NA HAJI NASSOR, PEMBA@@@@
WANANCHI wanaotumia
barabara ya Mkoan-Chake chake, wameikumbusha serikali kuanza ujenzi wa barabara
hiyo kwa kiwango cha lami, ili waitumie kwa utulivu wanapokuwa katika harakati
zao za maendeleo.
Walisema, kwa sasa barabara hiyo
imekuwa kero kwao, kutokana na uwepo wa mashimo, misingi, na mipasuko mipana
ambayo wakati mwingine husababisha ajali ambazo zinaweza kuepukika.
Wakizungumza na mwandishi wa habari
hizi, baada ya kutokezea ajali hivi karibuni eneo la Ngezi, walisema, mashimo
ambayo huongezeka kila mvua zinaponyesha, ndio chanzo cha ajali.
Mmoja kati ya wananchi hao Anuwari
Is-haka Omar wa Matuleni, alisema wakati umefika sasa kwa serikali kutimiza
ahadi ya ujenzi wa barabara hiyo.
‘’Kwa muda mrefu tumekuwa tukiskia
kuwa ujenzi wa barabara hii, utaanza wakati wowote, lakini hadi sasa imeshapita
miaka hatuoni kinachofanyika,’’alisema.
Kwa upande wake Mwanaisha Omar Haji
wa Kipapo, alisema katika eneo la Chanjamjawiri, limekuwa maarufu kwa vyombo
hasa vya maringi mawili, kugongana na kuanguka, kunakosababishwa na uchakavu wa
barabara.
‘’Barabara imepasuka na kutengeneza
mashimo makubwa, ambayo husababisha madereva kutozingatia upande aliopaswa
kupita, jambo ambalo husababisha ajali,’’alieleza.
Nae Hamida Mjaka Muhsin na mwenzake
Aisha Makame Juma wa Mizingani, wamesema wamekuwa na gamu wanapotaka kwenda
miji ya Chake chake au Mkoani, kutokana na uchakavu wa barabara yao.
Walisema, wanaamini serikali
itaijenga barabara hiyo, ingawa hawajui ni lini, kutokana na kuwekewa ahadi kwa
muda mrefu.
‘’Hata hivi karibuni Rais wa
Zanzibar Dk. Hussein Ali Mwinyi, alitueleza ana nia ya kuijenga lakini, ahadi
kama hiyo ilishawahi kutolewa na mtangulizi wake, sasa inaumiza matumbo,’’alifafanua
Hamida.
Dereva mmoja wa garia ya abiria
inayofanyakazi katika mji wa Wamba na Chake chake, alisema, kwa sasa hawapitii
tena vijiji vya Ngwachani, Kuyuni, Ngezi, Mgagadu, Kimbuni na Mizingani
kutokana na kuharibika kwa barabara ya Chake chake -Mkoani.
‘’Kwa sasa inatulazimu kupitia
barabara ya Kipapo-Mgelema hadi Wambaa, maana barabara kwa kupitia Mizingani
imeharibika vibaya,’’alisema dereva huyo.
Akijibu hoja za Mwakilishi wa Jimbo
la Mkoani, juu ya hatma ya ujenzi wa barabara hiyo, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti
wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi, alisema tayari mkandarasi wa
ujenzi wa barabara hiyo, ameshapatikana, ambapo ujenzi utakapoaanza mkandarasi
huyo, atashirikiana na kampuni ya Mecco.
Alisema pamoja na kupatikana kwa
mjenzi huyo, tayari mkataba umeshasainiwa na hata fedha za utangulizi
zimeshatolewa, ikiwa ni miongoni mwa matayarisho ya ujenzi wa barabara hiyo.
Dk. Mwinyi alisema, baada ya
matayarisho kukamilika, mkandarasi huyo anatarajiwa kuingia barabara wakati
wowote kuanza ujenzi huo, ili kuona wananchi wanaitumia.
Alieleza kuwa, katika kufanikisha
hilo, kazi kubwa ya serikali ni kuangalia uwezekano wa kulipa fidia, kwa ajili
ya majengo na vipando vya wananchi, ambavyo vimeshaonekana kuathirika wakati wa
ujenzi huo.
Dk. Mwinyi alieleza kuwa, hana
shaka kuwa barabara za Chake chake – Mkoani na Chake chake -Wete, mara
zitakapomalizika ujenzi wake, itakuwa ni sehmu ya kukifungua kisiwa cha Pemba,
kiuchumi.
‘’Wananchi wawe wastahamilivu, kwa
kuwepo kwa kero ya barabara ya Mkoani- Chake chake, na taarifa tulizonazo ni
njema, maana mjenzi ameshapatikana ni Propav atashirikiana na kampuni ya Mecco
na hata fedha za utangulizi tayari,’’alieleza.
Aidha Rais huyo wa Zanzibar na
Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi, alisema hata fidia
kwa upande wa ujenzi wa uwanja wa ndege kwa sehemu kubwa zimeshatolewa kwa
wananchi na zilizobakia mchakato unaendelea.
Mwisho
Comments
Post a Comment