NA ZUHURA JUMA, PEMBA@@@@
MWENYEKITI wa Bodi ya Jumuiya ya Utetezi wa Mazingira na Jinsia Pemba ‘PEGAO’ Alhajji-Amran Massoud Amran, amewashauri wahamasishaji jamii kudai haki zao za uongozi, demokrasia na siasa ‘Citizen bragged’ kisiwani Pemba, kuelekeza nguvu zao ngazi ya vyuo, ili kuwaibua wanawake wenye nia ya kugombea nafasi za uongozi.
Alisema, wanafunzi wanawake ambao wanajitayarisha kuja kuitumikia jamii, wako katika skuli za sekondari na vyuo vikuu, hivyo ni vyema kwa wahamasishaji hao, sasa kuhamia katika eneo hilo kufanya uhamasishaji.
Mwenyekiti huyo wa bodi, aliyasema hayo jana, alipokuwa akizungumza na mwandishi wa habari hizi juu nafasi ya wahamasishaji jamii kutoka TAMWA, namna ya kuwaandaa wanawake kuwa viongozi katika nafasi mbali mbali.
Alisema, wanawake walioko ngazi ya elimu ya sekondari na vyuo vikuu, ndio tegemeo kubwa kwa jamii, hivyo ikiwa watawezeshwa mapema, kuingia katika nafasi za uongozi, itakuwa rahisi kwao, baada ya kumaliza masomo.
‘’Kwanza nipongeze kazi yenu kubwa ya kuzipitia shehia mbali mbali hata zile za visiwani, kwa lengo la kuihamasishaji jamii, kudai haki zao za uongozi, lakini msisahau kupitia na vyuoni,’’alipendekeza.
Katika hatua nyingine, Mwenyekiti huyo wa Bodi ya ‘PEGAO’ Alahajji-Amran Massoud Amran, alisema bado elimu zaidi inahitajika kwa jamii, ili imuamini mwanamke kwenye safu ya uongozi.
Hata hivyo alisema, juhudi zinazofanywa kwa pamoja kati ya PEGAO, ZAFELA na TAMWA zinafaa kuungwa mkono, kwani inakuja kuchapuza ukuaji wa demokrasia na uwazi nchini.
Mapema Mkurugenzi wa ‘PEGAO’ Hafidh Abdi Said, aliwasisitiza wahamasishaji hao, wanapoibua changamoto kwa jamii, wahakikishe wanaifuatilia hadi mwisho.
‘’Kwa mfano, wapo wanawake hata vitambulisho vya mzanzibari mmegundua hawana, au hawana huduma za kijamii kama maji safi na salama, sasa hapa lazima mzitafutilie ufumbuzi wake, ili wawaamini,’’alishauri.
Hata hivyo Mkurugenzi huyo, aliwakumbusha wahamasishaji hao, kuwamakini wanapoandika ripoti zao, ili zianishe changamoto, suluhisho na mkakati wa baadae.
Kwa upande wake Mratibu wa mradi wa kuihamasisha jamii kudai haki zao za kisiasa, uongozi na demokrasia ‘SWIL’ kutoka ‘PEGAO’ Dina Juma, alisema ni vyema kwa taasisi na mashirika, kuendelea kushirikiana na asasi za kiraia.
‘’Sisi asasi na zile taasisi za serikali, sote tunatengeneza jamii moja, sasa tunawapowafikia, kuwasilisha changamoto zao, waone kama tumewasaidia kazi,’’alieleza.
Mhamasishaji jamii kutoka Wete Salim Hamad Sharif, aliuomba uongozi wa ‘PEGAO’ kupanga timu maalum, kwa ajili ya kwenda kwa wananchi wa kisiwa cha Fundo, kutoa elimu kwa upana.
‘’Wananchi wa kisiwa cha Fundo baadhi yao hawajaelewa kwa upana, umuhimu wa elimu kwa watoto wao, ndio maana mtoto anaweza kutolewa darasani aende habarini, bila mzazi kujali jambo hilo,’’alieleza.
Nae Mohamed Maalim, alisema kama inakubalika popote mtu anapofanyia kazi kufikisha elimu, sasa atahakikisha kila eneo anafika, ili kuelezea haki jamii katika uongozi, siasa na demokrasia.
Wakiwasilisha ripoti zao hivi karibuni, viongozi wa wahamasishaji jamii kutoka wilaya nne za Pemba, walisema wamekuwa wakiibua changamoto zinazoikabili jamii, ingawa upatikanaji wa suluhisho ndio kikwazo.
Mradi wa kuihamasisha jamii kudai haki zao za uongozi, demokrasia na siasa ‘SWIL’ unatekelezwa na Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania, ‘TAMWA’ –Zanzibar, Jumuiya ya Wanasheria Wanawake Zanzibar ‘ZAFELA’ na Jumuiya ya Utetezi wa Mazingira na Jinsia Pemba ‘PEGAO’ kwa ufadhili wa Ubalozi wa Norway.
Mwisho wa utekelezaji wa mradi huo, huo wa ‘SWIL’ unatarajiwa wanawake wasiopungua 6,000 iwe wamesha wezeshwa kudai haki zao.
Mradi huo uliozinduliwa Novemba, 2020, na ukitarajiwa kutia nanga mwaka 2024, watu 100 wakiwemo wanawake na wanaume, iwe tayari wameshajengewa uwezo, ili nao sasa kuwafikia wanawake 400, ambao nao wenyewe wanatarajiwa kuwafikia wanawake hao 6,000.
Idadi hiyo wanawake 6,000 watakaofikiwa, ni sawa na PEGAO, TAMWA na ZAFELA kuwafikia wanawake 1,200 kwa kila mkoa mmoja, kati ya mitano ya Unguja na Pemba.
Ambapo hapo ni sawa na wanawake 546 kutoka kila wilaya moja, kati ya wilaya 11, ambapo Pemba zipo nne na Unguja saba.
Zanzibar yenye majimbo 50 ya uchaguzi, mradi huu wa ‘SWIL’ utawafikia wastani wa wanawake 120, kutoka kila jimbo moja la uchaguzi, sawa na kufikiwa wanawake 55 kwa kila wadi moja, kati wadi 110 za Unguja na Pemba.
Mwisho
Comments
Post a Comment