NA ZUHURA JUMA,
PEMBA@@@@
MKAGUZI wa shehia
ya Pandani wilaya ya Wete Pemba, Inspekta wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Kaskazini
Pemba Khalfan Ali Ussi, amewataka wananchi kuchukua tahadhari na kujikinga na
majanga mbali mbali yanayoweza kutokea ikiwemo ya moto.
Alisema kuwa, ni
vyema kufuata utaratibu nzuri, wakati wanapoamua kujenga nyumba katika maeneo
yao, kwa kuweka nafasi ya kutosha baina ya nyumba moja na nyingine, ili
linapotokea janga la moto lisiweze kuathiri nyumba nyingi.
Aliyasema hayo
wakati akikabidhi msaada wa vifaa vya skuli, kwa watoto wa familia ya mzee
Mwalimu Kombo Said wa kijiji cha Madebeni shehia ya Pandani wilaya ya Wete, kufuatia
tukio la moto lililounguza nyumba yao Novemba 11 mwaka jana.
Alisema kuwa,
familia hiyo ilipata janga la moto ambao uliunguza nyumba yao na kuteketeza
kila kitu kilichokuwemo ndani, hali iliyomfanya kuiahidi familia hiyo
kuwanunulia watoto vifaa vyote vya kusomea.
"Nawapongeza
wananchi kutafsiri kwa vitendo dhana ya ushirikishwaji wa jamii, kutokana na
ushirikiano wao wa pamoja katika kuisaidia familia hiyo kwa hali na mali, baada
ya kufikwa na tukio hilo la kuhuzunisha," alisema Mkaguzi huyo.
Aidha Inspekta huyo
aliwataka wananchi hao, waendeleze umoja na upendo, kwani majanga kama hayo,
hayachagui bali yanaweza kumfika mtu yeyote na wakati wowote, hivyo kila mmoja
ni muathirika hawana budi kusaidiana.
Katika hatua
nyengine, Mkaguzi huyo aliwaasa wazazi na walezi wa shehia hiyo, kuwahimiza na
kuwasimamia vijana wao, washughulikie masomo yao zaidi, ili kujitengenezea
maisha bora ya baadae, sambamba na kujiepusha na makundi maovu.
‘’Msingi bora na
imara wa kumjengea mtoto wetu, ni kuwatenga mbali majanga mbali mbali ya udhalilishaji
na kila wakati kuwahimiza, ili washugulike na masomo yao,’’alieleza.
Kwa upande wao
wanafamilia, iliyoathirika kwa janga la moto pamoja na wanakijiji, walimpongeza
Mkaguzi huyo, kwa kuonesha moyo wake wa upendo kwa kuisaidia familia hiyo,
jambo ambalo limewafanya wajenge imani kwake.
Walieleza kuwa, Jeshi
la Polisi mkoa wa kaskazini Pemba, limewakabidhi mtu muhimu na adhimu anaejali
watu mbali mbali, jambo ambalo wamekuwa wakiridhia kila anachoweleza katika
kuzuia uhalifu.
Aidha wananchi hao,
wamemuahidi Inspekta huyo kuwa, watawasimamia vijana wao katika kuhakikisha
wanapata elimu bora na kufuata maadili yaliyo mema, ili wajengeke vizuri na
kupata mafanikio katika maisha yao ya kila siku.
Miongoni mwa vifaa
vilivyotolewa na Mkaguzi huyo ni fomu za skuli, viatu, mabuku, kampasi pamoja
na vifaa vyengine vya kusomea ambavyo vimegharimu kiasi cha shilingi 230,000
huku watoto wawili wakifaidika na msaada huo.
MWISHO
Comments
Post a Comment