NA HAJI NASSOR, PEMBA@@@@
MAKAMU wa Pili wa Rais Zanzibar Hemed Suleiman
Abdalla, amesema, serikali inampango wa kuzijenga bandari za Wesha, Wete na
Shumba, ikiwa ni miongoni mwa maono ya Rais wa Zanzibar Dk. Hussein Ali Mwinyi,
kukifungua kisiwa cha Pemba kiuchumi.
Alisema kwa kuanzia, tayari shughuli kadhaa
zimeshafanyika kwa awamu ya kwanza, kuelekea ukamilishaji wa upanuzi wa bandari
ya Mkoani, ikiwemo ujenzi wa njia za kupitia abiria, ujenzi wa eneo la kuwekea
makontena pamoja na ununuzi wa mashine za kushushia makontena hayo.
Makamu huyo wa Pili, aliyasema hayo Disemba 7, mwaka 2024, bandarini
Mkoani Pemba, mara baada ya uzinduzi wa bandari hiyo, ikiwa ni shamra shamra za
miaka 60 ya mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964,
Alisema, ili kuelekea uchumi mzuri, serikali inayodhamira
ya kweli ya kuhakikisha bandari nyingine za kisiwani Pemba, zinajengwa na zinakuwa
za kisasa, ili wananchi watanue wigo wa usafiri na usafirishaji.
Alieleza kuwa, kazi hiyo inatarajiwa kuanza wakati
wowote, kwani baadhi ya kazi za muhimu kuelekea ujenzi wa bandari hizo,
zimeshafanyika, kwa lengo la kukifungua kisiwa cha Pemba kiuchumi.
‘’Leo (jana), tukiwa ndani ya miaka mitatu ya uongozi wa
Dk. Mwinyi samba mba na maadhimisho ya miaka 60 ya mapinduzi, bandari yetu ya
Mkoani, iliyoasisiwa mwaka 1925, inaelekea kuwa ya kimataifa,’’alieleza.
Akizungumzia upanuzi wa bandari hiyo, alisema lengo la
serikali ni kuona, bidhaa zinapotoka nje ya nchi, zinaletwa moja kwa moja
katika badari hiyo kwa kushushwa.
Alieleza kuwa, mwisho wa wafanyabiashara wa kisiwani
Pemba, kukumbana na changamoto ya uingaji wa bidhaa zao na kugharimu fedha nyingi,
unaelekea kuwa mwisho, mara baada ya kumalizika kwa mradi huo.
Alifahamisha kuwa, kinachotakiwa kwa wananchi ni kuamini
na kuipa nafasi serikali, kukamilisha awamu nyingine ya upanuziu huo wa bandari
ya Mkoani, kama ilivyoahidi na Rais wa awamu ya nane Dk. Hussein Ali Mwinyi.
‘’Lengo la upanuzi wa bandari ya Mkoani, ni kuwaondolea
adha wasafiri, wasafirishaji wanaotoa a kuingiza bidhaa, ili kuona
haziwagharimu, na kisha kuuza bei ya juu kwa walaji,’’alieleza.
Akizungumzia usafiri wa baina ya Unguja, Tanzania, Tanga
na Pemba, Makamu huyo wa Pili, alisema tayari serikali iko katika hatua za mwisho,
za ununuzi wa boti mbili za mwendo kasi.
Alieleza kuwa, boti hizo zinatarajiwa kufanya safari zake,
baina ya miji hiyo, ili kuona wananchi wanakuwa na usafiri wa uhakika, pamoja
na ile Meli ya M.V Mapinduzi II, iko katika hatu za mwisho ya kukamilika kwake.
‘’Kwa sasa meli hiyo, iko mbioni kukamilika, na serikali
imeshaidhinisha ununuzi wa boti mbili, kwa ajili ya miji hiyo, na ziko hatua za
mwisho kukamilika ujenzi wake,’’alieleza.
Akizungumza miaka 60 ya Mapinduzi, alisema yanashabihiana
na kuasisiwa kwa bandari hiyo, kuanzia mwaka 1925, ambapo kisha mwaka 1989 bandari
hiyo ikafanyiwa matengenezo.
‘’Tunapogusa maana halisi ya mapinduzi, ni maendeleo kupitia
miradi mikubwa, ambayo inamgusa kila mmoja kwa alipo, na Dk. Mwinyi anakoleza
mwendo wa kasi,’’alifafanua.
Mapema Mkurugenzi mkuu, wa Shirika la Bandari Zanzibar
Akfu Khamis, alisema bandari ya Mkoani, imewekwa kama njia kuu ya kukifungua
kisiwa cha Pemba kiuchumi, na hasa kupitia sera ya uchumi wa buluu.
Alisema kuwa, serikali, imedhamiria kuipanua bandari hiyo
na kuiwezesha kumiundombinu, ili iweze kupokea meli za kimataifa moja kwa moja,
kutoka nje ya nchi.
Mkurugenzi huyo Mkuu, alieleza kuwa, mradi huo mkubwa wa
bandari, ulikuwa na awamu kadhaa ikiwemo ya kuweka kwa vikalio vya meli, na ujezi
wa eneo la kuwekea makontena lenye upana wa skweya mita 4,200 .
Alieleza kuwa, awamu ya pili ni ujenzi wa njia kwa ajili
ya kupita zana nzito, njia maalum ya watembea kwa miguu yenye upana wa mita 2.5
na uwekaji wakivuli kwenye njia hizo.
‘’Gharama za mradi huo, kuanzia awamu ya kwanza hadi ya
pili, umeshatumia shilingi bilioni 6.77, pamoja na ununuzi wa mashine ‘crane’
tatu, mbili zikiwa na ujanzo wa tani 45 na moja tani 90, kwa ajili upakuzi wa
makontena na mezani ya kidigitali,’’alieleza.
Kwa upande wake, Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na
Uchukuzi Zanzibar Dk. Khalid Salum Mohamed, alisema Dk. Mwinyi ameweka vipaumbele
vinne, ikiwemo cha Uchumi wa buluu, utalii, miundombinu ya usafiri na
usafirishaji, pamoja na huduma za kijamii.
‘’Kwenye miundombinu, Dk. Mwinyi amedhamira ujenzi wa
kiwanja cha ndege, ujenzi wa bandari za Wesha, Mkoani, Shumba na Wete, ili kuongeza
huduma za kijamii na kukuza uchumi,’’alisema.
Mkuu wa mkoa wa kusini Pemba Mattar Zahor Massoud, alisema
kila mmoja ni shahidi, juu ya miradi mikubwa iliyotekelezwa baada ya mapinduzi,
ikiwemo upanuzi wa bandari ya Mkoani.
Mwisho
Comments
Post a Comment