NA HAJI NASSOR, PEMBA@@@@
LEO Mei 7, mwaka 2024, Idara ya Katiba
na Msaada wa Kisheria Zanzibar ofisi ya Pemba, imekutana na wadau wake mbali
mbali wakiwemo watoa msaada wa kisheria na wasaidizi wa sheria, ili kupanga
mikakati ya kuelekea, wiki ya msaada wa kisheria hapa Zanzibar.
Kwenye kikao hicho kilichofanyika Gombani Chake chake, na
kuongozwa na Afisa Mdhamini, Ofisi ya Rais, Katiba, Sheria,
Utumishi na Utawala Bora Pemba, Halima Khamis Ali, kwanza kilipokea ripoti
ya wiki ya msaada ya mwaka 2023, iliyotolewa na Mkuu wa Divisheni ya Katiba na
Msaada wa Kisheria Pemba, Bakar Omar Ali.
Ambae kwenye ripoti hiyo, alielezea mafanikio yaliopatikana
ikiwa ni pamoja na kuwafikia wananchi waliokuwa wakihitaji msaada wa kisheria
katika makaazi yao.
Alisema jingine ni waendesha boda boda kutoa malalamiko
yao, juu ya madai ya kunyanyaswa na askari wa usalama barabarani pamoja na
faini kubwa wanazopigwa kwa makosa madogo.
Mkuu huyo wa Divisheni, alieleza kuwa jingine ni
kuwakutanisha watoa msaada wa kisheria na wasaidizi wa sheria kuelezea
changamoto wanazokumbana nazo wakati wanapokuwa katika shughuli mbali mbali.
‘Lakini pia katika wiki ya mwaka jana ya utoaji wa msaada
wa kisheria, wapo wasaidizi wa sheria mbali mbali, pamoja na waandishi wa
habari walionekana kufanyakazi vizuri na kupata tunzo,’’alifafanua.
Akizungumzia kuhusu wiki ya msaada ya mwaka huu, alisema walipanga
kuvitembelea vyuo vya mafunzo pamoja na kukutana na wanananchi waliomo kwenye mpango
wa kaya maskini.
Alieleza kuwa, shughuli hiyo haitofanywa tu na Idara ya
Katiba na Msaada wa kisheria, bali kila jumuia ya wasaidizi wa sheria na
taasisi nyingine, zinazojishughulisha na utoaji wa elimu ya sheria zitatakiwa
kufanya shughuli yoyote.
Akifungua mkurtano huo, Afisa Mdhamini, Ofisi ya Rais,
Katiba, Sheria, Utumishi na Utawala Bora Pemba, Halima Khamis Ali, alisema ni
vyema kila taasisi, ikajipangia itafanya nini katika wiki ya msaada wa kisheria
mara tu, itakapoanza mwezi ujao.
Alieleza kuwa, Idara ya Katiba na Msaada wa Kisheria, itaanza
kupokea mpango kazi wa kila taasisi, iwe ni mahakama, ofisi ya mwanasheria mkuu
na hata jumuiya za wasaidizi wa sheria, ili kuona wanawafikia wananchi.
Alieleza kuwa, bado kuna changamoto kadhaa zilizomo ndani
ya jamii, ambazo zinahitajika kupatikana ufumbuzi wa kisheria, na jamii
inawategemea wanasheria na wasaidizi hao wa sheria.
‘’Lakini sisi wizara, tunaridhishwa mno na kazi
mnazozifanya, lakini msibweteke muendelee kukaza buti, kwani jamii inaendelea
kukumbwa na majanga mbali mbali ya kisheria,’’alieleza.
Kwa upande wake mwakilishi wa Shirika la Msaada wa kisheria
na Haki za Binaadamu ‘ZALHO’ Said Rashid Hassan, alisema yapo makundi kama ya
wafanyakazi serikali, yanahitajika kufikiwa ili kuelezea changamoto zao.
Nae Mwanasheria kutoka baraza la mji wa Wete Hafidhi Sadra
Hassan, aliiomba Idara hiyo kwa mwaka wa fedha ujao wa fedha, kupanga bajeti
maalum ya shughuli hiyo, ili kuwatia moyo watendaji.
Hata hivyo Mkurugenzi wa Jumuiya ya Wasaidizi wa sheria
wilaya ya Chake chake ‘CHAPO’ Nassor Bilali Ali, alipendekeza kuwa, kinachofanyika
kisiwa kimoja na chingine kufanyike, ili kuweka usawa.
Hii itakuwa ni mara ya tano kufanyka kwa wiki ya msaada wa
kisheria Zanzibar, kuanzia mwaka 2020, ambapo kwa mwaka huu, inatarajiwa
kuzinduliwa Juni 24, na kuadhimishwa Juni 29 kisiwani Unguja.
Mwisho
Comments
Post a Comment