NA ZUHURA JUMA,
PEMBA@@@
Katika majimbo
mengi Unguja na Pemba ni kawaida kusikia malalamiko ya waliochaguliwa
kuingia Baraza la Wawakilishi, Bunge na Udiwani nadra kuonekana, tafauti na
walipohangaika kuchaguliwa.
Hii ilipelekea majimbo mengi kuzorota kimaendeleo kwa vile hapakuwepo
watu waliohangaikia shida zao na kilichosikika ni wananchi kulalamika kwamba
waliowachagua kupeleka mbele madai yao hawaifanyi kazi kama walivyotarajia.
Hali ilianza kubadilika hivi karibuni kutokana na kuibuka wanawake
majasiri na wanaojituma kuhangaikia kero hizi baada ya kushika hatamu za
uongozi katika ngazi mbali mbali.
Wapo watu
waliodiriki kusema laiti zamani kungekuwa na wawakilishi wanawake kama hawa
waliopo sasa, matatizo ya majimbo mengi yangepatiwa ufumbuzi na
yangepungua.
Licha ya kuwepo
viongozi wanawake wachache, lakini kazi waliyoifanya wengi wao ni kubwa na
inathibitisha maelezo ya kwamba siku zote mama huwa na huruma na ndio maana
wawakilishi wanawake wanatumia vizuri fedha za mfuko wa Jimbo na wakati
mwengine wanatoa mifukoni mwao ili kusukuma gurudumu la maendeleo katika
majimbo yao.
Uchache wao haukuwa
sababu wasitekeleze walichowaahidi wananchi na wamejitokeza kusimama kidete
kuhakikisha wanatimiza ndoto za wananchi waliowapa nafasi za uongozi.
Zanzbar inayo wawakilishi
wanawake 29, wakiwemo wanane (8) waliochaguliwa, 18 viti maalumu na watatu (3) wateule wa Rais.
Wote wanafanya kazi
vizuri kwa kila siku kuibua matatizo ya wananchi na kufanya juhudi za kuyapatia
ufumbuzi.
"Kila
nilipoiangalia jamii niliona imeelemewa na mzigo wa changamoto na
walioumia zaidi ni wanawake na watoto na walikosa watetezi.
Nilikuwa naumia na
ndio maana siku moja nikaamua kujitokeza kutaka kuwatetea kwa kuingia jimboni
kugombea,” anasema Zawadi Amour Nassor, mwakilishi wa Jimbo la Konde Pemba.
Alikwenda jimboni
kuchukua fomu ya kugombea akiwa hana tamaa ya kupata kutokana na baadhi ya watu
kumbeza kwa kile walichodai hakuwa na pesa za kuwagaia.
"Nilikuwa
nasikia lazima uwe na pesa ndipo ufanikiwe, lakini niliamua kutafuta mzee mmoja
kupata ushauri, lakini aliniangusha kwa kuniambia niende viti maalumu, lakini
sikuridhia," anaeleza Zawadi.
Alimtafuta mzee
mwengine mwaka 2019 na kumshauri kuchukua fomu ambapo kufanikiwa na sasa
anaendelea kutatua changamoto za wananchi.
Katika kipindi
kifupi cha kuwa mwakilishi ametatua changamoto mbali mbali, ikiwa pamoja na
kuchimba visima vinane.
Anasema, visima
saba kati ya hivyo viligharimu shilingi milioni 14 kila kimoja na kimoja
ambacho ni kikubwa kiligharimu shilingi milioni 21.
Mwakilishi huyu
anahimiza malezi mazuri ya watoto kwa kutoa elimu na kulizungumzia suala hilo
katika Baraza la Wawakilishi.
Mambo mengine
ambayo anajihusisha nayo ni mpambano dhidi ya dawa za kulevya na udhalilishaji
wa wanawake na watoto.
Vile vile, ameweka
gari ya kubebea wagonjwa na huwasaidia sana akinamama na watoto ambao hupelekwa
hspitali bila ya malipo.
Kwa kutumia fedha za mfuko wa Jimbo alizijengea uzio skuli mbili na kununua eneo la kiwanja katika kijiji cha Kipange ambacho Wizara ya Elimu inawajengea skuli, ili kuwapunguzia watoto masafa marefu ya kwenda skuli.
Pamoja na hayo yote, mwakilishi huyo ametengeneza uwanja wa michezo na kwa sasa wapo katika hatua ya mwisho.
"Tumezipatia jezi timu 26 za mpira na nimezisajili kwa kutumia zaidi ya shilingi milioni nne, kwa sasa timu hizi zinashiriki ligi kuu, vile vile nimewapatia mafunzo waendesha bodaboda 43 kwa gharama zangu, ili kuwasaidia kujiepusha na ajali’’, aliongeza.
Mafanikio yake mengine ni pamoja na kuitengeneza skuli yamaandalizi ya Makangale, ili kutimiza ahadi aliyitoa wakati akiomba kura.
Maryam Thani Juma, mwakilishi wa Jimbo la Gando, anasema alichukuwa fomu ya kugombea katika uchaguzi wa mwaka 2015.
Anaeleza,
alishawishiwa na mumewe kugombea uongozi baada ya kuona nafasi nyingi
zinachukuliwa na wanaume, huku utetezi ukiwa mdogo katika kushughulikia masuala
ya maendeleo katika Jimbo.
Wakati akiwa
barazani amekuwa akitetea mambo mengi na mafanikio yaliyopatikana ni pamoja na
kujengwa kwa skuli ya ghorofa iliyopo Kizimbani, hospitali ya Wilaya Kinyasini,
ujenzi wa tangi la maji Raha, uchimbaji wa visima Junguni na barabara za ndani.
Alizitumia fedha za
mfuko wa jimbo kukarabati madarasa na vyoo vya skuli mbali mbali, kujenga
mabanda mawili ya skuli ya maandalizi Kwale Mpona.
Vile vile alichimba
visima vinne katika Jimbo lake, ambapo vitatu ni kupitia fedha za wahisani na
kimoja kwa kutumia fedha zake mwenyewe.
Alivipatia vikundi
nane vya wanawake wajasiriamali zana za kufanyia kazi na fedha kwa kila kikundi
laki mbili, ambapo wengine aliwadhamini kuchukua mkopo benki ya CRDB na mwisho
wa siku kulipa yeye.
Alifanya kombe kwa wanamichezo na kutumia zaidi ya shilingi milioni nne katika kuziendeleza timu za mpira na pia alichezesha ligi ya mbuzi kwa gharama zake mwenyewe.
Baadhi ya mambo aliyoyafanya Mwakilishi wa Jimbo la Chambani
Bahati Khamis Kombo katika kuling’arisha jimbo lake ni, kujenga skuli za
maandalizi Chumbageni, Pujini na Chambani.
‘’Pia nimejenga madarasa na kuezeka skuli za msingi Wambaa,
Ukutini na Dodo ambapo katika skuli ya Dodo pia nimekarabati vyumba vyengine
vinne na stoo kwa kutia saruji na plasta,’’ anasema.
Mwakilishi huyo aliweka kifusi kwenye barabara za Wambaa-
Kwaazani sokoni, alichimba kisima kwa ajili ya wananchi na wanafunzi wa skuli
ya Ukutini, kulaza mipira ya kusambazia huduma ya maji safi na salama, pamoja
na kufikisha huduma ya umeme kijiji cha Kwaazani.
Alijenga barabara ya kijiji cha Kumvini- Kibaridi kwa
kiwango cha lami, kusimamia ujenzi wa barabara kuu ya Ole –Kengeja na vituo vya
mama na mtoto, ambapo hutumia fedha za mfuko wa jimbo na fedha zake kuhakikisha
maendeleo yanapatikana.
CHANGAMOTO
WALIZOKUMBANA NAZO WAKATI WA KUGOMBEA.
Ni baadhi ya watu kuwatia hofu na woga kwani wao walichukulia kuwa ni kitu kikubwa na hakiwezekani kufanywa na wanawake.
Kuvunjwa moyo na kuambiwa kuwa hawawezi kufanya chochote kutokana na maumbile yao ya kike, jambo ambalo sio sahihi kwani wameweza na wanaendelea kuwatumikia wananchi wao.
Mwakilishi wa Jimbo la Konde yeye alikerwa na baadhi ya marafiki na vipenzi vyake walivyobadilika nyoyo zao na kuwa zaidi ya nyoka, kutokana na tamaa ya pesa zaidi kuliko utu na ihsan.
Mwakilishi wa Jimbo
la Gando anahadithia wanaume walitumia kigezo cha dini kuwakataza wanawake kuwa
viongozi, ingawa yeye alikuwa anawatolea mifano hai ya wanawake wa kiislamu
walioongoza enzi za manabii.
NINI KIFANYIKE
Wanawashirikisha wananchi katika kuibua na kutatua changamoto mbali mbali zinazowakabili na ndio maana wanafanikiwa katika kutekeleza yale waliyojipangia kuyafanya.
"Unaposikiliza
kero za wananchi na kuzitatua basi unapungukiwa kubezwa na kuonekana huna
thamani, hivyo tunajivunia kuaminiwa katika majimbo yetu," anasema
mwakilishi Zawadi Amour Nassor.
Ili kuondosha migogoro kwa wananchi ni vyema wachukue juhudi ya kuwasikiliza na kuwaondolea matatizo katika vijiji vyao, watumie fedha za mfuko wa Jimbo kupeleka maendeleo kwani uwezo wa kusaidia wanao.
ASASI ZA KIRAIA
Mratibu wa TAMWA Pemba Fat-hiya Mussa Said anasema, wana mpango mkubwa wa kuwajengea uwezo wanawake na jamii, ili wawe na muelekeo chanya kushiriki kwenye vyombo vya maamuzi.
“Na tumeona kwamba
wanawake wengi waligombea katika chaguzi zilizopita, ingawa hawakushinda wote
lakini walionesha moyo mzuri na walioshinda wanaendelea kufanya vizuri katika
majimbo yao,” anaeleza.
Kwa Pemba, TAMWA
imeshawapatia mafunzo wanawake 70 wenye nia ya kugombea na wamewaunganisha na
wanawake mashujaa ambao tayari wameshagombea nafasi mbali mbali, ili kuwajengea
uzoefu na kuwatoa hofu.
Hafidh Abdi Said ambae ni Mkurugenzi wa PEGAO anaeleza, wanawake wachache wanaokaa katika nafasi za uongozi, wanaonekana juhudi kubwa wanazozifanya katika kutekeleza majukumu yao.
WANANCHI
Wanasema kuwa, wapo
tayari majimbo yote yachukuliwe na wanawake kutokana na utendaji wao wa kazi
pamoja na kuwatatulia shida zao.
"Kwa vyovyote
vile mwanamke ana huruma, hivyo wanajitahidi kutekeleza zile ahadi
walizozichukua kwa vitendo, hilo limetufanya tuwapende," wanaeleza
wananchi hao.
Hassan Salim Ali
mkaazi wa Kizimbani Wete anasema, wawakilishi wanawake wamekuwa mstari wa mbele
katika kuisaidia jamii kuwa na maendeleo, hivyo ni muhimu kuwepo hata katika
majimbo yote.
"Mimi naona
tulichelewa sana kutambua hili, lakini tungejua mapema naona majimbo yote
tungechukua sisi, mwakilishi wetu anajitutumua kwa kweli kutatua matatizo yetu,
anahitaji pongezi," Asha Suleiman mkaazi wa Kiuyu kwa Manda.
Wingi wa wanawake
waliopo nchini haujawawezesha usawa wa jinsia katika nafasi za uongozi
zinazotokana na uchaguzi ili kufikia 50 kwa 50.
Kwani mwaka 2020 wanawake walioingia katika Baraza la Wawakilishi ni 29 kati ya 75 ya wawakilishi wote huku wanaume wakiwa 46.
Ambapo wanawake
waliogombea ni 61 na walioshinda ni nane (8), huku wanaume waliogombea wakiwa
190 na walioshinda ni 42.
Kwa mujibu wa tume ya uchaguzi Zanzibar, wanawake walioingia Baraza la Wawakilishi mwaka 2015 ni 28 sawa na asilimia 36, kati ya wawakilishi wote 84.
Kutokana na idadi hiyo inaonesha dhahiri kwamba elimu imewafikia ipasavyo wanajamii na wanawake katika ushiriki wa wanawake kwenye uongozi na ndio maana idadi inaongezeka.
Kwa kutambua umuhimu wa mwanamke,
sera na sheria mbali mbali za Zanzibar zimeeleza kuhusu haki ya wanawake
kushiriki katika demokrasia na uongozi.
Kifungu cha 21 (2) cha Katiba ya
Zanzibar ya mwaka 64 kimeeleza kwamba, kila mzanzibari anayo haki na uhuru wa
kushiriki kikamilifu katika kufikia uamuzi juu ya mambo yanayomuhusu mwanamke
na taifa lake.
Katiba ya Zanzibar mwaka 1964
iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2010 imeeleza wazi katika kifungu nambari 67 (1)
kuwa, kutakuwa na wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wanawake kwa idadi ya asilimia
40 ya wajumbe wote wa kuchaguliwa katika majimbo.
MWISHO.
Comments
Post a Comment