MASHEHA kisiwani
Pemba, wameonya kutojishusisha na uuzaji wa ardhi, kwani sheria zinazosimamia
ardhi, hazitambui nafasi yao, katika zoezi la awali la uuzaji ama ununuaji.
Ushauri huo umetolewa
leo Mei 25, 2024, na Hakimu wa mahkama ya ardhi ya mkoa wa kusini Pemba,
Abdalla Yahya Shamuuni, wakati akijibu maswali ya wananchi wa shehia ya Kukuu
Kangani, wilaya ya Mkoani, kwenye mkutano wa wazi, uliondaliwa na Idara ya
Katiba na Msaada wa kisheria Zanzibar, kupitia mradi wa upatikanaji haki,
unaofadhiliwa na UN-WOMEN kupitia Umoja wa Ulaya ‘EU’.
Alisema, sheria ya
Ardhi, zinaanza kutambua kazi ya sheha wa eneo husika, lililouzwa ardhi, wakati
wa uhaulishaji, ambapo hapo yatahitajika maoni yake, pamoja na ya Mkuu wa
wilaya.
Alieleza kuwa, ni
kosa kwa sheha, kujihusisha na mauziano ya ardhi, ingawa hutakiwa kuwepo
kama shahidi, ili kuwa na taarifa sahihi zinazoendelea katika eneo lake.
‘’Sheha hahusiki moja kwa moja
wakati wa mauziano ya aradhi, bali sheria zimemtaja wakati wa zoezi la
uhaulishaji, kutoka kwa mnunuzi kwenda kwa mnunuaji,’’alieleza.
Katika hatua
nyingine, Hakimu huyo wa mahkama ya ardhi mkoa wa kusini Pemba, Abdalla Yahya
Shamuuni, alisema migogoro mingi ya ardhi, inachangiwa na wananchi walio wengi
kuwa na uwelewa mdogo wa sheria.
‘’Umiliki wa aradhi
sheria unatambua njia tano pakee, ikiwemo ya kununua, kurithi, kupewa zawadi,
kuvunja pori na kupewa na waziri husika, ambapo kisha suala la kuisajili ni la lazima,’’alifafanua.
Akizungumzia suala
la mirathi, ameitaka jamii kuharakisha kufanikisha zoezi hilo, kwa kuitumia
Kamisheni ya Wakfu na Mali ya Amana Zanzibar, ili kupata vielelezo rasmi kutoka
serikalini.
‘’Suala la kurithi hata
masheikh wetu wa mtaani wanafaa, lakini kisha hawakupi nyaraka za urithi na
umiliki, kama unazopewa Kamisheni ya Wakfu, hivyo niwashauri mkimbilie huko,’’alishauri.
Mapema Afisa Sheria
kutoka Idara ya Katiba na Msaada wa Kisheria Zanzibar Salma Suleiman Abdulla,
aliwataka wananchi wa shehia ya Kukuu, kuitumia Idara yao, wanapokuwa na
changamoto za kisheria.
Alieleza kuwa,
Idara hiyo imeanzishwa na serikali, kwa lengo la kuwasaidia wananchi wasiokuwa
na uwezo, hivyo ni wajibu wao kuitumia Idara hiyo.
‘’Lakini mkiona
sisi tuko mbali, basi waoneni wasaidizi wa sheria, ambao wapo katika ngazi ya
shehia, kwani ni wajibu wao kutoa elimu, ushauri na msaada wa kisheria bila ya
malipo,’’alifafanua.
Mkurugenzi wa
Jumuiya ya wasaidizi wa sheria wilaya ya Mkoani ‘MDIPAO’ Nassor Hakim Haji, aliwashauri
wananchi kuwatumia wasaidizi wa sheria, ili kufanya sulhu nje ya mahkama, kwa
kesi za madai.
‘’Ofisi yetu iko
Mkoani, lakini hata hapa shehia ya Kukuu, yupo msaidizi wa sheria, mtumieni na
changamoto ya kisheria ikiwa kubwa, tutakuja kwa ajili ya kutafuta sulhu,’’alieleza.
Afisa sheria wa
Wakala wa Usajili wa Matukio ya Kijamii Zanzibar, Faki Haji Faki, aliwataka
wazazi na walezi, mara wanapopata mtoto kuhakikisha ndani ya siku 42, wanaanza
taratibu za kumtafutia cheti cha kuzaliwa.
Baadhi ya wananchi
wa shehia ya Kukuu, wamesema njia ya kuwafikia shehiani kwao, kuwapa elimu ya
sheria ni nzuri, na kuiomba Idara hiyo, kufanya kila wakati utakaporuhusu.
Hata hivyo, baadhi
ya wananchi hao akiwemo Bakar Khalfan Ali, yeye alitaka kujua, ikiwa kundi la
watu linaweza kumiki ardhi yao, baada ya kufuata utaratibu.
Nae mwananchi
Kassim Mohamed Faki, alitaka kujua kwanini wanawake, nao hawatiwi hatiani,
kwenye tendo la ubakaji na badala yake adhabu hiyo hutiwa mwanamme pekee.
Kwa upande wake,
mwananchi Abdalla Mohamed Salim, alipendekeza kuwa, ni vyema somo la sheria,
likaanzia ngazi elimu ya msingi, kutokana na umuhimu wake katika nchi.
Awali kulitanguliwa na utoaji elimu kwa njia ya igizo, lililotoa ujumbe wa kuharakisha urithi, kuandikiana wakati wa ujenzi na umuhimu wa kujua sheria
Mwisho
Comments
Post a Comment