WANACHAMA
wa ushirika wa ‘twaomba kheir’ wa wanawake wa kijiji cha Chanjamjawiri
shehia ya Shungi wilaya ya Chake chake Pemba, wamekopeshana mikopo minane, yenye
thamani ya shilingi 800,000 katika kipindi cha mwaka jana pekee.
Wapo wanachama
sita, waliokopa shilingi 100,000 kila mmoja na wawili kukopa shilingi 50,000, kwa
ajili ya kutimiza malengo yao mbali mbali, ikiwemo kukamilishia ujenzi wa
nyumba zao.
Ushirika huo
wenye wanachama 15, unasema kima hicho cha fedha walichokopeshana sio kidogo
kwa wao, kutokana na hali zao za umaskini wa kipato ulivyokuwa hapo awali.
Akizungumza na
mwandishi wa habari hizi, Mashika wa ushirika huo Sharifa Mohamed Khamis,
alisema fedha hizo zilitokana na michango yao ya awali ya kila mwanachama, kujiwekea
hisa ya shilingi 8,000 kwa mwezi, sawa na shilingi 2,000 kila mwisho wa wiki.
Alisema kuwa,
utaratibu huo ulianza tokea mwezi Septemba mwaka 2022, ambapo kwa mwezi,
wanauwezo wa kukusanya shilingi 120,000 wastani wa shilingi milioni 1,440,000
kwa mwaka.
‘’Fedha hizi
ndio ambazo wapo waliokopa hadi shilingi 100,000 na wingine kufanikisha
matibabu, kuendeleza ujenzi wa nyumba zao, harusi pamoja na vifaa vya masomo
kwa watoto,’’alisema.
Mshika fedha
huyo alieleza kuwa, kwa hali zao za maisha zilivyo, wamepiga hatua kubwa ya maendeleo,
kutoka utegemezi wa kipato usio na uhakika hadi sasa kujiamini kukopa kima chochote
kwa ajili ya kutatua changamoto.
Katibu wa
ushirika huo Mkali Juma Ali alisema, baada ya kuona mafanikio, kisha walianza na
mtaji wa kununua sabuni ya unga na kukopeshana, na kwa mara ya kwanza, walitumia
shilingi 38,000 na kujiingizia faida ya shilingi 8,800.
‘’Tulifanya
hivyo kwa mara saba na tukajikuta tumenunua sabuni ya unga ya shilingi 266,000
na kujipatia faida ya shilingi 61,600 kwa mtindo wa kuuzia paketi ya kilo moja kwa
shilingi 1,700,’’alifafanua.
Mwenyekiti wa
ushirika huo Bimkubwa Othman Khamis, alisema baada ya kuona wanapata faida, waliamua
kujinunulia sukari kilo 200 kwa mara nne tofauti, kwa gharama ya shilingi 300,000
kwa wakati huo.
‘’Baada ya
kuuziana kwa vipindi vinne tofauti, kwa bei ya kilo moja shilingi 2,000 tulijipatia
shilingi 400,000 na kujiingizia faida ya shilingi 100,000 na hapo tulikuza
mtaji wetu,’’alifafanua.
Alifafanua kuwa,
kwa sasa baada ya kuimarika kwa hisa, wamekijikuta kuwa na miradi miwili ya
uuzaji wa sabuni na usukari huku uwekaji wa hisa na ukopaji ukiendelea.
Mwanachama wa
ushirika huo Asma Said Abdalla, alikiri kuwa, kwa sasa maisha yake ya kipato
yako tofauti kabla na baada ya kuingia kwenye ushirika huo.
‘’Hivi
karibuni niliwahi kukopa shilingi 150,000 na kumalizia ujenzi wa vyumba vitatu,
jambo ambalo kama sio ushirika huu, nisingekuwa na uwezo huo,’’alieleza.
Nae mwanachama
wa ushirika Zulekha Nassor Hilali, alisema alikopa shilingi 150,000 kwa ajili ya
matibabu, jambo ambalo lilimsaidia kutatua changamoto hiyo.
‘’Kwa hakika
mafanikio yetu makubwa ni kujiamini sasa na hatuna hofu kwa jambo la shilingi 100,000
hadi shilingi 500,000 kwangu sio kikwazo nikitokezewa na shida,’’alifafanua.
Moja ya changamoto
wanazokumbana nazo kwa sasa, ni pamoja na masharti magumu ya upatikanaji mikopo
jambo ambalo, linawarejesha nyuma kimaendeleo.
Sheha wa
shehia ya Shungi Hamad Ramadhan Soud, alisema ushirika huo umekuwa mfano wa
kuigwa ndani ya shehia yake, kutokana na kufanya vizuri, kuanzia uwekaji hisa
hadi biashara.
‘’Naendelea
kufautilia namna ambayo wanaweza kupata mikopo yenye masharti nafuu, ili kuona
wanaendeleza biadhara zao na kuongeza mtaji wao hapo badae.
Ushirika huo
wa ‘twaomba kheir’ wa kijiji cha Chanjamjawiri shehia ya Shungi, unao wanachama
15 wote wanawake, ulianza mwaka 2022, unaendesha uwekaji hisa, uuzaji wa sabuni
na sukari na wanampango wa kununua nguo hapo baade.
Mwisho
Comments
Post a Comment