NA MWANDISHI MAALUM,
DODOMA@@@@
VYOMBO vya habari vina dhima
na jukumu la kusaidia katika kuimarisha demokrasia hususan katika kuelimisha
umma masuala ya uchaguzi ili waweze kushiriki kwa ukamilifu katika uchaguzi na
kuimarisha demokrasia ya ushiriki wa wananchi kwa ukamilifu.
Akizungumza katika kongamano
la wadau wa habari na uchaguzi Tanzania lillilofanyika leo April 30, 2024, katika ukumbi wa hoteli ya Dodoma Waziri mkuu
mstaafu Jaji Joseph Warioba alisema kuwa nguvu ya vyombo vya habari havina budi
kutumika katika mchakato wa uchaguzi tokea kujiandikisha hadi kupiga kura ili
kuimarisha shughuli hizo za uchaguzi.
Jaji warioba alisema kuwa
bado vyombo vya habari havikufanya kazi zake kwa ukamilifu katika chaguzi zilizopita hivyo kuna haja ya
kubadilika katika vyombo vyetu vya habari ili viweze kufanya kazi zake kwa
ufanisi.
“Vyombo vya habari vinatoa
habari sio elimu na vinajikita zaidi katika matokeo na havifanyi utafiti”,
alifafanua.
Jaji Warioba alisema kuwa enzi
zile vyombo vya habari hususan katika maoni ya mhariri vilijikita katika
utafiti wa kina na kufanya uchambuzi ambao ulisaidia kuizindua serikali na
kuweka sera ambazo zinasaidia kataika kujenga na kuimarisha haki na demokrasia
katika masuala mbali mbali.
Alisisitiza haja ya vyama
vya siasa kuwa na mawanda mapana katika kuimarisha demokrasia hapa nchini
hususan katika hatua za awali za uteuzi wa wagombea.
“Vyama vya siasa viimarishe
demokrasia katika uteuzi wa wagombea tuwapelekee wananchi wagombea
wanaokubalika kwa wananchi”, Aliongeza
Alitoa wito maalum kwa
vyombo vya habari kusaidia kupunguza changamoto za uchaguzi katika hatua zote
tokea kujiandikisha, kupiga kura pamoja na kuchagua wagombea ambao wamekubalika
kwa wananchi.
Vurugu katika uchaguzi
zinatokea kutokana na kwamba wananchi hawakuridhika na mchakato wa
uchaguzi na sauti na kero zao hawana
pahala za kuzitoa hivyo ni muhimu kulitazama kwa kina suala hili la uchaguzi
katika hatua zote ili usawa, haki na uwajibikaji uweze kupatikana katika hatua
zote.
Katibu Mtendaji wa Baraza la
habari Tanzania Ernest Sungura alisema kuwa Baraza la habari Tanzania
limejikita katika kukuza maadili na weledi kwa waandishi wa habari ili waweze
kutumia kalamu zao katika kujenga misingi ya haki , uwazi na uwajibikaji katika
hatua zote za uchaguzi.
Alisema kuwa nguvu ya vyombo
vya habari havina budi kutumika kujenga jamii iliyo bora na imara ili lengo la
vyombo hivyo katika kuelimisha umma liweze kutekelezwa.
“Kuongeza elimu kwa wapiga
kura itakayowasaidia kufanya maamuzi makini na sahihi katika sanduku la kupiga
kura”, alifafanua.
Alisisitiza kuwa kwa kipindi
vyombo vya habari Tanzania havikuwa na mshikamano na maandalizi ya pamoja na
kuimarisha habari za uchaguzi katika hatua zote ili kuimarisha elimu kwa wapiga
kura lakini pia wananchi waweze kupata taarifa ambazo zitawasaidia katika
kufanya uamuzi wakati wa kupiga kura.
“Vyombo vya Habari vya
Tanzania huwa havina maandalizi ya Pamoja ya namna ya kuandika na kutangaza
Habari za uchaguzi katika kila hatua ya mchakato wa uchaguzi kuanzia uboreshaji
wa daftari la wapiga kura, kujiandikisha kwa wapiga kura, uteuzi wa wagombea,
elimu kwa mpiga kura, kampeni hadi siku ya kupiga kura”.Alifafanua
Hivyo alisema kuwa Baraza la
habari linakusudia Kuviandaa vyombo vya Habari mapema kwa kuandaa Mpango Kazi
wa Kitaifa unaolenga kuvisaidia vyombo vya Habari kufanya kazi ya kihabari ya
kutoa taarifa sahihi kwa wakati sahihi kufichua uovu na kuwajibisha na kuibua
masuala ili yajadiliwe.
Mwakilishi wa ubalozi wa
Marekani Kalisha Holmes, alisema kuwa vyombo vya habari ni muhimili wa nne na
hivyo vina wajibu wa kuelimisha umma katika masuala ya uchaguzi ili waweze
kufanya maamuzi sahihi.
Katika kipindi hiki ni
wakati muafaka wananchi kupata habari zilizo sahihi ili waweze kufuatilia kwa
karibu hatua zote za kuimarisha demokrasia pamoja na kutumia vyombo vya habari kama
njia muhimu ya kuimarisha demokrasia hususan katika kuelekea uchaguzi.
“Umuhimu wa uhuru wa vyombo
vya habari unahitajika. Vyombo huru na vinavyojitegemea ni nguzo muhimu katika
kukuza na kuimarisha demokrasia”, aliongeza.
Wakichangia katika kongamano
hilo Usia Nkhoma Mtaalam wa mawasiliano kutoka UNICEF alisema kuwa Vyombo vya
habari viwe na agenda ili viakisi maoni na matakwa ya wananchi ili tuwe na
vyombo vya habari makini, tunalo jukumu kubwa la namna gani tunaweza kujenga vyombo
vya habari imara ambao tulazimishe
wanasiasa waweke masuala ambayo yanayokidhi mahitaji ya vizazi vyetu.
Edda Sanga mwandishi mkongwe
alisema wanawake hawana budi kupewa fursa ya kuchagua na kuchaguliwa kwa mujibu
wa matakwa yao na kamwe wasitumike kama ngazi katika uchaguzi. Sauti za walioko pembezoni pia ziweze kupewa
nafasi katika uchaguzi na kero zao ziibuliwe na kujadiliwa na kupatiwa
ufumbuzi.
Pili Mtambilike mtaalamu wa
sekta ya habari amesema vyombo vya habari vina dhima kubwa ya kuondoa sumu iliyojengeka
katika uchaguzi na hivyo kuongeza elimu
ya wapiga kura katika vyombo vya habari. Vyombo vya habari viwe mstari wa mbele
katika kusaidia kueneza suala hilo la elimu kwa mpiga kura.
Aliongeza umuhimu wa makundi
yote ya pembezoni kuwemo katika hatua zote za uchaguzi hususan makundi ya
walemavu ili kuimarisha ushiriki wa watu wote katika masuala ya uchaguzi.
Mchakato wa kuwapata wagombea katika makundi hayo uwe wa uwazi na uzingatie
haki na usawa kwa wote.
Kongamano hilo la siku moja
ambalo limefanyika leo katika ukumbi wa Dodoma Hotel likiwa na kauli mbiu ya
uandishi wa habari za uchaguzi kwa weledi na kujenga usawa, haki na uwajibikaji
limeandaliwa na Baraza la habari Tanzania na limewashirikisha wadau wa habari,
wanasiasa, waandishi wa habari pamoja na asasi za kiraia.
Hii ni mara ya kwanza kwa
kongamano la aina hiyo kufanyika hapa nchini likiwa na lengo la Kujadiliana na
kuweka mikakati ya pamoja kuongeza UWAZI, HAKI na UWAJIBIKAJI tunapoelekea
katika uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka 2024 na uchaguzi mkuu mwaka 2025.
Kongamano hilo limefadhiliwa na Ubalozi wa Marekani na IFES (The international
and Foundation for Electoral system)
mwisho
Comments
Post a Comment