IMEANDIKWA NA
KHAULAT SULEIMAN
WAANDISHI wa habari
nchini wameshauriwa kutumia kalamu zao vizuri, ili kuleta mabadiliko ya
kimaendeleo katika jamii.
Akizungumza katika mahafali ya pili kwa waandishi wa habari
vijana (YMF) yaliyofanyika katika Ukumbi wa Bima Mpirani Mjini Unguja, Mjumbe
kutoka TAMWA Zanzibar Shifaa Said Hassan aliwataka waandishi hao kujitahidi
katika kazi zao ili kuwaletea mafanikio yao na jamii kwa ujumla.
Alisema kuwa, wandishi wa habari ni chachu ya kuleta maendeleo
katika jamii, hivyo ipo haja ya kutumia kalamu zao vizuri kwa kuandika
habari za kuibua changamoto ili zipatiwe ufumbuzi kwa kwa maslahi ya jamii na
Taifa.
"Kuna waandishi wanajitahidi sana kuandika habari na
tunaona zinaleta mabadiko chanya kwa jamii, hivyo tuendelee kujitolea katika
kuisaidia jamii yetu ili tufanikiwe," alisema.
Aidha aliwataka waandishi hao vijana kuwahamasisha wengine pindi
zinapotokea fursa za mafunzo washiriki kikamilifu, ili kupta elimu na
kukuza maendeleo yao na hiyo itasaidia kuleta mabadiliko.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa TAMWA Zanzibar Mzuri Ali Issa
alisisitiza kufata miongozo na kanuni ya uwandishi wa habari, ili kuwainua wale
wasioweza na kuwafanya wakasikika.
"Tunatoa mafunzo mbali mbali kwa waandishi vijana na hata
wale wasio vijana, lengo letu ni kuona jamii inapata mabadiliko ya kimaendeleo
katika nyanja mbali mbali, hivyo zitumieni fursa hizi," alisema Mkurugenzi
huyo.
Alisema kuwa, wamekuwa wakiwatumia waandishi katika kazi zao,
ambapo hufanikiwa kwa asilimia kubwa, hivyo wanatambua mchango wa wanahabari
katika kuleta mabadiliko.
Nao wahariri waliohudhuria mahafali hayo, wamewataka wandishi
hao kutumia lugha fasaha ambayo itawafanya wasomaji wao au waskilizaji
kuelewa vizuri maudhui yaliyokusudiwa.
"Pia tunaiomba TAMWA wanapowapa mafunzo waandishi
wahakikishe wanawaita na wahariri ili wanapokuja kwetu isiwe tunakinzana, hii
itatusaidia kujua habari mnazozitaka," walisema wahariri hao.
Waliwapongeza waandishi hao kwa kazi nzuri walizofanya katika kuihamasisha jamii katika suala zima la mwanamke kuwa kiongozi, ambapo kwa asilimia kubwa jamii imeindokana na dhana potofu ya kwamba mwanamke hawezi kuwa kiongozi.
MWISHO.
Comments
Post a Comment