NA MUZNAT KHAMIS, ZANZIBAR@@@@
TOFAUTI na
vilimo vyengine tulivyovizoea ambapo mkulima hulazimika kuchimba ardhi kwa kutumia
jembe ama zana nyengine, kuweka mbegu, mmea huanza kuota na tofauti na mwani
ambao hulimwa kwenye maji ya bahari.
Kilimo cha mwani kilianza mwishoni mwa mwaka miaka
ya 1980 hapa Zanzibar, ambapo wanaume wakiwa kwenye hatari za uvuvi wanawake
walizana kuingia kwenye kilimo hicho.
Hata hivyo, wanawake wengi hapo awali waliokuwa
wakijishughulisha na kilimo cha mwani ni wale waliokuwa kwenye mazingira magumu
wakiwemo wajane, ambao ndio waliokiona kilimo hicho kuwa mkombozi.
Umaarufu wa kilimo hicho zaidi unatokana na faida
zake kiuchumi na kwa sababu wakulima wengi wa zao hilo hapa Zanzibar ni
wanawake, ina maanisha kwamba zao hilo limekuwa moja ya nguzo ya kiuchumi
katika maisha ya akina mama Zanzibar.
Makala haya yanalenga kuangalia japo kwa ufupi sana
namna zao hilo linavyowanufaisha kiuchumi akina mama na namna zao hilo
lilivyobadilisha maisha yao.
MWANI
UNAVYOBADILISHA MAISHA YA WANAWAKE
Mariyam Mussa Haji mkaazi wa Fuoni Melitano, ambaye
ni muanzilishi wa kikundi cha ‘Muzne products’ chenye watu watatu, alisema
thamani ya zao la mwani imeongezeka ikilinganishwa na miaka iliyopita.
“Thamani ya zao la mwani imeongezeka kwa sababu
sehemu ya mwani inayozalishwa hapa Zanzibar inasarifiwa na kuzalisha bidhaa
mbalimbali”, alisema Mariyam.
Alisema tofauti na zamani mwali wote uliozalishwa
Zanzibar ulisafirishwa nje, hivi sasa hatua ya mwani kuzalishwa bidhaa hapa
nchini kumeongeza mnyororo wa tathamani kwa wajasirimali hasa wanawake.
Mariyam alisema tangu kukindi chao kuanza kuuza
bidhaa zitokanazo na mwani wamekuwa wakipata faida kubwa ikiwemo kujikwamua
kimaisha kutokana uuzaji wa bidhaa hizo.
Miongoni mwa bidhaa ambazo makala haya ilibatika
kuziona zilizozalishwa na kikundi cha ‘Muzne products’, kilichopo Fuoni Meli
tano ni pamoja na sabuni, mafuta, jam na unga wa lishe wa mwani.
“Kwa kiasi fulani fedha tunazopata zinatusaidia
kimaisha na kuepukana na ukali wa umasikini, wengine wamepata ajira za kudumu
kwa kuuza bidhaa”, alisema Mariyam.
Alisema kwa mwezi mmoja inategemea sana hali ya
soko, hata hivyo katika kipindi hicho ana uhakika wa kuingiza kuanzia shilingi
300,000 kwenda juu.
“Kwa kawaida biashara inaenda na msimu kwa wastani
tunaweza kuingiza 500,000, ikiwa biashara haiku vyema hatukosi shilingi
300,000”, alisema.
Mariyam alisema wanunuzi wa bidhaa za mwani mara
nyingi hutoka Tanzania bara pamoja na wazungu wanaotembelea katika maduka yao.
Kwa upande wake, Mwanaisha Makame ambaye ni mmoja
kati ya wachakataji wa zao la mwani kutoka Paje, alisema kazi hiyo imesaidia
kuinuka kiuchumi kwani amefanikiwa kuwasomesha watoto wake wawili katika ngazi
mbalimbali.
Safia Hashim mkaazi wa Muungoni wilaya ya Kusini
Unguja, alisema yeye ni mmoja kati ya wanawake waliofaidika na kilimo cha
mwani, ambapo amefikia hatua ya kumiliki nyumba.
Safia alisema alipata mafunzo ya miezi mitatu
kutoka kwa mtaalamu kutoka Indonesia ambayo yamemuwezesha kuwa na ujuzi wa
kusarifu zao la mwani.
"Kwa sasa naweza kutumia mwani kutengeneza
vitu mbalimbali kama vyakula, juisi, chachandu, pilipili, kachumbali, chipsi,
tambi, chauro, visheti, keki, pipi, jam ya matunda, sabuni, shampoo na mafuta
ya kupaka na nywele”, alisema Safia.
Joyce John Denis, ofisa uvuvi kitengo cha mwani
katika Idara ya Maendeleo ya Uvuvi na Mazao ya Baharini, alisema hatua ya
wajasirimali kuzalisha bidhaa mbalimbali kumelipa heshima zana zao hilo kwa
kiliongezea thamani.
Ofisa huyo alibainisha kuwa bidhaa zinazotokana na
zao la mwani zinasaidia wanawake wajasirimali kuongeza mapato na kuchochea bei
katika soko ikilinganishwa na mwani mbichi.
Aidha alisema bidhaa zitokanazo na mwani husaidia
kuimarisha afya ya jamii, kwani bidhaa zitokanazo na zao hilo zinapo sarifiwa
na kuwa chakula huasaidia mwili wa mwanadamu kupata virutubisho muhimu.
MWANI KUTOKA
MALIGHAFI HADI KUZALISHWA BIDHAA
Kilimo cha mwani kimewapatia ajira za kudumu
wanawake wengi katika sehemu za pwani za vijiji vya Zanzibar, ambapo baadhi ya
akina mama waliozungumza na gazeti hili wamesema pamoja na kwamba kilimo hicho
ni kigumu lakini kimebadilisha maisha yao.
Wanawake wengi wamejiajiri katika kilimo hicho,
ingawa wengi wao wanasema kuwa licha ya kazi kubwa kipato ni kidogo
wanachokipata, hata hivyo zipo faida wanazozipata.
Mwani umebadilisha mtazamo sio tu kiuchumi lakini
hata kitamaduni visiwani Zanzibar kwani wanawake wengi wa Zanzibar wanategemea
maisha kutokana na kipato cha mwani.
UZALISHAJI NA
USAFIRISHAJI MWANI ZANZIBAR
Kwa mujibu wa wizara ya Uchumi wa Buluu na Uvuvi,
uzalishaji wa zao hilo hapa visiwani umeongezeka kutoka, tani 10,531 kwa mwaka
2021, hadi tani 12,594 kwa mwaka 2022 sawa na ongezeko la asilimia 20.
Kwa mujibu wa taarifa za wizara hiyo, usafirishaji
wa mwani nje ya nchi umeongezeka kutoka tani 12,124 kwa mwaka 2021 hadi tani
13,972 mwaka 2022, sawa na ongezeko la asilimia 15.
Zanzibar ni nchi ya nne 4 duniani kati ya nchi
zinazozalisha mwani (Mwekundu) ikiongozwa na nchi ya Indonesia, Ufilipino na
Malaysia, ambapo mwaka 2021 Zanzibar imezalisha zaidi ya tani 12,000.
SERIKALI YA
AWAMU YA NANE INAVYOSAIDIA KILIMO CHA MWANI
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la
Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi, alisema Zanzibar ni nchi inayoongoza kwa
uzalishaji wa mwani barani Afrika uzalishaji umeongezeka zaidi kwa tani 12,594
kwa mwaka 2021/22.
Alisema mafanikio yote yanatokana na utekelezaji
wa sera na mikakati ya uchumi wa buluu ambapo serikali imeunda sera mpya ya
uchumi wa buluu pamoja na mikakati ya uzalishaji wa mazao ya baharini ukiwemo
mwani.
Alisema serikali imewekeza fedha nyingi katika
kuwasaidia wakulima na wajasiriamali wa sekta ya mwani wapatao 5,000 Unguja na
Pemba kwa kuwapatia boti maalumu za kuwawezesha kwenda katika maji ya kina
kirefu zaidi kwa ajili ya ulimaji wa mbegu bora za mwani.
TAFITI ZA
KITAALAMU KUHUSU MWANI
Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na Suleyum Talib
Ali kutoka Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar ulioangazia mchango wa kilimo cha
mwani katika uchumi wa buluu, ulieleza kuwa zao hilo limekuwa na nafasi ya
pekee katika kusaidia maisha ya wakulima.
Kwa mujibu wa utafiti huo mkulima wa mwani kwa
mwezi ana uhakika wa kupata kati ya shilingi 120,000 hadi 200,000, ambazo
humsaidia katika kukabiliana na changamoto mbalimbali za kimaisha katika
familia.
Mtafiti wa mwani Flower Msuya, yeye alisema kilimo
cha mwani kinasaidia kwa kiasi kikubwa maisha ya wakulima na wajasirimali
wanaouza bidhaa za zao hilo.
Mwani ni wa pili kuingiza fedha za kigeni
Zanzibar, kilimo cha zao hilo kina manufaa makubwa sana kwa wanawake wa visiwa
hivyo kwa kuwa kimeboresha maisha yao.
"Katika utafifi wetu tumebaini kuwa mwani
unaoitwa cottonie unaweza kulimwa kwenye maji mengi na ndio mwani bora zaidi,
hivyo tunatumia tuber note kulima mwani huo, njia hiyo inatumia neti na bomba
kupanda mwani kwenye bahari badala ya vijiti”, alisema.
DIRA YA
MAENDELEO ZANZIBAR
Kwa kutambua shughuli za wakulima wa mwani, Dira
ya mpango wa maendeleo endelevu ya Zanzibar ya mwaka 2020-2050 imeeleza,
kupitia matumizi sahihi ya bahari chini ya mikakati ya muelekeo wa uchumi wa
buluu ni kupatikana faida ya ajira na kupunguza umasikini kwa watumiaji wa
rasilimali hiyo.
Aidha dira imeiweka uchumi wa buluu kama sekta
muhimu ya kiuchumi ambayo itaufanya uchumi wa Zanzibar kuwa endelevu.
Dira hiyo inakwenda sambamba na malengo ya 14 na 6
ya agaenda ya bara la Afrika 2063, ambayo inasisitiza matumizi mazuri na
endelevu ya bahari katika kuleta maendeleo.
Comments
Post a Comment