IMEANDIKWA NA ZUHURA JUMA, PEMBA@@@@
SPIKA wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar Zubeir Ali Maulid amewataka vijana kutumia vyema fursa zilizopo, ili kustawisha uchumi wa nchi na kujiletea maendeleo.
Aliyasema hayo Disemba 6, mwaka 2024 wakati akifungua kongamano la miaka 60 ya Mapinduzi Zanzibar lililoandaliwa na Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo katika Ukumbi wa ZSSF Tibirinzi Chake Chake Pemba.
Alisema kuwa, Zanzibar imepiga hatua kubwa kimaendeleo katika sekta zote tofauti na kabla ya Mapinduzi, ambapo Serikali ya awamu ya nane imeweka mazingira mbali mbali ya kuwawezesha wananchi wake kiuchumi, hivyo ni vyema wakazitumia zaidi fursa hizo kwa ajili ya kujiimarisha.
"Hatua hii tuliyofikia sasa inaenda sambamba na mafanikio ya Mapinduzi yetu matukufu ya Zanzibar, hivyo hatuna budi kuyaenzi na kuyaendeleza kwa maslahi bora ya Taifa letu," alisema spika huyo.
Aidha alieleza kuwa, ni wajibu wa kila mwananchi kuwa na uzalendo, kulinda amani ya nchi na kuwa tayari kukemea kitendo chochote cha uvunjifu wa amani, kushirikiana na viongozi katika kujenga nchi.
Kwa upande wake Katibu Mkuu Kiongozi na Katibu wa Baraza la Mapinduzi, Mhandis Zena Ahmed Said alieleza kuwa, Serikali imesaidia kuleta mabadiliko makubwa katika sekta zote, ili kuhakikisha nchi inapata maendeleo na kukiinua kisiwa cha Pemba kiuchumi.
"Sekta zote zinazotoa huduma zimepewa kipao mbele ili kusudi zitoe huduma bora na kuimarisha maisha ya wananchi, sekta hizo ni kama vile sekta ya utalii, uchumi wa buluu, elimu, afya na uwezeshaji wananchi kiuchumi, hii itasaidia sana kupata maendeleo", alieleza.
Mapema, Waziri wa Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Zanzibar Tabia Maulid Mwita alisema, lengo la kongamano hilo ni kuongeza uelewa kwa wananchi ambao wataendeleza kuijenga zanzibar kimaendeleo pamoja na kuijua historia ya Mapinduzi.
"Kongamano hili linatusaidia kujua mambo mbali mbali ya kihistoria, hivyo tunapata faida ya kuchota fikra na maona ya mambo mengi, kwa hiyo ni muhimu sana kwetu kwani tunapata uelewa zaidi", alieleza Waziri huyo.
Akiwasilisha mada ya umuhimu wa amani, Balozi Amina Salum Ali alisema suala la amani na utulivu iliyopatikana baada ya Mapinduzi ndio iliyochangia kuleta maendeleo ya Zanzibar ambayo hapo awali yalikosekana.
Nae Dk. Abdulhamid Yahya Mzee akiwasilisha mada ya umuhimu wa uzalendo alisema, ni vyema wananchi kuwa na maandili mema kwani itasaidia kufanya kazi ya uzalendo moja kwa moja.
"Maadili na uzalendo vinakwenda sawa, ikiwa una maadili mema basi ni lazima utakuwa mzalendo, hivyo tuwafundishe vijana wetu mambo haya na waachane na utandawazi ambao kwa asilimia kubwa huharibu maadili yao," alifahamisha.
Katika kongamano hilo jumla ya mada nne zimewasilishwa ikiwemo umuhimu wa kutunza amani, umuhimu wa uzalendo katika kuleta maendeleo, maendeleo ya uchumi wa Zanzibar katika miaka 60 ya Mapinduzi ya Zanzibar, mafanikio fursa na changamoto, pamoja na malengo ya Mapinduzi, muelekeo wa Serikali ya awamu ya nane kuifungua Pemba kiuchumi.
MWISHO
Comments
Post a Comment