NA HAJI NASSOR, PEMBA@@@@
JAJI Dhamana wa Mahkama kuu Zanzibar kisiwani
Pemba, Salim Hassan Bakari, amewataka wahitimu ya mafunzo ya sheria, kuwa
mstari wa mbele, kuongoza mapambano dhidi ya rushwa katika taasisi za umma, ili
kwenda samba mba na kasi serikali ya awamu ya nane.
Jaji huyo aliyasema hayo leo Mei 10, 2024 , ukumbi wa Maktaba
Chake chake, wakati akiyafunga mafunzo ya sheria, yalioendeshwa na Kituo cha Mafunzo
na Utafiti Zanzibar ’ZLRC’ kilichopo chini ya Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka
Zanzibar, kwa upande wa Pemba.
Alisema, sasa wameshaongeza uwelewa wa
mapambano dhidi ya rushwa hasa baada ya kuisoma sheria husika zikiwemo za
manunuzi, ni vyema baada ya kuhitimu mafunzo hayo, wakawe mstari wa mbele
katika eneo hilo.
Alieleza kua, serikali ya awamu ya nane, nayo
imekuwa ikikemea kwa nguvu zote, juu ya utoaji na upokeaji wa rushwa, hivyo nao
wanaojibu huo, ikiwa ni sehemu ya kuimarisha utawala bora.
‘’Leo mmehitimu mafunzo ya kisheria, na bila
shaka suala la rushwa na athari zake mmeligusa, hivyo ni wajibu wenu sasa
mkaongoze mapambano hayo, kuanzia sehemu zenu za kazi hadi uraiani,’’alieleza.
Aidha Jaji huyo mkaazi, aliwataka wahitimu hao, sasa kufanya manunuzi kama sheria inavyotaka, ili kutimiza malengo ya kutungwa kwa sheria hiyo.
Alieleza kuwa, suala la manunuzi yasiozingatia
sheria, huigharimu serikali ikiwa ni pamoja na kupata hasara na kuwa sehemu ya
kichecheo cha rushwa kwa maafisa husika.
Katika hatua nyingine, Jaji huyo dhamana, alikipongeza
Kituo cha mafunzo na Utafiti Zanzibar, kilichopo chini ya Ofisi ya Mkurugenzi
wa Mashataka kwa kuendelea na mafunzo hadi kisiwani Pemba.
Mapema Mratibu wa mafunzo hayo Asya Mohamed Ibrahim,
alisema mafunzo hayo, ni sehemu ya kuchochea uwajibikaji, uwazi na kuwajengea
uweleza zaidi maafisa husika.
Alieleza kuwa, anaamini waliopatiwa mafunzo na
kama watayafanyiakazi kama walivyoaahidi, kunaweza kukajitokeza mabadiliko
makubwa katika sehemu zao za kazi, ikiwemo suala la manunuzi ya kisheria.
‘’Mimi niwaombe sana, wenzetu waliopata
mafunzo haya, kwamba lazima tuone kunamabadiliko kwenye taasisi zenu katika
maeneo ya manunuzi, matumizi na uhifadhi wa kumbu kumbu za serikali,’’alifafanua.
Kwa upande wake Kaimu Afisa dhamana wa ofisi
ya Mkurugenzi wa Mashataka Pemba Seif Mohamed Khamis, aliwakumbusha wahitimu
hao, kuangalia uwezekano wa kuongeza maarifa, katika kazi zao za kila siku.
Mafunzo hayo ya siku tano, yalioanza Mei 6, na
kufungwa Mei 10, yaliandaliwa na Kituo cha mafunzo na utafiti Zanzibar, na kuwashirikisha
washiriki 19, kutoka taasisi za umma, wakiwemo wahasibu, maafisa sheria na maafisa
manunuzi.
Miongoni mwa mada zilizofundishwa ni sheria za
manunuzi, sheria na miongozo ya kimataifa ya manunuzi, muhushiano kati ya
sheria za manunuzi na nyingine, uhusiano kati ya katiba na sheria, usimamizi wa
mikataba, zabuni na namna ya kuanzisha mchakato wa manunuzi.
Mwisho
Comments
Post a Comment