NA HAJI NASSOR, PEMBA@@@@
WANAWAKE wa shehia ya Mgelema wilaya ya Chake
chake Pemba, wamesema baada ya kukamilika kwa ujenzi wa barabara yao kwa
kiwango cha lami, roho zao zimewatua na hasa inpotekezea kutaka kwenda
hospitali kuu, kufuata huduma za mama na mtoto.
Walisema, kwa karne zaidi ya moja, hawakuwa na furaha na
wakielewa na machungu, inapotokezea wamepewa rufaa ya kwenda hospitali ya
wilaya ya Chake chake, kutokana na shida ya barabara yao, ilivyokuwa.
Wakizungumza na mwandishi wa habari hizi kijijini hapo,
mara baada ya kufunguliwa kwa barabara yao ya Kipapo-Mgelema, na Makamu wa
Kwanza wa Rais Zanzibar Othman Massoud Othman, walisema sasa joto limewatua.
Mmoja kati ya wanawake hao Maryam Mohamed Issa, alisema ijapokuwa
ni mgeni kijijini hapo, lakini ameshatimiza miaka tisa ya mateso, shida na tabu
ya kuitumia barabara hiyo.
‘’Binafsi, mara mbili nilipokuwa mjamzito, nilitakiwa niripoti
hospitali ya wilaya ya Chake chake, kwa uchunguuzi zaidi, lakini nilishindwa
kutokana na uchakavu wa barabara ulivyokuwa,’’alieleza.
Nae Mayasa Hassan Abdalla, alisema kwa mateso waliyokuwa
nayo, hawakutarajia kuwa iko siku, wengepata barabara nzuri na ya kisasa, kama
iliyofunguliwa hivi karibuni.
‘Tulishazoea sisi wajawazito hali ikiwa ngumu, na hasa
kwa siku za mvua, ni kubebwa kwa magunia au gari za Ng’ombe, hadi bara bara kuu
Kipapo,’’alifafanua.
Hata hivyo alisema, kwa sasa wamepata faraja ya kuongezewa
thamani ya utu na heshima yao, kutokana na kuwepo kwa bara bara hiyo, ya
kisasa.
Kwa upande wake Hassina Shehe Ussi na mwenzake Raya Hamad
Naasor walisema, kwa sasa wana hakika hakuna dhiki ya usafiri na hasa kama
ikitokezea, mwenzao amepata na hitilafu ya huduma za mama na mtoto.
Wakati huo huo wanawake hao, wameiomba wizara husika
kuangalia uwezekano wa kuwekewa matuta katika maeneo ya mikusanyiko ya watu,
ambapo bara bara hiyo imepita.
Kwa upande wa Omar Iddi Hassan, alisema barabara hiyo sio
tija kwa wajawazito pekee, hata wao kwani ndio wasafirishaji wakubwa, ikitokezea
mjamzito kupelekwa hospitali.
‘’Hakukua na tajiri aliyethubutu kuleta gari yake Mgelema,
tena kwa bei yeyote, hivyo ilikuwa akitokezea mazazi amepata changamoto,
ilikuwa ni dhiki mara mbili,’’alieleza.
Nae Omar Ussi Ali alisema, kilichobakia kwa sasa ni kwa
watumiaji wa barabara hiyo, na wananchi wingine, kila mmoja kuwa mlinzi kwa mwenzake.
Akizungumza hivi karibuni Mkuu wa wilaya ya Chake chake
Abdalla Rashid Ali, alisema serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, imekuwa
inatekeleza kila inachokiahidi.
Wakati huo huo Mkuu huyo wa wilaya, alisema wajibu wa
kuitunza barabara hiyo sio jukumu la wizara husika pekee, bali kila mmoja na
kwa nafasi yake.
Awali barabara hiyo ilifunguliwa hivi karibuni na Makamu
wa Kwanza wa Rais Zanzibar Othman Massoud Othman, ambae nae aliwataka wananchi
hao, kuhakikisha wanaitunza barabara hiyo.
Katibu Mkuu wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi
Zanzibar Khadija Khamis Rajabu, alisema ujenzi wa barabara hiyo ya Kipapo-
Mgelema yenye urefu wa kilomita 5.3, ujenzi wake uligawika katika awamu mbili, ambapo
moja wapo ni ujenzi wa Kipapo –Mgelem.
Aidha Katibu Mkuu huyo alieleza kuwa, barabara hiyo ina upana
wa mita sita, na mabega {road shoulder} yenye upana wa mita 0.5
kwa kila upande, na ujenzi wake umetumia mfumo wa lami moto.
Alieleza kuwa, kama barabara hiyo ya Kipapo- Mgelema
itatunzwa inaweza kuishi kwa wastani wa miaka 10, bila ya kuharibika.
Ujenzi wa barabara hiyo, hadi kukamilika kwake, umeshatumia
zaidi ya shilingi bilioni 2.109, fedha zilitolewa na serikali ya Mapinduzi, kupitia
Mfuko wa Bara bara na imejengwa na Wakala wa Barabara Zanzibar.
Mwisho
Comments
Post a Comment