HABIBA ZARALI, PEMBA@@@@
Ushiriki mdogo kwenye michezo kwa watoto wa kike, Kisiwani
Pemba ni sababu moja inayopelekea wanawake kuwa nyuma katika sekta hiyo.
Wakizungumza na mwandishi wa habari hizi kwa nyakati tofauti
kisiwani humo, wananchi hao walisema bado wanawake ushiriki wao ni mdogo,
katika michezo ya aina mbali mbali, hivyo jitihada zinahitajika kuhakikisha nao
wanashiriki kama walivyo vijana wa kiume.
Said Ali Said wa Mkoani, alisema watoto wa kike huishia
maskulini kushiriki michezo na wanapomaliza hawajiendelezi na wala hakuna mtu
wala taasisi ya kuviendeleza vipaji hivyo.
"Wapo watoto wa kike wanakuwa wazuri tu katika michezo
mbalimbali, kama mpira wa miguu, kikapu, mpira wa Pete na mengine, lakini
cha kusikitisha ni kuwa baada ya kumaliza skuli hawajiendelezi tena,"alisema.
Massoud Ali Mohamed wa Chake Chake, alisema kutokana na
changamoto ya mavazi, kunasababisha kudumaza kwa michezo kwa watoto wa
kike.
Alifahamisha kuwa, kama hakutozingatiwa mavazi ya stara kwa
watoto wa kike, kunaweza kukaendelea kuwa na mwitikio mdogo wa kushiriki watoto
wa kike kwa kutoruhusiwa na wazazi wao.
"Mimi nahisi kuwe na sheria hasa watoto wa kike ya
kuvaa vazi ka heshima ‘Islamic hijab’ wanapokuwa katika michezo ili waweze na
stara,"alishauri.
Salma Suleiman wa Mkoani alisema, ili watoto wa kike waweze
kuwa sawa na wanaume, kwenye suala la kushiriki michezo ni lazima Serikali
itowe elimu, iwawezeshe kifedha na kuvaa nguo za maadili.
Katibu wa chama cha mpira wa miguu Wilaya ya Chake chake
Jongo Juma Jongo, alisema kwa sasa ushiriki wa wanawake katika mchezo huo upo,
ingawa ni mdogo.
Alifahamisha kuwa, mwitikio mdogo wa watoto wenyewe, jamii
inavyochukulia mpira wa miguu ni uhuni kwa watoto wa kike inawafanya
wasiendelee mbele kwenye michezo.
Akigusia kwa upande wa mavazi, Jongo alisema isiwe kikwazo
kwa wanawake wani wanaruhusiwa kuvaa nguo za stara ikiwemo treki, vilemba na
kuwataka wazazi wawaruhusu watoto wa kike, kushiriki michezo ili waweze
kutimiza ndoto zao.
"Kuwazuwia watoto wa kike kutoshiriki michezo si haki kwa
sababu, dunia ya sasa imebadilika na kupiga hatuwa
Kwani, kuna nafasi za kusoma nje ya nchi kupitia michezo na
hatimaye kupata ajira",alisema.
Idara ya michezo na utamadini wizara ya elimu na
mafunzo ya elimu, ilisema wizara inayo mikakati mbali mbali ya kuhakikisha
wanawake wanakuwa sawa, katika ushiriki wa michezo.
Akiitaja mikakati hiyo ni pamoja na kuanzisha somo la sanaa
na ubunifu, michipuo wa michezo pamoja na kuanzisha elimu ya juu vyuoni.
Kaimu mratib wa michezo wizara ya Habari, Utamadini na
Michezo Khamis Hamad Juma, alisema katika kuhakikisha vijana wa kike
wanashihiriki kikamilifu katika michezo inaweka miundo mbinu ya kujenga viwanja
vinne vitakavyozingatia mahitaji yote kisiwani Pemba
Alieleza kuwa, viwanja hivyo, ambavyo kila kimoja kitakuwa
na viwanja vya kuchezea michezo minne tofauti, ambapo ujenzi unaanza mwanzoni
mwa mwezi wa sita mwaka huu 2024.
Mwalimu kutoka skuli ya Sekondari Uweleni Khamis Mohamed
Ussi, alithibitisha kuwa wanafunzi wanaoshiriki katika michezo, ndio
wanavofanya vizuri katika masomo yao.
Hivyo aliwaomba wazazi, kuwaruhusu watoto wao kushiriki
katika michezo mbali mbali, ili waweze kupata fursa zinazotokea kupitia sekta
ya michezo.
Hakuna hata sheria moja, kati ya zile 17 zinazoongoza mpira
wa miguu, zinazomzuia mtoto wa kike, kushiriki mchezo, kwani kanuni ya kwanza
ni uwepo wa uwanja ya pili ni mpira, idadi ya wachezaji, vifaa vya michezo, mwamuzi
pamoja na shera ya 17 ya pigo la kona.
Mwisho
Comments
Post a Comment