NA HAJI NASSOR, PEMBA@@@@
JESHI la Polisi mkoa wa kaskazini Pemba,
limesema haliko tayari kuona maisha ya wavuvi yako hatarini, kwa kule kutofuatilia
taarifa za wataalamu wa mamlaka ya hali ya hewa nchini.
Hayo yameelezwa bandari ya Tanda Tumbi, kwa
nyakati tofauti na Mkaguzi wa shehia ya Mjananza
kutoka Jeshi la Polisi mkoa wa kaskazini Pemba, Inspekta Khalfan Ali Ussi, wakati
akizungumza na wavuvi hao, kwenye bandari za shehia hiyo, alipofanya ziara
maalum.
Alisema, Jeshi la Polisi linawajibu wa
kuwakumbusha wavuvi hao, kufuatilia kila siku taarifa za utabiri wa hali ya
hewa, kwani Jeshi halipendi kuona maisha yao yako hatarini.
Alieleza, kuwa, wavuvi ni moja ya kundi lenye thamani
kubwa katika jamii, hasa la kukuza pato la taifa, na ndio maana Jeshi la Polisi,
likaamua kukutana nao, ili kuwakumbusha jambo hilo.
Aidha Inspekta huyo alifahamisha kuwa, hasa
kwa kipindi hichi cha kuvuma upepo wenye kasi ya ajabu, ambao unauwezo mkubwa, ni
vyema wavuvi wakawa makini.
‘’Jeshi la Polisi limeamua kuwafuata bandarini,
ili kuwapa tahadhari ya upepo unaoendelea katika baadhi ya maeneo, kwamba umakini
unahitajika mno, na sio twende kimazoea kama zamani,’’alifafanua.
Katika hatua nyingine, Mkaguzi huyo wa shehia
ya Mjananza kutoka Jeshi la Polisi mkoa wa kaskazini Pemba, Inspekta Khalfan
Ali Ussi, aliwashauri wavuvi hao, kuweka mawasiliano ya uhakika kati yao na
walioko majumbani.
‘’Kwanza anzisheni utaratibu wa kutoa taarifa
mnapokwenda baharini kwa watu wenu wa karibu, lakini jingine ni kutoa nambari
zenu za simu, ili kila wakati mnawasiliana na walioko nchi kavu,’’alishauri.
Hata hivyo, aliwataka wavuvi hao kuwa walinzi na
kisha kutoa taarifa watakapoona kunafanyika baishara ya magendo, kwani wapo
baadhi ya wananchi, huzitumia vibaya bandari hizo.
Nao wavuvi hao walimpongeza Mkaguzi huyo, kwa
kufika na kuwakumbusha jambo hilo muhimu, katika maisha yao ya kutafuta riziki
baharini.
Walisema, utaratibu huo ni vyema ukawa
endelevu, katika bandari nyingine, ili taarifa hizo ziwafikie wavuvi na
wananchi mbali mbali kwa upana wake.
Aidha wavuvi hao, walimpongeza kwa ahadi
aliyoitoa, ya kununulia simu, kwa ajili ya kuwa na mawasiliano ya uhakika, kati
yao na familia zao.
Hii ni zaiara ya saba ya kuyatembelea makundi
mbali mbali ya kijamii, kufanywa na Mkaguzi wa shehia ya Mjananza kutoka Jeshi
la Polisi mkoa wa kaskazini Pemba, Inspekta Khalfan Ali Ussi, kwa lengo la
kuongeza uwajibikaji na uwazi.
Mwisho
Comments
Post a Comment