HABIBA ZARALI, PEMBA@@@@
MICHEZO
ni sehemu muhimu katika utamaduni wa kila jamii ya binadamu kote duniani.
Michezo iko ya aina nyingi, ambayo jamii ya
makabila tofauti hushiriki kutokana na utamaduni walionao na kwa madhumuni
tofauti.
Pamoja na michezo kuwa na faida lukuki, ikiwemo
kupata ajira, kujenga afya ya mwili na
akili, kuburudisha, kuelimisha, kutambulisha, kujenga ukakamavu, kuonesha
vipaji na kujenga urafiki, lakini bado jamii iko nyuma kwa hilo.
Ingawa hakuna tamko linaloonesha kuwa watoto wa
kike hawapaswi kushiriki katika michezo, ingawa bado hali haijaridhisha.
Sera ya maendeleo ya michezo 2018 imeonesha hali ya
sasa tangu kuanzishwa kwa wizara yenye dhamana ya michezo na baraza la michezo
la taifa, maendeleo katika maeneo mbalimbali ya michezo yamepatikana.
Sera hiyo haikumbaguwa mtu yoyote kushiriki michezo
na kuonesha kuwa, michezo mingi mipya imaenzishwa na kuleta mafanikio makubwa
kulingana na vipaji na uwezo walionao wananchi.
Ambapo nayo Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984,
kifungu cha 11 kimeeleza kuwa binadamu wote ni sawa, na kifungu cha 12
kikaweka usawa ndani ya sheria.
Katika makala haya, inaangazia chanagamoto za
watoto wa kike kuwa na ushiriki mdogo katika michezo.
WADAU
WA MICHEZO
Mwenyekiti wa Shirikisho la mpira wa miguu ZFF Mkoa
wa Kusini Pemba Nassor Hakim Haji, anasema kutokuwa na mazingira mazuri
yaliyoandaliwa kuhusu watoto wa kike, kujishirikisha na michezo inachangia
watoto hao kuwa na ushiriki mdogo.
Anasema mchanganyiko kati ya wanaume na wanawake
katika viwanja vya michezo, ni jambo moja linalowarejesha nyuma huku
ikizingatiwa wazazi bado mwamko wao ni mdogo.
Anasema kwa upande wa jamii, bado haijawa tayari
kuona ushiriki wa wanawake katika masuala ya michezo kwani wao ndio chanzo cha
kupiga kelele na kuweka dhana potofu kwa michezo ni uhuni.
“Mimi katika wanafunzi wangu nilionao tayari watatu
wamefanikiwa kupata ajira kupitia michezo, wawili wako Jeshi la Polisi na mmoja
mwanajeshi na si hao tu wako wengi,’’anasimulia.
Kocha wa mpira wa kikapu ‘basketball’ wilaya ya
Mkoani Mohamed Salim Khamis (Gabs) anasema,
kutokuwa na uwanja maalum kwa watoto wa kike hasa katika hatuwa za awali
kunapelekea ushiriki kuwa mdogo.
Anasema uwanja mmoja ambao wanacheza wanaume ndio
huohuo wanaochezea wanawake huku ukiwa sehemu ya uwazi ni jambo jingine, linalowapelekea
watoto wa kike kujiskia aibu na kukataa kujishiriki michezo.
Jambo jengine ni uhaba wa walimu kwa upande wa basketball
ambapo kwa upande wa wilaya ya Mkoani, hakuna timu pinzani ambayo watashindana kirafiki
ama kujipima hadi wafunge safari wilaya ya Chake chake au Wete.
Changamoto nyingine anasema ni ,muono finyu wa
jamii kuhusu watoto wa kike, kushiriki michezo huku wakiwa na dhana ya kuwa ni
uhuni.
“Na kuhusu mchezo wetu huu vifaa vyake ni ghali
sana ikiwemo viatu , mipira, jezi, koni ‘Cones’ haya yote kwa watoto wa kike
kwao ni sehemu ya changanamoto,’’anafafanua.
Kocha wa mpira wa miguu wanawake Ramla Juma Khamis anasema
wazazi wengi wako nyuma, kuelewa faida zilizomo katika michezo na kupelekea
kuwakataza watoto wao kushiriki.
Anasema pamoja na kuwa dini haikukataza wanawake
kushiriki michezo, ingawa bado baadhi ya viongozi wa dini wanakuwa na tafsiri tofauti,
ambayo inawarejesha nyuma watoto wa kike kushiriki michezo.
‘Huekwa mihadhara katika mitaa na kuzungumzia jinsi
ya watoto wa kike wanavyojishirikisha na michezo kwa kisingizio cha kuwa watakuwa
wahuni,’’alisema.
Mwalimu wa michezo skuli ya Sekondari Uweleni Abdull
Ali Abdalla, anasema jamii inahitaji kupewa elimu ya kutosha kuhusiana na
umuhimu wa michezo kwa watoto wa kike.
Alisema kuna tamaduni zilizowagubika wana jamii na
kuona kuwa watoto wa kiume ndio wanaostahiki kujishughulisha na michezo pekee,
kuliko wa kike linapaswa kufahamishwa.
WATOTO
WA KIKE WANASEMAJE
Maimuna Fatawi Khamis, mwanafunzi wa kidato cha nne
skuli ya sekondari Uweleni anasema baada ya kujishirikisha na michezo
alikatazwa na wazazi wake kwa kisingizio cha uhuni, na jamii iliyomzunguka ili mbeza
na kumuambia michezo haina faida.
Nassra Ali Sheha ni mwanafunzi kutoka skuli ya
sekondari ya Uweleni, anasema baada ya kuanza kujishirikisha na michezo
alikatazwa na wazazi wake, kwa kisingizio cha kuwa michezo ni uhuni.
Kwa vile alikuwa tayari keshavutika na michezo
baada ya kuwaona wenzake wanacheza, aliamuwa kuendelea na sasa anamekuwa
tofauti hata katika ufahamu wake wa masomo yake.
“Naamini kama michezo inajenga akili, kwani nimekuwa
na utofauti mkubwa kabla sijaingia katika michezo na sasa, nimeweza kujuwana na
watu wengi tunapokwenda kushindana,”anasimulia.
Fatma Massoud Kombo anasema awali wa kujulikana
kuwa anashiriki katika michezo, aliambiwa hatoweza kufaulu kwani akili yake
ataitowa kwenye kushughulikia masomo, jambo ambalo aliliona sio kweli.
Anacheza mpira wa pete ‘netball’ akiwa skuli na
hata mchezo wa nage anapokuwa nyumbani, lakini hali yake ya masomo yake haijaathirika.
WAZAZI
WANASEMAJE
Salma Suleiman wa Mkoani anasema, ili watoto wa
kike waweze kuwa na ushiriki sawa na wanaume, lazima wawekewe mazingira sawa
kuanzia viwanja na hata mavazi.
Anasema wapo watoto wa kike wanaoshiriki michezoya
aina mbalimbali lakini utamaduni haukubaliani iwapo watachanganyika pamoja na
wanaume.
“Sisi wazazi hatuoni furaha kwa watoto wetu wakike
kuona wanafanya jambo, lenye viashiria vibaya na tunasema lakini hebu serikali
ifanye kuwaona watoto hawa wa kike, katika mazingira ya mazuri kwenye
michezo”,anashauri.
Saumu Omar wa Kiwani, anasema mtoto wake wa kike
aliacha kushiriki michezo akiwa skuli, baada ya kufanyiwa istizai na watoto wa
kiume, lakini kama kungelikuwa na kiwanja maalum kwa ajili yao, engendelea.
Anasema bado jamii inahitaji kuelimishwa kuhusiana
na umuhimu wa mtoto wa kike kujishirikisha na michezo, ili nao waweze kupata
faida.
“Tunaona kama michezo inasaidia ana katika upatikanaji
wa ajira, lakini jamii ilotuzungumka bado haina mwamko huo mtoto wako
anapoingia kwenyemichezo, siku chache unaekewa vikao jambo ambalo siosahihi,’’anaeleza.
Kombo Shaibu wa Mwambe anasema tokea enzi ya wazazi haikuonekana kama ipo
haja kwa mtoto wa kike kujishirikisha na michezo .
Anasema ni jambo la busara kwa serikali ama taasisi
zinazojishughulisha na michezo kuelimisha jamii kuhusiana na umuhimu wa watoto
wa kike, kushiriki michezo mbalimbali.
VIONGOZI
WA DINI WANASEMAJE
Sheikh Said Ahmad kutoka ofisi ya Mufti, anasema
dini ya kiislam haijambagua mtu kushiriki kwenye michezo, kutokana na jinsia
yake.
“Dini imeweka wazi watu wafanye mazoezi, ili kuweka
mwili sawa na kuisitiza kufuata taratibu ikiwemo kuvaa nguo za stara,”anasisitiza.
Mchungaji Samwel Elias Maganga wa kanisa la
Makangale anasema hata dini ya kikiristo, nayo haijamkataza mwanamke
kujishirikisha na michezo, ila maadili yazingatiwe.
Michezo ni vitu vinawafanya watu wasahau
chanagamoto zilizowapata watuna kuwakusanya pamoja na hilo linatokea tokea mtu
anapokuwa mtoto kwani viungo vyake hukuwa kupitia michezo.
“Michezo ni ya watu wote na hata ulimwengu kutoka
nchi moja na nyingine, unaunganika kupitia michezo,”alisema.
TAMWA
ZANZIBAR
‘’Ni kweli watoto wa kike wako nyuma katika ushiriki wa
michezo na kuwataka waandishi wa habari kuhakikisha wanatumia kalamu zao, kulisemea
ili kuondoa mawazo finyu kwa jamii, kuwa watoto wa kiume ndo wanaofaa kushiriki michezo pekee,’’anasisitiza.
Lengo la mradi huo unaofadhiliwa na shirika la
maendeleo la kimataifa la Ujerumani, ambao unatekelezwa na jumuiya ya
wanasheria wanawake Zanzibar ‘ZAFELA’, kituo cha majadiliano kwa vijana ‘CYD’ ni
kuhakikisha wanawake wanashiriki katika michezo kwa hali ya kuridhisha.
‘Kwa vile kila mtu anayo haki ya kushiriki katika
michezo, kwa nini wanawake wabakie nyuma na tutahakikisha usawa wa kijinsia
unapatikana katika michezo,’’anaeleza.
WIZARA
HUSIKA INASEMAJE
Mkuu wa
divisheni ya michezo na utamaduni
Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Pemba Mzee Ali Abdalla, anasema kupitia skuli,
watoto wote wanashirikishwa na hawabaguliwi.
Anasema
watoto wanapokuwa masomoni, wanasomeshwa sawa somo la sanaa na ubunifu, kwa
nadharia na vitendo kwa pamoja kati ya wanawake na wanaume.
“Tunaposhiriki katika mashindano ya elimu bila
malipo tunakuwa nazo timuza wanaume na wanawake, bila yaubaguzi na fursa zote
zinazotokea basi wanapewa sawa,’’anaeleza.
MWISHO
Comments
Post a Comment