Skip to main content

MAJUKUMU MAZITO YA FAMILIA CHANZO CHA WANAWAKE KUTOGOMBEA UONGOZI

 




IMEANDIKWA NA ZUHURA JUMA, PEMBA

Jamii ya Tanzania, kama ilivyo katika nchi nyingi nyengine, imejenga mazoea ya kuwa mwanawake ni mama wa nyumbani tu na hapaswi kushiriki au kushirikishwa katika mambo ya maendeleo.

 

Kwa maana nyengine mwanamke amekuwa kama abiria katika basi na hana maamuzi juu ya safari, seuze ya kupewa usukani wa kuongoza hicho chombo.                   

 

Mtazamo huu uliokuwa unatumika kwa muda mrefu umeiathiri jamii na kumuacha mwanamke kuwa nyuma, jambo ambalo sio sahihi kabisa.

 

Hali hii ipo kinyume na mafunzo na maelekezo ya dini mbali mbali. 

 

Kwa mfano, katika dini ya Kiislamu mwanamke hatakiwi kuachiwa pekee mzigo mzito wa nyumbani na pamekuwepo matokeo ya mwanamke kupewa uongozi hata katika masuala mazito, kama ya kuongoza kikosi kwenye vita.

 

Zipo hadithi sahihi na simulizi nyingi juu ya namna wanawake walivyoongoza kwa mafanikio, wakiwa kama majeshi.

 

Mzigo mzito wa nyumbani wanaoachiwa akina mama umekuwa sababu kubwa ya kuwakwaza na kushindwa kushiriki katika shughuli za jamii, uchumi, siasa na maendeleo.

 

Katika visiwa vya Unguja na Pemba wapo wanawake ambao wanakiri kwamba kikwazo kikubwa kwao kujiendeleza kimaisha na hata kushika nafasi za uongozi ni mzigo mzito wa malezi na kazi za nyumbani.

 

Miongoni mwa wanawake wenye uzoefu wa kuielewa hali hii inayowakuta wanawake wengi ni Saumu Ali Abeid, mkaazi wa Fuoni, Unguja.

 

Anasema, uzito wa kazi za nyumbani unaomzunguka mwanamke ni pamoja na kupika, kushughulikia usafi wa nyumba, malezi ya watoto, kumhudumia mume na wakati mwengine wazee wa mume na wa kwake mwenyewe.

 

‘’Katika hali kama hii sio rahisi kwa mwanamke kujiingiza katika harakati za kugombea uongozi," anaeleza.

 

Anafahamisha kwamba, mwanamke anayezongwa na kazi nyingi za nyumbani hushindwa kushiriki kwenye vikundi na kutoa mawazo yake ambayo yangempa ujasiri na maarifa na hivyo kujiamini kuwa anaweza kuongoza wenzake au jamii.

 

Mwananchi wa kijiji Kipangani Wete, anasema, mzigo wa kazi za nyumbani aliokuwa nao mwanamke umepelekea kuwepo wanawake wachache katika vyombo vya maamuzi.

 

Hii ndio moja ya sababu ya kushindwa kutatuliwa changamoto kadhaa zinazowakabili wanawake, kwani panakuwa hakuna mtetezi wa hali ya wanawake katika vyombo vya maamuzi.

 

"Kazi za nyumbani zinatuchosha sana na kushindwa kujiingiza kwenye mambo ambayo yatailetea maslahi jamii kwa ujumla," aliongeza.

 

Maida Saleh yeye ameona mzigo mzito wa nyumbani unadumaza fikra za mwanamke na hivyo kupoteza haki zao.

 

Salama Mohamed wa Ole Pemba, anasema mara nyingi mrundiko wa kazi za nyumbani unawazuwia wanawake kushiriki katika nafasi za uongozi.

 

Hafidh Abdi Said ambae ni Mkurugenzi wa mradi wa kutoka PEGAO anasema, kazi nyingi za nyumbani zinasababisha wanawake wengi kutoshiriki katika uongozi.

 

‘’Tokea mwanamke anapoamka ni kazi mpaka jioni huwa hana hata muda wa kupumzika au kufanya mambo mengine nje ya kuta ya nyumba yake’’, aliongeza.

 

Alitoa nasaha kwamba kama jamii itaendelea kuwaachia mzigo mzito akinamama basi hata maendeleo ya nyumbani yatachelewa kupatikana.

 

‘’Mwili unahitaji mapumziko ili baadaye uweze kufanya vizuri’’, anaeleza.

Katibu Kanda ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA Pemba, Habid Ali Khamis anaeleza, wanawake wanakosa msaidizi, hivyo hata anapokwenda kwenye vikao anachelewa na hatimae kukosa ajenda zilizozungumzwa, ambapo yeye huishia kuwa msikilizaji.

Mwalimu Saleh Nassor Juma ambae ni Katibu wa ACT Wazalendo Mkoa wa Chake Chake kichama, anasema elimu inahitajika zaidi ili wagombee na kazi za nyumbani isiwe kikwazo kwao kuwa viongozi.


 

ATHARI YAKE 

Mratibu wa TAMWA Pemba Fat-hiya Mussa Said anasema, akinamama watashindwa kuingia katika vyombo vya maamuzi na hatimae hawana mtetezi katika masuala yao.


''Tunajitahidi kuwajengea uwezo wanawake kwa kuwapa elimu na jamii kwa ujumla, ili kuondosha dhana potofu na wajiamini kuingia majimboni,'' anafahamisha.





Saumu Ali mkaazi wa Fuoni anasema, mwanamke huwa anadumaa kiakili pale ikiwa hana jengine la kufanya baada ya kuhudimia nyumbani.

 

"Mwanamke aliyeelemewa na kazi za nyumbani huwa hapati fursa ya kujiendeleza, inawezekana ana mawazo mazuri ya kuleta mabadiliko na maendeleo katika jamii, lakini hapati fursa ya kwenda kuyatoa, hivyo, mawazo yake huwa anakaa nayo tu moyoni," aliongeza.

 

Awatif Ramadhan Awesu  wa Kariakoo Dar-es-salaam anataja athari ya mwanamke kubanwa na kazi za nyumbani  ni kuendeleza ukosefu wa usawa wa kijinsia na kuzuia maendeleo yao kitaaluma.

 

Anasema mwanamke anayezidiwa na majukumu ya kifamilia anakosa muda wa kujijengea uwezo, kujifunza na kujiendeleza katika uwanja wa uongozi.

 

‘’Hali hiyo huchangia ukosefu wa usawa kwenye fursa za uongozi na kuwafanya wanawake washindwe kufikia uwezo wao kamili katika maswali ya kazi na uongozi’’, alisisitiza.

 

Zainab Hassan Ali, mkaazi wa Bopwe Wete anasema inakuwa vigumu kwa mwanamke anayekuwa nyumbani wakati wote kupanua akili yake au kuchanganua mambo kwa sababu akili yake inabaki nyumbani na haitoki nje ya kuta za nyumba hizo.

 

TUNAWASAIDIAJE WANAWAKE.

 

Mkaazi wa shehia ya Uwandani Wilaya ya Chake Chake, Safia Abdalla, anaamini ushirikiano katika familia unawapa nafasi wanawake kushiriki katika masuala ya kijamii na hatimae kuwa na ujasiri wa kivifikia vyombo vya maamuzi.

 

Anashauri kutolewa elimu zaidi ili imsaidie mwanamke kujipanga mapema kushiriki katika mambo mbali mbali ya kijamii, kiuchumi na kimaendeleo.

 

Kilichoitokeza katika mahojiano zaidi na wanaume na wanawake wa maeneo mengine ni kuwepo umuhimu wa kuubadili mwenendo wa maisha katika familia zetu na zaidi kwa wanaume kuwapunguzia kwa njia moja au nyenine wenza wao na hata watoto wao wa kike mzigo mzito wa kazi za nyumbani.


Wapo walioshauri wanawake wapewe elimu ya kujitambua ili wapate uelewa mzuri utaowafungulia njia ya kujiendeleza na hata kuwa viongozi katika jamii.

                     MWISHO.

 

Comments