NA ZUHURA JUMA, PEMBA@@@@
WANANCHI wa shehia ya Mjananza Wilaya ya Wete Pemba wametakiwa kushirikiana pamoja kuhakikisha bandari zilizopo kwenye shehia yao hazitumiki vibaya.
Akizungumza na wananchi wakati wa ziara ya kukagua bandari bubu, Mkaguzi wa shehia hiyo Inspekta wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Kaskazini Pemba Khalfan Ali Ussi alisema, ni vyema bandari hizo zikatumika vizuri ili zisiwaingize kwenye makosa.
Alisema kuwa, siku zote bandari bubu hutumika vibaya kwa baadhi ya wananchi kusafirisha bidhaa kwa njia ya magendo, hivyo wananchi hao hawana budi kushirikiana pamoja kuhakikisha hawaruhusu kupitishwa bidhaa, kwani ni kosa kisheria.
"Suala la ulinzi na usalama wa bandari hizi sio la watu maalumu bali ni la wananchi wote, hivyo kila mmoja kwa nafasi yake ana wajibu wa kuzilinda bandari hizo ili zisitumike vibaya," alisema Khalfan.
Aidha aliwataka wanajamii hao kutoa taarifa kwa vyombo vya ulinzi pale tu watakapoona kuna bidhaa ama vitu vimeingizwa, kwani wanaofanya hivyo hawana nia njema ambapo adhma ya Serikali ni kukusanya mapato kwa ajili ya maendeleo ya wananchi.
"Bandari hizo hazijarasimiahwa hivyo wanapopitisha magendo inaikosesha Serikali mapato yake ambayo ndio yanayotumika kuwafikishia wanajamii huduma mbali mbali, kwa hiyo atakaejihusisha na huu uhujumu wa uchumi atchukuliwa hatua za kisheria kwani anadumaza maendeleo," alisema Inspekta huyo.
Kwa upande wa wananchi walisema kuwa, watashirikiana na kikundi cha ulinzi shirikishi kuhakikisha wanalinda na kufanya doria kwenye maneno yote ikiwemo ya bandari hizo, ili kuepuka kupitishwa bidhaa.
"Hatutoruhusu bandari hizi kupitishwa vitu kwa njia ya haramu, kwa sababu tunaibiwa ng'ombe kila siku na wanapitishwa hapa hapa, kwa kipindi hiki ng'ombe watano wameshaibiwa, hatutolifumbia macho hili," walisema wananchi hao.
Inspekta huyo akiongozana na Kamati ya ulinzi na usalama ya shehia hiyo walikagua bandari ya kwa Mbwana na bandari ya kwa kichupa, wakiwa na lengo la kuangalia shughuli zinazofanyika katika bandari hizo na namna ya kudhibiti kupitishwa kwa bidhaa za magendo.
MWISHO.
Comments
Post a Comment