NA HAJI NASSOR, PEMBA@@@@
WADAU wa Tume ya Utangaazaji Zanzibar, kisiwani
Pemba, wamekutana na watendaji wa Tume hiyo, tayari kwa ajili ya kuanza
mchakato, wa kuifanyia mabadiliko sheria yao nambari 7 ya mwaka 1997.
Kwenye kikao hicho, kilichofanyika leo Disemba 19, 2023 ukumbi wa wizara ya
Habari Gombani Chake chake, pamoja na mambo mingine, watendaji hao wa Tume,
waliwasilisha mapendekezo yao, na kisha kupokea ya wadau wao.
Akizungumza kabla ya upokeaji wa maoni hayo, Katib Mtendaji
wa Tume ya Utangaazaji Zanzibar Suleiman Abdalla Salim, alisema, wanakusudia
kuwa na sheria rafiki kwa vyombo vya habari vya utangaazaji na vile vya
mtandaoni.
Alisema, ndio maana Tume imeanza kuwashirikisha wadau wa
Unguja na Pemba, ili nao kupata nafasi ya kutoa maoni yao, kuelekea sheria mpya
hapo baadae.
Alieleza kuwa, haikuwa busara kwa Tume kujifungia ndani
na wataalamu wake na kisha kuwasilisha rasimu ya sheria ngazi ya Makatibu wakuu,
bila ya kukutana na wadau wao.
‘’Tume kwa sasa, imeshaanza mchakato wa kuifanyia Marekebisho
sheria yake nambari 7 ya mwaka 1997, pamoja na yale marekebisho yake yaliyofanywa
mwaka 2010,’’alifafanua.
Akigusia baadhi ya vifungu ambavyo kwa sasa wanavipitisha
kwa wadau na kutaka maoni, ni pamoja na jina la taasisi, mundo na masharti ya
kuomba leseni.
Afisa Sheria wa Tume ya Utangaazaji Zanzibar Khadija Mabrouk
Hassan, alisema wanatamani kuwa na sheria rafiki kwa utangaazaji na
wanaoandikia maudhui mtandaoni.
Alisema sheria hiyo, vipo vifungu wanataka kuvipeleka kwa
wadau, ili wavijadili na kuwa sheria
yenye kwenda na wakati uliopo kwa maslahi ya umma.
Alifafanua kuwa, kwa mfano kifungu cha 16 cha kutoa
adhabu, kwamba atakayevunja masharti ya leseni, pamoja na kwamba ataonywa au
kutakiwa asawazishe vipindi vyake, lakini akishindwa atatozwa faini ya shilingi
milioni 1.
‘’Lakini anaweza kusitishiwa leseni yake ya utangaazaji
pamoja na kufutiwa kabisa, pindi ikionekana ameshindwa kusawazisha kama sheria
inavyotaka kwa sasa,’’alifafanua.
Aidha alieleza kuwa, pia kifungu cha 17 kinachoelezea
haki na wajibu wa utangaazaji juu ya utaratibu wa kukanusha habari, iliyotangaazwa
ambayo sio ya ukweli.
Akifungua kikao hicho, Afisa Mdhamini wiara ya Habari,
Vijana, Utamaduni na Michezo Pemba Mfamau Lali Mfamau, aliwataka wanaoendesha
vyombo vya habari pasi na kuvisajili, wafanye hivyo haraka.
Alieleza kuwa, sasa wakati umefika kwa Tume ya
Utangaazaji kutowafumbia macho, kwani kufanya hivyo, ni kosa kwa mujibu wa
taratibu zilivyo.
‘’Niwatake wale wenye tv, redio na tovuti na blogi,
wafike Tume kujisaliji, ili wawe halali na huru kuendesha shughuli zao za kihabari,’’alifafanua.
Akitoa maoni yake, Mkurugenzi wa Jamii tv Ali Massoud
Kombo, alipendekeza kuwa, ada ya kila mwaka ya shilingi 500,000 ipunguzwe na
iwe shilingi 100,000.
Aidha alipendekeza kuwa, katika Bodi ya Tume, lazima
kutengwe nafasi maalum kwa ajili ya wajumbe wanawake, waandishi wa habari wa
vyombo binafsi na watu wenye ulemavu.
Nae mwandishi wa redio Jamii Micheweni Time Khamis Mwinyi,
alipendekeza kuwa, lazima Tume iwe na kifungu cha sheria kinachotambua muda wa
majiribio, kwa waanzilishi wa redio na vyombo vya habari mtandaoni.
Mmiliki wa pwani habari tv, Juma Mussa Juma, alipendekeza
kuwa, kama chombo cha habari kimekosea na kuna lazimika kupigwa fani, ianzie
shilingi 100,000 na sio shilingi milioni 1 kama ilivyo sasa.
Akifunga kikao hicho, Mrajisi Tume ya Utangaazaji
Zanzibar Mohamed Said Mohamed, alisema lazima kila jambo, kuwepo ushirikiano
miongoni mwao.
Hata hivyo, amewakumbusha wamiliki wa redio, tv na vyombo
vya habari mtandaoni, kuharakisha ada ya malipo ya mwaka pamoja na malipo ya
leseni zao.
Tume ya Utangaazaji Zanzibar, imeanzishwa chini ya sheria
nambri 7 ya mwaka 1997, ambapo moja ya kazi zake ni kusimamia shughuli za
utangaazaji ikiwemo kutoa leseni.
Mwisho
Comments
Post a Comment