IMEANDIKWA
NA ZUHURA JUMA, PEMBA
MADAKTARI
na wauguzi wa kituo cha Afya shehia ya Pandani wameshauriwa kuendelea kutoa
huduma bora za kimatibabu ili jamii iwe na afya njema.
Akizungumza mara baada ya kukabidhi taa katika kituo hicho,
Mkaguzi wa shehia hiyo Inspekta wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Kaskazini Pemba
Khalfan Ali Ussi alisema, licha ya changamoto wanazokumbana nazo lakini hawana
budi kujitolea katika kazi zao.
Alisema kuwa, ili jamii ipate maendeleo inahitaji watu wake
wawe na afya njema kwa ajili ya kufanyakazi vizuri, hivyo ni vyema kwa
madaktari kuendelea kutoa huduma bora kwa mgonjwa anaefika kituoni hapo kwa
matibabu.
"Kwa kweli madaktari wanafanya kazi kubwa, hivyo
tuendelee kujitolea kwa moyo safi ili jamii ipate huduma bora na afya
njema," alisema Mkaguzi huyo.
Inspekta Khalfan aliwataka wananchi kutoa ushirikiano kwa
wafanyakazi wa kituo hicho kuhakikisha kinadumu kwa muda mrefu, kwani wao ndio
walengwa wa kupatiwa huduma.
"Lengo la ziara yetu ni kukagua maeneo mbali mbali na
kujua hali halisi ya kiusalama katika taasisi za Serikali na jamii kwa ujumla,
kujua changamoto zinazowakabili na namna ya kuweza kuzipatia ufumbuzi,"
alisema.
Aidha Mkaguzi huyo aliwataka wananchi pamoja na wafanyakazi
wa kituo hicho kuzitunza taa hizo ili zitumike kwa muda mrefu.
Kwa upande wake Mkuu wa kituo hicho Dk. Muhsin Ali Shehe kwa
niaba ya wafanyakazi wenzake alishukuru kupatiwa msaada huo wa taa na kusema
kuwa ilikuwa ni changamoto ya muda mrefu iliyokuwa ikiwakabili ambayo kwa sasa
imeshatatuliwa.
"Tumefarajika sana kupata msaada huu na pia
tunamshukuru Mkaguzi huyu kwa kutimiza ahadi yake kwa sababu kipindi cha nyuma
alikuja akaona hii changamoto na leo ameitatua," alieleza daktari huyo.
Nao wananchi walisema kuwa, taa hizo ni msaada mkubwa kwao
kwani eneo hilo limekuwa giza kwa muda mrefu kiasi ambacho watoto walikuwa
wanaogopa ingawa sasa watapata kuwatuma.
"Eneo hili kwa usiku ilikuwa sio zuri kupita kwa
kuhofia usalama wetu na watoto wetu lakini sasa tunaweza kupita muda wowote,
tumefurahi sana," walisema wananchi hao.
Sheha wa Pandani Khamis Rashid Ali alisema kuwa, anapata
faraja kuona kwamba Mkaguzi huyo anafanya kazi za kusikiliza kero na
kuhakikisha shehia anazozisimamia zinakuwa katika hali ya usalama.
MWISHO.
Comments
Post a Comment