakini waliendelea na kufundisha vijana kucheza wakiwa na
kocha Mohamed Juma.
Anazidi kusimulia wakati
wakiendelea na mchezo huo, jamii iliyowazuguka mwanzo haikukubali mchezo huo, na
hapo ndipo, maneno kadhaa yaliweza kutoka kwa wanajamii kuwa mchezo wa mpira wa
miguu.
‘’Kwa wanawake ni haramu, ukafiri, uhuni,
umalaya, ingawa maneno hayo hayakufua dafu kwake,’’anafafanua.
‘Ingawa hakuna aliyekatisha njiani, kwani nilikuwa
nashajihisha kwelikweli na mimi sikuvunjika moyo niliendelea mwanzo mwisho,
hadi vijana wakaweza kucheza,”anaeleza.
Kumbe kila siku
zinaposonga, wanachukuwa ushauri kwa Shirikisho la mpira wa Miguu Zanzibar ‘ZFF’
na siku zikisonga wanacheza kirafiki na
timu ya Mkoa wa Kaskazini Wete.
Tumu nyingine ni za
vijana chini ya umri wa miaka 17 za watoto wanaume ni kwa sababu hakuna timu ya
wanawake kwa karibu.
Wakati akiwa katika ligi timu
yake, iliwahi kushindana na timu ya New generation, ambayo ilikuwa ni tishio
kwa Zanzibar, ingawa walifungwa mabao 3, lakini nao walijipinda na kuwaingia
kwa goli moja la kufutia machozi.
“Watu walitushangaa na
kutupongeza kwa sababu timu ya New generation, ilikuwa inatambana haifungwi
lakini sisi tulipata goli moja,”alisema.
Anasema kwa vile mchezo huo ulikuwa dani ya moyo na damu yake, hakuridhika na kufungwa, ndipo alipoamuwa kushajihisha, ili waweze kupata ushindi.
‘Nakumbuka kila
tunapocheza na timu yoyote ile tutapambana,
lakini tufunge na tukishindwa sawa lakini si kwa bila,”alisema.
Anasema ni jambo linalomuhuzunisha
sana kuona timu hiyo inasuasua kwa namna moja ama nyingine na ndio maana,
hutowa fedha zake mkononi kuhakikisha timu inasonga mbele.
Akitaja mafanikio anasema
ni pamoja na kutambua kwa jamii ya Mkoani kuwa timu ya mpira wa miguu, ipo na
kuwa na uelewa japo si kwa kiasi kikubwa.
Anasema jingine ni kutowa
vijana nje ya Zanzibar hadi baadhi ya mikoa ya Tanzania Bara, kwa ajili ya kushiriki
na kucheza.
Mafanikio mengine ni
vijana wengi kuhudhuria mafunzo ya mpira wa miguu kupitia ZFF, kujiunga na timu
ya taifa ya Zanzibar kwenda Kenya, kupata ajira kwenye serikali kupitia mchezo
huo.
Kocha Ramla aliwahi
kupata mafunzo mbalimbali ya ukocha, kupitia ZFF ambapo walikuja wakufunzi
kutoka ndani na nje ya Zanzibar, kujifunza uwalimu wa soka kwa watoto wa kike.
‘Nilitamani niwe kama
kocha Hatma Mwalim Khamis wa timu ya taifa ya Zanzibar, kutokana na utendaji
wake mzuri, ufuatiliaji na ‘usmati’,’’anasema.
Anataja changamoto na
kusema kwenye mchezo huo hakuna wafadhili, na hulazimika kutembeza bakuli, uhaba
wa timu za mpira wa miguu za wanawake hasa kisiwani Pemba.
Uhaba wa mashindano ya
mara kwa mara na mabonanza, umasikini wa familia za Watoto, jambo ambalo liliifanya timu hiyo kutoshiriki ligi
kuu ya soka la wanawake Zanzibar mwaka 2024/2025.
Nafasi alizowahi kukamata
ni mjumbe wa Wilaya kamati tendaji Wilaya ZFF, kamati tendaji Mkoa, kamati
tendaji taifa soka la wanawake Zanzibar.
Jambo ambalo hatoweza
kulisahau, ni kule kuuanzisha mpira huo wilaya ya Mkoani, kuifunga timu New generation
amabayo ni maarufu na mabingwa kwa mchezo huo Zanzibar.
Endapo atapata msaada (support)
matarajio yake ni kuupeleka mchezo huo katika baadhi ya skuli wilaya ya Mkoani,
ili waweze kuuendeleza.
Akitowa ushauri wake,
anaiomba serikali kuongeza mkazo zaidi kuwaendeleza vijana wa kike hasa Pemba,
kwani vipo vipaji vigi tokea mwaka 2014 ilipoanzishwa Mkoani Queens, bado
hakuna timu nyengine wilayani humo.
Kocha Ramla alizaliwa
mwaka 1986, ni mtoto wa tatu kwa mama Zainab na kwa baba ni mtoto wa tisa na hadi
sasa mtoto wake wa kiume, Ibrahim miaka 13 ndie ambae anaonekana kumrithi.
Ibrahim yuko katika timu
ya matayarisho ya watoto chini yamiaka 16, ambapo anamuona na hamu na hamasa kubwa ya kushiriki mazoezi bila
kuhimizwa.
Akimzungumzia Kocha Ramla, mmoja wa wanawake
wanaosiamia mpira wa miguu Zanzibar Hatma Mwalim Khamis, anasema ni mwanamke
anaejitolea kwa hali na mali, kuhakikisha mpira wa miguu unasonga mbele.
Kocha Ramla kakulia
kimichezo humlazimu kutowa chake cha mfukoni, alimradi mchezo uendelee kwani ni
mmoja anaeonesha kuukubali mchezo huo
‘Sifa ya Ramla hakuwa mtu
wa kukata tamaa na aliweza kujitia moyom na kuukubali mchezo wa mpira wa miguu,
tokea akiwa mwanafunzi hadi leo tayari ni kocha wa kuaminika,’’anamsifia.
Mohamed Juma ni mmoja wa
walimu walioanza kufundisha pamoja na kocha Ramla, anasema ingawa walianza
pamoja kufundisha ilipoanzishwa timu hiyo lakini Ramla, hakusita hadi leo ni kocha
bora.
Anasema wanajivunia kuwa
katika wilaya ya Mkoani, wamekuwa wanasifikana kupitia mchezo huo chini ya
kocha Ramla, kwani anaongoza timu hiyo, na kuhudhuria vikao kadhaa.
Anasema ni vyema makocha
wakatambulika na wapatiwe nafasi za kusoma ukocha, hasa kwa wale wenye malengo
ya kuendeleza mchezo.
Mmoja wa wachezaji wa
timu hiyo Hamida Juma Amani anasema miongoni mwa sifa za kocha Ramla ni mstaarabu
mwenye kueleweka wakati anapofundisha.
“Kocha wetu hatuachi
mkono tunapokuwa na shida huwa nasi bega kwa bega na ndio maana tunamkubali,”anasema.
Afisa mradi wa kukuza usawa wa kijinsia na ujumuishi kwenye michezo
unaofadhiliwa na shirika la maendeleo la
kimataifa la Ujerumani Khairat Haji,
anasema kila mtu anayo haki ya kushiriki katika michezo na hakuna sababu
ya wanawake kubakia nyuma.
Ndio maana anasema kupitia mradi huo TAMWA Zanzibar itahakikisha usawa
wa kijinsia, unapatikana katika michezo ya aina mbali mbali.
Pamoja na kuwa wanawake wako
nyuma katika ushiriki wa michezo, aliwataka wasirudi nyuma na washiriki kwa
hali ya kuridhisha.
Ili vijana wa kike waweze
kukua kimichezo ni vyema Shirikisho la mpira wa miguu Zanzibar ‘ZFF’ lianzishe
mashindano mbalimbali pamoja na mabonanza, kwani bila ya kuutangaza mchezo huo
hautokwenda mbele.
MWISHO...
Comments
Post a Comment